‘Serikali ina kibarua kujibu maswali magumu mwaka 2023’

Muktasari:

  • Mwandishi mkuu wa gazeti la Mwananchi, Elias Msuya Mwandishi mkuu wa gazeti la Mwananchi, Elias Msuya amesema Serikali ina kazi kubwa ya kujibu maswali ya wananchi kuhusu hali ya siasa, hali ngumu ya uchumi na upatikanaji wa huduma za jamii.

Dar es Salaam. Mwandishi mkuu wa gazeti la Mwananchi, Elias Msuya amesema Serikali ina kazi kubwa ya kujibu maswali ya wananchi kuhusu hali ya siasa, hali ngumu ya uchumi na upatikanaji wa huduma za jamii.

Msuya ameyasema hayo leo katika mjadala wa mtandao wa X wenye mada isemayo, “mwaka 2023 ulikuwaje kiuchumi, kisiasa na kiuchumi,” unaoendeshwa na Mwananchi Communications Ltd.

Katika suala la siasa, Msuya ametaja maridhiano ya vyama vya siasa, akieleza jinsi Chadema wanavyoilalamikia CCM kutotekeleza mapendekezo yake, kuibuka kwa mjadala wa uwekezaji na uendelezaji wa bandari na mjadala unaoendelea kuhusu miswada ya Sheria za Uchaguzi, Sheria ya Tume ya Uchaguzi na Sheria ya vyama vya siasa.

“Mjadala wa uwekezaji katika bandari ulionyesha jinsi ambavyo wananchi wamekuwa na mwamko wa kuhoji mambo n ahata baada ya Serikali kupitisha mkataba kati yake na kampuni ya DP World, bado wananchi wameendelea kufuatilia,” amesema.

 Kuhusu miswada wa Sheria za Tume ya Uchaguzi wa mwaka 2023, Sheria za Vyama vya Siasa wa Mwaka 2023 na Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa 2023, amesema;

“Miswaada hiyo imeendelea kupingwa sio vyama vya upinzani tu ila hata wanasheria na wanaharakati na baadhi ya watu binafsi, wakisema haionyeshi dhamira ya kufikia muafaka wa kuimarisha demokrasia,” amesema.

“Kimsingi, tunapomaliza mwaka huu, Serikali inatakiwa kutafuta majibu ya maswali ya wananchi magumu tunapoelekea mwaka 2024 ambao pia tutakuwa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa,” amesema.