Serikali yaja na mkakati uhaba wa mafuta ya kula nchini

Muktasari:

  • Katika kukabiliana na uhaba wa mafuta nchini, Serikali imesema itasambaza mbegu za alizeti katika vyama vyote vya ushirika na kuziwezesha kampuni kubwa za uchakataji kuongeza uzalishaji.

Arusha. Katika kukabiliana na uhaba wa mafuta nchini, Serikali imesema itasambaza mbegu za alizeti katika vyama vyote vya ushirika na kuziwezesha kampuni kubwa za uchakataji kuongeza uzalishaji.

Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda alisema hayo jana, alipokutana na wadau wa kilimo kutoka nchi za Ulaya kujadili namna bora ya kuondokana na vikwazo kwenye sekta ya kilimo.

Aprili mwaka huu, wadau wa bidhaa ya mafuta walilieleza gazeti hili kuwa ongezeko la bei ya mafuta ya kula katika masoko ya kimataifa na gharama za uzalishaji kwa wazalishaji wa ndani ni sababu ya kuadimika kwa bidhaa hiyo nchini.

Hadi mwishoni mwa Mei mwaka huu, dumu la lita tano la mafuta lilikuwa linauzwa Sh39,000 kutoka Sh18,000 iliyokuwa ikitumika takribani miezi minne iliyopita.

Kwa mwaka mahitaji halisi ya mafuta ya kupikia nchini ni tani 570,000 za ujazo na kiasi kinachozalishwa ni tani 205,000, hivyo kuna upungufu wa tani 365,000 ambazo huagizwa kutoka nje ya nchi.

Profesa Mkenda alisema changamoto ya uhaba wa mafuta nchini ichukuliwe kama fursa kwa wakulima wadogo wa ndani kuwekeza katika kilimo cha alizeti ili kuzalisha mafuta kwa wingi.

“Juni 13 mwaka huu tunazindua mkakati wa uzalishaji wa mafuta ya alizeti hapa nchini na ili kufanikisha hili tutatoa mbegu kwenye vyama vyote vya ushirika hapa nchini na wale wenye mashamba makubwa,” alisema Profesa Mkenda.

“Kampuni zinazofanya kazi ya kuchakata mbegu kupata mafuta tutawawezesha kupitia benki zetu hapa nchini ili kuhakikisha tunaongeza uzalishaji wa mafuta ya ndani,” alisema Profesa Mkenda.

Mwekezaji wa Kampuni ya Hortenzia kutoka Ulaya, Rory Nightingale alisema wataendelea kuwekeza nchini na kuita wawekezaji wengine kutoka nje ya nchi baada ya Serikali kuwawekea mazingira mazuri ya kilimo.

“Jana tumesikia bajeti ya Serikali, tumeona namna ilivyotupunguzia kodi wawekezaji hapa nchini na sisi tutaendelea kuwekeza kwa nguvu zote kutokana na mazingira rafiki tuliyowekewa,” alisema Nightingale.