Rais Samia ateua majaji 24, Naibu AG na Katibu Mkuu

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan
Muktasari:
- Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu ya Tanzania, Zuhura Yunus ametoa taarifa kwa umma kuhusu uteuzi uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan wa viongozi mbalimbali wakiwemo majaji 24 na naibu mwanasheria mkuu wa serikali.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali akiwemo naibu mwanasheria mkuu wa serikali (DAG), katibu mkuu, balozi na majaji 24 wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu.
Uteuzi huo umetangazwa saa 4 usiku wa Jumapili, Septemba 3, 2023 kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na Zuhura Yunus, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu ya Tanzania.
“Rais Samia amemteua Balozi Stephen Mbundi kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Aidha amemteua Balozi Said Mussa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo,”imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Pia amemteua Profesa Kennedy Gastom kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kabla ya uteuzi huo Profesa Gastom alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki naye anaenda kuchukua nafasi ya Dk Evaristo Longopa ambaye ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu.
Katika uteuzi huo Rais Samia ameteua Majaji wa Mahakama ya Rufani wanne na Majaji wa Mahakama Kuu 20.


