Takukuru Arusha yaokoa miradi ya Sh3.8 bilioni

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo.

Muktasari:

 Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Arusha imekwamua miradi ya elimu yenye thamani ya Sh3.84 bilioni iliyokuwa imekwama.

Arusha. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Arusha imekwamua miradi ya elimu yenye thamani ya Sh3.84 bilioni iliyokuwa imekwama.

Miradi hiyo ni ya nyumba za walimu katika shule mpya ya sekondari ya Kiutu iliyopo kata ya Sekei, jijini Arusha, ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya Orbomba, wilayani Longido na mabweni mawili ya katika sekondari ya Mringa, wilayani Arumeru.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Machi Mosi, 2024, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo amesema wamebaini upungufu katika miradi hiyo walipofuatilia fedha za umma zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi kwa miezi mitatu kuanzia Oktoba hadi Desemba, 2023.

Amesema wamebaini ucheleweshaji wa siku zaidi ya 30 wa mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Kiutu yenye thamani ya Sh3.844 bilioni kinyume cha makubaliano ya mkataba, sambamba na mradi wa ujenzi wa mabweni mawili katika shule ya Sekondari Mringa wenye thamani ya Sh260 milioni.

“Tumekwamua pia mradi wa ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya wasichana Orbomba iliyoko wilayani Longido yenye thamani ya Sh3 bilioni ambao umechelewa kwa siku 15 kinyume cha mkataba,” amesema.

Baada ya kubaini hayo, Zawadi amesema walifanya mawasiliano na wasimamizi wa miradi hiyo ambao ni wakurugenzi wa halmashauri husika ili kuchukua hatua ikiwemo kuharakisha ukamilishwaji wake.

Zawadi amesema wamebaini ucheleweshaji wa utoaji huduma katika sekta ya ardhi, hasa utoaji wa hati miliki zinazotakiwa kutolewa ndani ya siku 14 kwa mujibu wa muongozo lakini zingine huchukua hadi siku 390, hivyo wanaendelea kuchukua hatua dhidi ya hilo.

“Taasisi yetu pia imeendelea kupokea malalamiko kwa njia mbalimbali, kwa miezi hii mitatu tumepokea 89, kati ya hayo 73 yalihusu rushwa na hadi sasa yako katika hatua mbalimbali za uchunguzi. 16 hayakuhusu rushwa hivyo tumefunga majalada hayo,” amesema.

Zawadi amewataka wananchi mkoani Arusha kutoa taarifa za matukio ya rushwa na miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao ili ufuatiliaji ufanyike mapema.

Akizungumzia mradi wa shule ya sekondari Kiutu, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Juma Hamsini amesema  walipokea barua kutoka Takukuru na wameshafanya marekebisho, ikiwemo kukamilisha umaliziaji wa maeneo yaliyokuwa nyuma ya muda.

"Shule hii iliyokuwa inajengwa chini ya mradi wa uboreshaji elimu kwa shule za sekondari (Sequip) kazi iliyokuwa imebaki nyuma ya muda ni uwekaji milango na madirisha katika majengo ya maabara, uwekaji PVC katika maktaba, na mfumo wa maji katika baadhi ya vyoo. Kazi yote imekamilika ndani ya muda waliotutaka," amesema Hamsini.