Shahidi kesi ya Sabaya aeleza alivyopigwa, kuporwa simu

Shahidi kesi ya Sabaya aeleza alivyopigwa, kuporwa simu

Muktasari:

  • Shahidi wa tatu wa Jamhuri, Ramadhan Rashid (26) na shahidi wa nne, Hadjirin Saad (32), juzi waliieleza mahakama kuwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya aliamuru wapigwe, kupekuliwa na kunyang’anywa simu na baadaye kuwalaza chini.

Arusha. Shahidi wa tatu wa Jamhuri, Ramadhan Rashid (26) na shahidi wa nne, Hadjirin Saad (32), juzi waliieleza mahakama kuwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya aliamuru wapigwe, kupekuliwa na kunyang’anywa simu na baadaye kuwalaza chini.

Wakitoa ushahidi wao mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Odira Amworo, mashahidi hao walidai awali walikuwa wakimtambua Sabaya kupitia runinga kutokana na habari zake kutangazwa mara nyingi.

Shahidi wa tatu, Ayoub alidai kuwa kati ya watu wote aliowakuta dukani, aliweza kumkariri Ole Sabaya kwa kuwa ndiye aliyekuwa akitoa amri ya yeye kupigwa.

Shahidi huyo ambaye alijitambulisha kama mfanyabiashara mdogo maarufu kama machinga, alidai mahakamani hapo kuwa alinyang’anywa vitu hivyo katika duka alilokuwa amekwenda kununua bidhaa, ambapo aliwakuta watu kadhaa ndani ya duka hilo wakiongozwa na Ole Sabaya.

Kesi hiyo unayosikilizwa mfululizo hadi Julai 30 mwaka huu, Jamhuri waliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu Tumaini Kweka, Wakili mwandamizi Abdallah Chavula na Wakili wa Serikali Baraka Mgaya.

Katika shauri hilo la jinai namba 105 la mwaka huu, watuhumiwa wengine ni Sylvester Nyegu na Daniel Mbura ambao wanawakilishwa na mawakili Duncan Oola, Mosses Mahuna, Edmund Ngemela, Sylvester Kahunduka, Fridolin Gwemelo na Jeston Jastin.

Akiongozwa na wakili Mgaya, shahidi huyo alidai kuwa anajishughulisha na biashara ya kuuza neti, mapazia, mashuka na kuwa anafanyia biashara zake katika eneo la Soko la Kilombero, karibu na Shoppers Supermaket.

Shahidi wa nne, Hadjirin Saad akiongozwa na wakili Chavula alisema alikwenda katika duka hilo ambalo ni la kaka yake, Mohamed Saad baada ya kuombwa na kaka yake huyo kwenda kutazama kuna nini.

Alisema alipofika alikuta milango imefungwa ila vitu vingine bado vipo nje, ndipo alifungua na kabla hajaingia alivutwa ndani na kuwakuta Sabaya na watu wengine.

Alisema akiwa na mtoto wake, alianza kuhojiwa amefuata nini, akanyang’anywa simu na kuanza kupekuliwa.

Saad alijibu kuwa aliambiwa na kaka yake afike dukani kwa kuwa kuna shida. Shahidi huyo alisema aliambiwa apige magoti na pembeni aliona watu wengine wamelala chini.

Alidai Sabaya alimweleza kuwa wao ni wahujumu uchumi wanaofanya pia biashara ya kubadilisha fedha za kigeni na kwamba kuna Dola 70,000 zimeibiwa Moshi. Sehemu ya mahojiano shahidi wa tatu na wakili Mgaya ni kama ifuatavyo:

Wakili: Hebu ieleze mahakama hizi bidhaa zako unazouza huwa unazitoa wapi?

Shahidi: Bidhaa hizo nachukua katika maduka ya jumla.

Wakili: Hebu iambie mahakama 9/2/2021 jioni ulikuwa wapi na kitu gani kilitokea?

Shahidi: Tarehe hiyo nakumbuka nilipata mteja alikuwa anataka neti nikawa sina, nikamuomba anisubiri nikachukue bidhaa sehemu ninakochukua. Nikaenda kuchukua neti soko kuu, kufika pale sehemu nachukua mizigo yao kila siku, nikakuta mageti yao ambayo ni ya kushusha na kupanda yamerudishiwa.

Wakili: Unalifahamu linaitwaje?

Shahidi: Nje ya duka wameandika Shahid Store.