'Serikali haitaanzisha mapori tengefu kwenye miradi ya maendeleo’
Muktasari:
- .Baadhi ya wafugaji wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wameingiwa na hofu na taharuki ya kuanzishwa mapori tengefu katika makazi yao na maeneo ya malisho.
Simanjiro. Serikali imesema haiwezi kuanzisha mapori tengefu kwenye maeneo ya malisho ya mifugo na makazi ya watu.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Aprili 16, 2024 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Suleiman Serera huku akiwatoa hofu wakazi wa Simanjiro mkoani Manyara.
Serera ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, ameyasema hayo katika tafrija ya kumuaga na kumkaribisha mkuu mpya wa wilaya hiyo, Fakii Lulandala na kuagwa kwake. Tafrija hiyo imefanyika katika mji mdogo wa Orkesumet.
Amesema jamii ya wafugaji wa Simanjiro inapaswa kutambua kuwa Serikali haiwezi kuweka miradi mingi ya maendeleo kwenye maeneo yao, kisha iwafukuze na kuanzisha mapori tengefu.
"Msikubali tu kuambiwa maneno potofu, mjinga akikwambia jambo la kijinga na wewe ukalikubali nawe utakuwa nani,” amesema.
Amewataka baadhi ya viongozi wa eneo hilo kutozusha maneno potofu kuwa Serikali ina mpango wa kuanzia mapori tengefu mapya kwa wafugaji.
Amesema huko ni kutaka kuwatia hofu na taharuki isiyo na sababu.
Serere amesema Serikali imeshatoa fedha nyingi za maendeleo kupitia miradi ya maendeleo, hivyo haitawafukuza watu bali ni maneno potofu.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Lulandala ambaye kitaaluma ni mwalimu, ameomba ushirikiano na wana Simanjiro, ili waweze kufanikisha maendeleo.
"Mimi ni mwalimu, nimefundisha kwa miaka 15 kwenye shule za msingi, sekondari na chuo, hivyo nina uhakika tutafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa," amesema Lulandala.
Katibu wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Amos Shimba amesema ameondoka mchakapazi Dk Serera na kumpokea mchakapazi mpya Lulandala.
"Chama kinakuahidi kukupa ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha utekelezaji wa ilani ya CCM unafanyika inavyopaswa," amesema Shimba.
Ofisa Madini Mkazi (RMO) Mirerani, Nchagwa Chacha amesema baadhi ya wilaya huwa akitoka mwanajeshi anakuja mwanajeshi, ila Simanjiro ipo shwari hivyo anatoka kada anaingia kada.
Mkazi wa kata ya Ngorika, Mokia Ole Mrefu amesema baada ya kuondoka Simanjiro Dk Serera wanatarajiwa kumpa ushirikiano mkuu mpya wa wilaya Lulandala, ili aweze kutimiza wajibu wake ipasavyo.