‘Serikali haitafunga mpaka wa Uganda’

Muktasari:
Serikali imesema itajikita katika kutoa elimu kwa umma kuhusu namna ya kujikinga na mlipuko wa Ebola badala ya kufunga mipaka mkoani Kagera.
Bukoba. Serikali imesema itajikita katika kutoa elimu kwa umma kuhusu namna ya kujikinga na mlipuko wa Ebola badala ya kufunga mipaka mkoani Kagera.
Hayo yalielezwa juzi na mkurugenzi msaidizi kitengo cha elimu ya afya kwa umma, Dk Ama Kasangala katika kikao na wadau wa afya mjini Bukoba, kilicholenga kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo.
“Hatuwezi kufunga mipaka kwani kuna shughuli mbalimbali zinaendelea za uzalishaji kwa wananchi, badala yake tutajikita katika kutoa elimu ya jinsi ya kujikinga na virusi hivyo kwa kunawa mikono na maji ya sabuni au kutumia vitakasa mikono na kuepuka safari zisizo za lazima katika nchi zenye ugonjwa wa Ebola” alisema.
Awali, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Ngara Murugwanza, Dk Remmy Andrew alishauri kila mpaka unaoingia Uganda ufungwe kudhibiti mlipuko huo hadi pale maambukizi yatakapopungua.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Dk Issessanda Kaniki alisema katika kudhibiti mlipuko huo, Serikali imeweka maabara tembezi ya kupima virus vya ugonjwa huo iliyofungwa katika Kituo cha Afya Kabyaire kilichopo Wilaya ya Misenyi mkoani humo.
“Mashine iliyofungwa kituo cha Afya Kabyaire baada ya mtu kupimwa virus vya Ebola majibu yanatoka ndani ya saa mbili na wameletwa wataalamu wa afya wanne katika kituo hicho,” alisema Dk Kaniki
Alisema mkoa huo umeandaa hospitali 12 zitakazokuwa zinatoa matibabu ya Ebola ikiwa kuna atakayegundulika na umetenga maeneo maalumu kwa ajili ya kuweka wagonjwa wa Ebola kwenye vituo vyote vya Afya mkoani humo.
Alisema pia kuna gari maalumu la kusafirisha watu watakaobainika na dalili za ugonjwa huo pamoja na zipo karantini zilizotengwa kwenye kila halmashauri ya mkoa huo.