Samia, Mwinyi waigiza filamu ya ‘Amazing Tanzania’

Rais Samia Suluhu Hassan (wa tatu kushoto) na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi (kulia)

Muktasari:

 Idadi ya watalii wa ndani imeongezeka kutoka 788,933 mwaka 2021 hadi watalii milioni 2.4 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 199.5.

Dodoma. Serikali imesema kutokana na mafanikio ya filamu ya ‘The Royal Tour’, imeandaa nyingine yenye hadhi ya kimataifa ya kutangaza utalii ya ‘Amazing Tanzania,’ iliyolenga soko la China.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kwenye hotuba yake bungeni leo Jumatano Aprili 3, 2024, amesema filamu ya ‘Amazing Tanzania’ imewashirikisha Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi na mchezaji filamu nguli kutoka nchini China, Jin Dong.

Amesema filamu hiyo imeandaliwa kwa lengo la kuvutia watalii hususani kwa soko la China na inatarajiwa kuzinduliwa Mei, 2024.

“Mwaka 2023 tumeshuhudia ongezeko la idadi ya watalii wa kimataifa kutoka 1,454,920 mwaka 2022 hadi kufikia watalii 1,808,205 mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 8.4.,” amesema.

“Mapato ya utalii yameongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 2.53 mwaka 2022 hadi kufikia Dola bilioni 3.37 mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 33.5,” amesema.

Waziri Mkuu amesema, “Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kutangaza utalii ndani na nje ya nchi ili kuongeza mapato yatokanayo na utalii.”

Amesema katika jitihada za kulinda bioanuai ya hifadhi na kuboresha maisha ya wananchi wanaoishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, Serikali imeendelea kuwahamisha kwa hiari wananchi kutoka ndani ya eneo la hifadhi kwenda katika maeneo yaliyotengwa na Serikali ya Msomera wilayani Handeni, Saunyi (Kilindi), Kitwai (Simanjiro) na maeneo mengine ambayo wananchi wamechagua.

Amesema katika awamu ya pili, jumla ya nyumba 5,000 zinajengwa katika maeneo ya Msomera (2,500), Saunyi (1,000) na Kitwai (1,500).

Amesema katika kipindi cha kuanzia Julai 2023 hadi 21 Februari 2024, jumla ya nyumba 700 zimekamilika na zingine 1,800 zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi.

“Katika kipindi cha Julai 2023 hadi Februari 2024 jumla ya kaya 491 zenye watu 3,451 na mifugo 14,599 wamehama kwa hiari, hivyo kufanya jumla ya kaya zilizohamia tangu kuanza kwa zoezi hili Julai 2022 kufikia 1,042, ikijumuisha jumla ya watu 6,461 na mifugo 29,919,” amesema.

Majaliwa amesema katika mwaka 2024/2025 Serikali itaendelea kuibua na kuendeleza mazao ya utalii ya kimkakati ikiwemo utalii wa fukwe, meli, mikutano na matukio, michezo na utamaduni; kuimarisha miundombinu katika maeneo ya hifadhi, kuimarisha matumizi na uhifadhi wa maeneo ya malikale kwa kukarabati majenzi ya kale na kuyatangaza.

Mwaka wa fedha 2022/2023

Majaliwa akiwasilisha taarifa ya ofisi yake ya mapato na matumizi bungeni kwa mwaka wa fedha 2022/2023 amesema filamu ya ‘ The Royal Tour’ ilichangia ongezeko la watalii nchini kutoka 922,692 katika mwaka 2021 hadi kufikia watalii takribani milioni 1.4 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 57.7.

Amesema idadi ya watalii wa ndani imeongezeka kutoka 788,933 mwaka 2021 hadi watalii milioni 2.4 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 199.5.

Amesema Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imeendelea kuwa bora duniani kwa miaka minne mfululizo kuanzia 2019 hadi 2022 imepata tuzo ya dhahabu ya utoaji wa huduma bora iliyotolewa na European Society for Quality Research.

Amesema kwa upande wa Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro, kumekuwa na changamoto ya ongezeko la watu, mifugo, makazi holela na shughuli za kibinadamu hivyo kukosekana kwa uwiano baina ya uhifadhi, ukuzaji wa utalii na maendeleo ya jamii.

“Hali hiyo imekuwa ikitishia uendelevu wa hifadhi na ustawi wa maisha ya watu wanaoishi katika hifadhi hiyo kutokana na sheria za uhifadhi kutoruhusu shughuli nyingi za kiuchumi na kimaendeleo katika eneo hilo.

“Ili kutatua changamoto hiyo, Serikali iliendesha zoezi la hiari la kuondoa makazi na shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi kwa kuhamisha wenyeji waliokuwa tayari kuhama kwenda kwenye maeneo yaliyotengwa,” amesema.

Majaliwa amesema kazi ya kuwahamisha imefanyika kwa umakini na kuzingatia haki za wanaohama.