Sh2bil kukarabati Shule ya Ufundi Moshi

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi.

Muktasari:

  • Serikali ya Awamu ya Tano yashukuriwa kwa kutambua umuhimu wa shule kongwe ya Ufundi Moshi ambayo imejengwa wakati wa ukoloni mwaka 1957

Moshi. Serikali inatarajia kutumia zaidi ya Sh2bilioni kukarabati Shule ya Sekondari ya Ufundi Moshi ili kuwezesha mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia.

Shule hiyo ambayo ni miongoni mwa shule kongwe nchini ipo katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Makamu mkuu wa shule hiyo, Zephania Wilson alitoa taarifa hiyo jana kwa Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na kuongeza kuwa ukarabati huo utahusisha jengo la utawala, madarasa 29, maabara tano, mabweni 40 ya wavulana, bweni moja la wasichana, bwalo la chakula, jiko, vyoo pamoja na miundombinu ya majisafi na majitaka.

Kamati hiyo ilifika shuleni hapo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo na kufuatilia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015 -2020.

Wilson alisema kwamba kukarabatiwa kwa shule hiyo, kutachangia ukuaji wa taaluma kwa kuwa awali mazingira ya uchakavu yaliwakatisha tamaa ya kufanya kazi shuleni hapo.

“Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutambua umuhimu wa shule hii kongwe ambayo imejengwa wakati wa ukoloni mwaka 1957 na kutoa fedha za ukarabati. Hali yake ilikuwa ni mbaya na yenye kukatisha tamaa. Walimu tulifanya kazi katika mazingira magumu sana, lakini kwa sasa inavutia na kutoa motisha kufanya kazi,” alisema Wilson.

Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi alisema kwamba kujenga na kufanya ukarabati ni jambo moja ila kinachohitajika kwa sasa kiwango cha taaluma kwa wanafunzi kukua.