Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Taharuki watoto saba wakitoweka nyumbani

Baadhi ya watoto waliotoweka kwao na kuzua taharuki baada ya kurudi.

Muktasari:

  • Watoto wadai walichukuliwa na kijana wasiyemfahamu wakapige ngoma.

Dar es Salaam. Baadhi ya wazazi wakazi wa Kimanga Juu, Bonde la Mchicha wilayani Ilala, wameingiwa taharuki baada ya watoto saba kutoweka kwa muda wa saa tatu pasipo kujua walipoenda.

Watoto hao walitoweka nyumbani jana Februari 21, 2024 saa 11 jioni hadi saa moja usiku waliporejea.

Watoto waliotoweka ni Richard Yaguruza mwenye miaka mitano, Jonson (8), Ikram (7), Ismail Salum (13), Wilson Silvanus (8), Baraka (7) na Ibrahimu (7), wote wakazi wa Bonde la Mchicha.

Wakizungumza na Mwananchi Digital jana Februari 21, 2024 katika eneo hilo, wamesema watoto hao walichukuliwa na kijana aliyejitambulisha kwa jina la Mint Boy akiwaeleza anataka wakampigie ngoma nyumbani kwake.

Richard Yaguruva (5), mwanafunzi wa elimu ya awali katika Shule ya Msingi Jeshini, amesema mtu huyo alienda eneo hilo siku moja kabla ya wao kufika nyumbani kwake.

"Nilimuona siku ile (akimaanisha Jumanne ya Februari 20,2024) alitukuta tunapiga ngoma akasema atakuja kutuchukua tukawaone wazungu na mbwa nyumbani kwake,” amesema Richard na kuongeza:

“Leo (jana Februari 21, 2024) amekuja akatuita ninyi watoto twendeni kwangu tukapige ngoma, tulipofika nyumbani kwake kulikuwa hakuna umeme tukaanza kupiga ngoma na yeye akicheza na kupiga makofi,” amesema.

Wilson Silvanus amesema siku ya kwanza wenzake walipokutana na mtu huyo hakuwapo.

"Mwenzetu alituita akasema tumfuate yule kaka na madumu yetu kwa ajili ya kumpigia ngoma, tulimfuata naye akisaidia kubeba baadhi ya madumu. Tulipofika nyumbani kwake alituambia hakuna umeme lakini tuendelee kupiga ngoma," amesema Wilson.

Ismail Salum, mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Jeshini amesema mtu huyo walikutana naye jioni na aliwasifia kuwa wanajua kupiga ngoma, akiwataka waende kufanya mazoezi nyumbani kwake.

"Alituuliza tunataka kuwa nani tukiwa wakubwa, mimi nikamwambia kwa sasa siwezi kusema kitu, akatuambia tukipata muda tuwe tunaenda kwake  kufanya mazoezi ya kupiga ngoma na endapo hatutafanya mazoezi ya ngoma atatufundisha muziki," amesema.

"Tulipofika kabla ya kuanza kupiga ngoma tuliandikishwa majina na tuliambiwa kila Jumamosi inatakiwa tuende kufanya mazoezi ya kupiga ngoma," amesema Johnson.

Amesema walipomaliza kupiga ngoma walipewa maelekezo kuwa ambaye hatahudhuria mafunzo jina lake litakuwa limekatwa.

Wazazi wazungumza

Agnes Ernest, mama mzazi wa Richard amesema mtoto wake hana tabia ya kucheza mbali, hata alipofikishiwa taarifa za kuondoka kwa mtoto wake alishangaa.

"Nilikuwa nimelala akaja jirani akaniuliza watoto wangu wako wapi, nikamwambia wapo bondeni wanacheza ndipo aliponiambia kuna mtu amewabeba kwenye gari na kuondoka nao," amesema.

Amesema baada ya kupewa taarifa alitoka kumtafuta na hakujua pa kuanzia zaidi ya kulia.

Amesema ushauri uliotolewa ni kwenda polisi, hivyo waligawana wapo walioenda kituo cha polisi External na wengine cha Tabata.

Wakiwa polisi, amesema walipigiwa simu kuwa watoto wamerudi nyumbani lakini kwa wakati tofauti, wakipishana kwa takribani dakika mbili.

Akizungumza pasipo kutaka kujitambulisha jina, jirani wa mama huyo amesema walishangazwa watoto kurudi nyumbani wakipishana maelezo kila mmoja akieleza kitu cha tofauti.

"Sijui huyo kaka kawaambia nini huko, maana kila mtoto anaeleza jambo lake. Wengine wanasema walikuwa wanacheza mpira hawakuwa pamoja," amesema jirani huyo.

Mama mzazi wa Johnson, amesema alipokea taarifa akiwa kibaruani kwake eneo la Posta kuwa watoto  wamechukuliwa na mtu ambaye hawamfahamu ndipo alipopiga simu kwa polisi anayefahamiana naye kumuuliza iwapo kuna wanawake wamefika kituoni kutoa taarifa za kupotea watoto.

"Siku hizi kumekuwa na matukio ya ajabu watoto kutekwa na kulawitiwa kwa hiyo nilivyoambiwa mtoto wangu hayupo nyumbani niliangua kilio nikajua yale ninayoyasoma mitandaoni yamenikuta na mimi,” amesema.

Mjumbe wa Mtaa wa Kimanga Juu, Steve Mwambene amesema alipata taarifa za watoto kutoweka akiwa kwenye msiba mtaani kwake.

Amesema kwa kushirikiana na vijana walifuatilia tukio hilo.

“Tukiwa na harakati za kwenda polisi tukaambiwa watoto wamerudi, tulipowauliza walikuwa wapi walisema walikuwa wanacheza mpira, hivyo hatukuwahoji zaidi,” amesema.

Hata hivyo amesema amekuwa akiwahimiza wazazi kuwa waangalifu na watoto kwa kuwa kumekuwa na matukio ya kutisha kwa sasa.


Polisi kwenye tukio

Askari kutoka Kituo cha Polisi Tabata na wale wa External walimchukua mtoto mmoja kati ya saba wakimtaka awaongoze hadi sehemu waliyopelekwa kupiga ngoma.

Safari ilianza Kimanga Juu eneo la Bonde la Mchicha, wakiwamo polisi sita kwenye gari pamoja na Johnson aliyeongoza msafara hadi Kimanga Buyuni.

Baada ya kutembea umbali kiasi, Johnson aliyekuwa amekaa mbele aliomba gari lisimamishwe watembee kwa mguu.

Kwa maelezo ya Johnson wakienda kwa gari atashindwa kupafahamu kwa kuwa ilikuwa mara yao ya kwanza kwenda na  walipelekwa kwa mguu.

Askari waliridhia na kuanza kutembea. Kutokana na umbali na kona alizokuwa anaongoza mtoto huyo, askari waliingiwa wasiwasi na kujadiliana wakisema huenda atakuwa amesahau njia ikizingatiwa mitaa hiyo kulikuwa na giza baada ya umeme kukatika.

Baada ya kutembea umbali wa dakika 20, Johnson alionyesha geti lenye rangi nyeusi.

Askari waliizingira nyumba hiyo ndipo mlango wa geti uligongwa.

Walikaribishwa na vijana watatu wa kiume waliokuwa wamekaa sebuleni.

Kati ya vijana hao ambao hawakujitambulisha majina, wawili walikuwa hawajavaa mashati, kichwani wakiwa wamesuka nywele na mwingine akiwa amewaka dawa nywele zake na kuzifanya kuwa nyeupe.

Askari mmoja kati ya watatu na Johnson walioingia ndani  aliuwauliza vijana: “Mnamjua mtoto huyu (yaani Johnson?”

Vijana wawili walikaa kimya, na aliporudia kuuliza swali, walijibu hawamjui lakini mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Juma alikubali anamfahamu.

"Huyu mtoto namjua ana kipaji cha kupiga ngoma anaishi mtoni mbele kule," alijibu Juma.

Baada ya kukiri kumfahamu mtoto huyo ndipo askari walimkamata na kuondoka naye hadi Kituo cha Polisi cha Tabata.

Polisi walitoa maelekezo kwa wazazi wa watoto wote saba kuwafikisha polisi leo Februari 22, 2024 watakapokuwa wametoka shuleni.


(Imeandikwa na Devotha Kiwelo na Tuzo Mapunda)