Samia ateua watendaji wa mahakama, mteuliwa atoa ujumbe
Muktasari:
- Rais Samia amefanya uteuzi mwingine wa watendaji wa Mahakama ya Tanzania katika ngazi ya ujaji na wasajili wa Mahakama, hatua inayolenga kuimarisha utendaji kazi wa mhimili huo wenye dhamana ya kusimamia na kutoa haki, huku Jaji mteule Kainda akitoa ujumbe wa matumaini kwa umma.
Dar es Salaam. Jaji Mteule wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Sylvester Kainda amewataka Watanzania kuendelea kujenga imani kwa Mahakama na kuwa na utaratibu wa kujielimisha kwa masuala mbalimbali ya kisheria na taratibu za kimahakama ili wasiporwe haki zao.
Jaji Mteule Kainda ametoa wito huo leo Jumatano, Aprili 3, 2024, wakati akizungumza na Mwananchi kuhusu uteuzi wake wa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu.
Kainda ameteuliwa saa chache zilizopita na Rais Samia Suluhu Hassan. Kabla ya uteuzi huo, Kainda alikuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani na pia Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.
Wengine walioteuliwa na Rais Samia ni Eva Kiaki Nky aliyeteuliwa kuwa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Wilbert Chuma aliyeteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Septemba 2023.
Kabla ya uteuzi huo Nkya alikuwa Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria, Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Pia, Rais Samia amemteua Chiganga Mashauri Tengwa kuwa Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, nafasi iliyoachwa wazi na Sharmillah Said Sarwat, ambaye pia aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Septemba, 2023.
Kabla ya uteuzi huo, Tengwa alikuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita.
Katika wito wake kufuatia uteuzi huo, Jaji mteule Kainda amewataka kwanza wananchi kuendelea kuwa na imani akisema bado kuna mtizamo mbaya kwani huko nyuma kweli kulikuwa na kunyoosheana vidole lakini kwa sasa Mahakama ya Tanzania imefanya maboresho makubwa na mambo yamebadilika sana.
“La pili wananchi wajizoeze kujielimisha kuhusu sheria na taratibu za Mahakama kwani wengi huwa wanajikuta wanapoteza haki zao hata kwa kutokujua hata mambo ya kawaida tu ya kisheria na taratibu za Mahakama,” amesema na kufafanua:
“Mfano mtu kesi yake inaamuriwa huko ngazi ya chini ya Mahakama kama hakutendewa haki anabaki ananung’unika kwa sababu hajui kuna hatua gani zaidi anapaswa kuzichukua. Yaani kuna wengine hawajui kuwa kuna kukata rufaa katika ngazi nyingine ya mahakama.”
Akizungumzia uteuzi huo, Jaji mteule Kainda ambaye amekuwa mtumishi wa Mahakama kwa muda mrefu katika ngazi mbalimbali amesema uteuzi ni dhamana inayotolewa na mkuu wa watumishi wote wa umma ni Rais.
Amesema ameupokea utumishi huo kwa mikono miwili kwa kuwa Rais ndiye anayejua kwamba nani anafaa wapi na atamsaidia wapi na kwa wakati gani.
“Kwa hiyo kwa kuwa utumishi wa umma ni dhamana, basi mtumishi unakuwa uko tayari kwa wakati wowote kufanya kazi kokote kwa sababu ni mtumishi wa wananchi. Kule ambako Mheshimiwa Rais anaona utamsaidia anakupeleka, unaupokea kwa mikono miwili.”
Amesema uteuzi huo ni hatua ya Rais kuonesha nafasi ya Mahakama ili kuona kila mtu anapata haki, kwa kuwa mahakama inadhama na mchango mkubwa katika kudumisha amani.
“Kwa hiyo wito kwangu ni kukidhi matarajio ya wananchi yale wanayoyatarajia kutoka kwa mahakama, na hili ni jambo ambalo Jaji Mkuu amekuwa akilisisitiza sana kwamba watumishi sisi wote hatimaye mwajiri wetu ni wananchi hawa tunaowatumikia,” amesema Jaji mteule Kainda.
Amesisitiza jukumu lao ni kutenda haki kwa kuwa Katiba imeipa mahakama jukumu la kutafsiri sheria na kwmaba hiyo maana yake ni kukidhi matarajio ya wananchi, kwa sababu kama mahakama ikishindwa kutimiza jukumu lake hata mihimili mingine kazi zao zote zitakwama.
Kabla ya kuingia katika utumishi wa Mahakama, Kainda alianza kufanya kazi Serikali za Mitaa, akiwa mwanasheria wa Halmashauri kwa miaka takribani mitano na baadaye akaingia katika utumishi wa Mahakama kama hakimu mkazi kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2005.
Baadaye aliteuliwa kuwa Hakimu Mfawidhi wa Wilaya nafasi aliyohudumu kwa miaka sita kisha akawa Hakimu Mfawidhi wa Mkoa kwa miaka mitatu na baadaye akateuliwa kuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi kwa miaka mitatu.
Kisha aliteuliwa kuwa Naibu Msajili Mahama ya Rufani kwa miaka miwili, halafu akarudi tena Mahakama Kuu ambako aliteuliwa kuwa Naibu Msajili Mahakama Kuu Morogoro kwa miaka miwili kabla ya Rais akamteu kuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani hadi alipoteuliwa leo kuwa Jaji wa Mahakama Kuu.
Kwa upande wake, Nkya pia aliwahi hakimu wa Mahakama mbalimbali ikiwemo Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Dar es Salaam, Kisutu, ambapo pamoja na kesi nyingine alizozisikiliza akiwa hapo ni kesi za wizi wa Fedha katika Akaunti ya EPA, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania.
Pia aliwahi kuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Dar es Salaam kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi hadi alipoteuliwa leo kuwa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.