Sintofahamu mikoa iliyotajwa kuwa na kipindupindu

Dodoma. Waganga wakuu wa mikoa iliyotajwa kuwa na kipindupindu wamefunguka kuhusu kinachowasibu maeneo yao kutajwa kuwa na ugonjwa huo, huku ukosefu wa vyoo ukitajwa kuwa sababu kuu.

Juzi Waziri wa Nchini Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu George Simbachawene alitangaza kuwa hadi Machi 11, 2023 Tanzania ilikuwa na wagonjwa wa kipindupindu 72, katika baadhi ya mikoa huku vifo vikiwa ni vitatu.

Hata hivyo, takwimu hizo huenda zikawa tofauti baada ya Mkoa wa Rukwa ulioripotiwa kuwa na wagonjwa 18 kukanusha kuwa hawana ugonjwa huo na taarifa kupelekwa wizarani lakini wanashangaa kusikia bado wamewekwa kwenye orodha.

Waziri Simbachawene alitoa taarifa hiyo juzi wakati wa uzinduzi wa Mpango Shirikishi wa Taifa wa kuzuia na kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu hadi ifikapo 2030, kwa kushirikisha wadau mbalimbali yakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali ya ndani na nje.

Baadhi ya mikoa iliyotajwa kuwa na wagonjwa ni Ruvuma 13, Kigoma saba, Katavi 34, na Rukwa wagonjwa 18 lakini Mkoa wa Manyara ulitajwa miongoni mwa iliyokuwa na wagonjwa pia.


Walichosema waganga wa mikoa

Akizungumza jana, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Dk Jesca Lebba alisema tatizo hilo lipo katika wilaya ya Uvinza na kwamba wamekuwa na mkakati wa namna ya kuondoa lakini kinachochangia ni kwa baadhi ya watu wenye utamaduni wa kutotumia vyoo.

Dk Lebba alisema eneo ambako kesi za kipindupindu zimeripotiwa, limekuwa mara kwa mara likikumbwa na ugonjwa huo, licha ya elimu na juhudi kubwa ambazo wameendelea kuzifanya ikiwemo kuhamasisha wananchi kuchimba vyoo na kuvitumia.

Alisema katika eneo hilo ndani ya wilaya ya Uvinza kuna kambi ambayo hawatumii vyoo na kwa hiyo idara yake ilishapeleka mapendekezo serikalini ili kuwaondoa wananchi na kufunga kambi hiyo kwa madai wahusika wanatakiwa kwenda kujifunza kwa wengine.

“Pale kuna kambi za watu ambao hawatumii vyoo kabisa, tumepeleka elimu na kuweka sheria kali lakini hakuna utekelezaji, sasa tumepeleka mapendekezo kwa mamlaka husika wawahamishe wananchi hao na kuzivunja kambi zao ili wakaishi kwa wengine wanaotumia vyoo,” alisema Dk Lebba.

Akizungumzia ugonjwa huo katika Mkoa wa Rukwa, Mkuu wa Mkoa huo, Queen Sendiga alisema hatambui kama mkoani kwake kuna wagonjwa au matukio ya ugonjwa huo, huku akimtaka mwandishi kuwasiliana na mganga mkuu wa mkoa huo.

Mganga Mkuu wa mkoa wa Rukwa Dk Ibrahimu Mwita, alishangazwa kusikia mkoa wake ukiendelea kutajwa wakati alishatoa taarifa wizarani siku nyingi kwamba hakuna sampuli zilizoonyesha kwamba mkoa huo una wagonjwa.

Dk Mwita alisema awali kulikuwa na watu waliohisiwa lakini walipochukua sampuli za vipimo na kuzipeleka kwa Mkemia Mkuu, majibu yalitoka kuwa hakuna ugonjwa huo ndipo akaiandikia wizara na hadi sasa hawana wagonjwa, huku akiomba mkoa huo uongolewe kwenye orodha.

“Sisi hatuna kipindupindu na wala hatukuwahi kuwa nacho niliwaandikia wizara baada ya kufuatilia maeneo yote lakini nashangaa kwa nini hadi leo tunatajwa tena kwamba ni miongoni mwa mikoa yenye shida ya kipindupindu tena, tutawaomba watuondoe,” alisema Dk Mwita.

Katika taarifa ya Waziri Simbachawene ambayo imesambazwa katika vyombo vya habari, moja ya changamoto katika ugonjwa huo ni ukosefu wa maji safi na salama, uelewa mdogo wa namna ya kupambana na kipindupindu,jamii kukosa vyoo bora na matumizi sahihi ya vyoo hivyo.

Simbachawene alisema hadi kufikia Machi mwaka huu nchi ya Malawi ilikuwa na jumla ya wagonjwa 52,167 na vifo 1620 kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ambapo alisema taarifa hiyo inatoa tahadhari ya uwezekano wa ugonjwa huo kuvuka mipaka na kuingia nchini.

Kwenye mkutano huo, Naibu Waziri wa Afya Dk Godwin Mollel alisema, wizara ya afya imejipanga katika hospital za kanda,mkoa hadi ngazi ya zahanati ili kuhakikisha inajikinga na kutokomeza ugonjwa huo.

Mwakilishi wa Shirika la Save the Children Angela Kauleni alisema shirika hilo liko tayari kushirikiana na Serikali kwa ajili ya kupambana na ugonjwa huo, huku akisisitiza kuwa elimu ya matumizi ya vyoo bado ni changamoto kwa wananchi.