EBARR yachimba visima zaidi ya 10 kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

Wakazi wa Kijiji cha Mingo katika Wilaya ya Mvomero , Morogoro wakichota maji yanayotoka katika kisima kilichochimbwa kupitia mradi wa EBARR unaotekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.

Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini, (Ecosystem Based Adaptation for Rural Resilience -EBARR), ni mradi unaotekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais na unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira Duniani (Global Environment Facility-GEF) Lengo la mradi ni kuwezesha jamii hasa za vijijini kukabiliana na kujenga uwezo wao wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mradi huu unatekelezwa katika wilaya tano, nne kwa upande wa Tanzania Bara na moja kwa upande wa Zanzibar. Wilaya nne za bara ni Wilaya ya Kishapu ambayo ipo mkoa wa Shinyanga, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Wilaya ya Mvomero iliyopo mkoani Morogoro na Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma. Kwa upande wa Zanzibar, mradi unatekelezwa katika wilaya ya Kaskazini A, Unguja. Mradi huu alianza mwaka 2018/19 na unategemewa kukamilika mwaka 2024.

Mradi huu unatekelezwa katika maeneo yanayokabiliwa na ukame mara kwa mara, maeneo yenye uhaba wa maji, na maeneo ambayo zinaishi jamii za wafugaji, wakulima, na wavuvi ambao hutegemea shughuli hizo kwa ajili ya maisha yao ya kila siku.

Athari za mabadiliko ya tabianchi kama vile ukame au uhaba wa mvua,  ongezeko la joto na  milipuko ya magonjwa, zinaathiri shughuli za wakulima, wafugaji,na wavuvi. Kwa hiyo, mradi huu umelenga hasa kuzisaidia jamii hizo za vijijini kuwa na uwezo wa kuhimili, pamoja na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mratibu wa mradi wa EBARR, Dk James Nyarobi anasema shughuli zinazotekelezwa na mradi huu ni pamoja na kuwezesha upatikanaji wa maji kwa ajili ya shughuli za kilimo cha umwagiliaji, kwa ajili ya mifugo, na pia kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

Kisima kirefu kilichochimbwa na mradi wa EBARR katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma katika Kijiji cha Ng’ambi.

Dk Nyarobi amesema “tumechimba visima takriban 14 kwenye maeneo yote mradi unakotekelezwa. Mpwapwa tumechimba visima vinne, Mvomero tumechimba visima viwili, Simanjiro tumechimba visima viwili, Kaskazini A Unguja tumechimba visima sita na bado shughuli za uchimbaji visima zaidi zinaendelea. Aidha, tumechimba malambo saba katika maeneo ya mradi.” anamalizia kwa kusema kuwa “hii yote ni katika kuhakikisha kuwa tunatatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika maeneo ya mradi.”

Visima vyote vilivyokamailika vinatumikazaidi kwa matumizi ya nyumbani, lakini pia kwa sababu mradi umejenga vitalu-nyumba (green houses) katika maeneo yote hayo,  visima hivi pia vinatumika katika vitalu nyumba kama mashamba darasa ya kuonesha mbinu bora za kilimo cha kutumia maji kidogo kwa kufanya umwagiliaji wa matone. Hivyo wananchi au vikundi vinavyonufaika na mradi huu, vinajifunza pia namna ya kutumia maji kidogo katika kuzalisha mazao kwa mwaka mzima.

Dk Nyarobi alisema kuwa hata kama kisima ni kimoja, katika eneo moja, kinaweza kikatumika kwa shughuli mbalimbali. Wanaweza kufanya shughuli za umwagiliaji mdogo na kuzalisha mazao kama mbogamboga kwa kipindi cha mwaka mzima na yale maji bado yakaweza kutumika kwa matumizi ya nyumbani, na pia wanaweza wakatengeneza birika kwa ajili ya kunyweshea mifugo.

Naye mratibu wa mradi wa EBARR katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Aziz Biiru, amesema wanufaika wa mradi huu sasa wametatua tatizo la kufuata maji umbali mrefu. Ameongeza kuwa,mafunzo ya kilimo cha mbogamboga katika vitalu-nyumba vilivyojengwa pembezoni mwa visima, yamewapa uelewa na mwamko mkubwa wa kilimo cha mbogamboga.

Mradi huu unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF) kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira – UNEP,  na unatekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais Tanzania.