Tanzania inavyotaka kuingia kwenye chumba kinachokimbiwa na Wakenya

Tanzania inavyotaka kuingia kwenye chumba kinachokimbiwa na Wakenya

Muktasari:

Katika agenda tisa zilizosababisha kuundwa kwa tume ya kusaka maoni ya maridhiano, mradi ukipewa jina la Mpango wa Kujenga Daraja, yaani Building Bridge Initiative (BBI) Kenya, nyingi zinaihusu na Tanzania, lakini ipo kubwa zaidi.

Katika agenda tisa zilizosababisha kuundwa kwa tume ya kusaka maoni ya maridhiano, mradi ukipewa jina la Mpango wa Kujenga Daraja, yaani Building Bridge Initiative (BBI) Kenya, nyingi zinaihusu na Tanzania, lakini ipo kubwa zaidi.

Moja ya agenda ambazo zilibebwa ili kuzitafutia ufumbuzi ni “Jinsi ya kushughulikia ukosefu wa moyo wa utaifa kwa wananchi.”

Dhahiri, ilionekana Wakenya hawana moyo wa utaifa. Mgawanyiko ni mkubwa kuanzia wa kikabila, kidini mpaka wa kisiasa.

Wakenya wamekuwa hawana uzalendo na taifa lao, badala yake hisia za ukabila, udini na siasa wanaziweka mbele zaidi.

Hilo na mengine manane, yaliwaumiza sana vichwa Rais Uhuru Kenyatta na mpinzani wake, Raila Odinga ya namna gani wanaweza kuifanya Kenya irudi kuwa moja na Wakenya wawe wazalendo kwa nchi yao.

Machi 2018, Uhuru na Raila walishikana mikono na kukubaliana kuanza mwanzo mpya wa kuijenga nchi yao bila migawanyiko ya kisiasa, ukabila na matabaka.

Unaweza kutafsiri kuwa Machi 2018, ilikuwa mwanzo wa mapambano ya Wakenya kujinasua katika hali ya mgawanyiko hadi watu kukosa uzalendo kwa nchi yao.

Kwa vile bado BBI haijafika mwisho, ni wazi mapambano hayo yanaendelea.

Na kwa kuwa si kila mtu Kenya anaunga mkono BBI, ni sahihi kusema mapambano si mepesi. Safari ya kwenda kufanya mabadiliko ya kikatiba kuruhusu mfumo wa nchi kulingana na maoni yaliyochakatwa na BBI, bado mbichi. Hata hivyo, kwa imani watashinda.

Watanzania wanapoingilia

Wakati Wakenya wapo kwenye mapambano ya kutibu mgawanyiko na kurejesha moyo wa uzalendo kwa nchi yao, Baadhi ya Watanzania wanataka nchi iingie kule ambako Kenya wanajaribu kujinasua.

Ni dhahiri baadhi yoa siasa zinawafanya wakose uzalendo kwa taifa lao. Mfano wa karibu, Kamati ya Mambo ya Kimataifa ya Bunge la Ulaya, hivi karibuni ilijadili mapendekezo ya kuifutia Tanzania misaada na mikopo, sababu ikitajwa ni ukiukwaji wa demokrasia.

Vilevile ilihojiwa kuwa Tanzania ilipataje msaada wa fedha euro 27 milioni (Sh75 bilioni) za Covid-19, wakati ilijitangaza haina ugonjwa huo?

Kutoka Bunge la Ulaya, mjadala ukahamia kwenye mitandao ya kijamii Tanzania. Bila kupepesa macho, Watanzania wengi walionyesha kufurahishwa na taarifa hiyo. Wanatamani kuona nchi yao haikopeshwi wala haipewi misaada. Kuna waliodiriki kuombea vikwazo kwa nchi.

Si kwamba wenye kuomba vikwazo hawapo Tanzania, la! Tatizo ni kuwa hisia za mgawanyiko zimekuwa kubwa kiasi kwamba wanahisi vikwazo vikiwekwa wao hawataakisi.

Wanadhani wataumia wengine. Hivyo ndivyo Watanzania wanapoteza moyo wa uzalendo.

Unaweza kuiweka hoja yako hivi; Wakenya baada ya kuishi kwenye mgawanyiko kwa muda mrefu, sasa wanatamani kuwa taifa moja lenye watu wazalendo kwa nchi yao. Na wanapambana kutimiza hilo. Watanzania baada ya kuishi kwa umoja miaka mingi sasa wanaombea mgawanyiko. Tena wanafurahia, ajabu sana!

Hukosei ukisema chumba ambacho Wakenya wanapambana watoke. Chumba cha mgawanyiko. Waingie chumba cha umoja. Chumba hicho cha mgawanyiko ndicho baadhi ya Watanzania wanakitaka ili waingie. Chumba cha uzalendo na umoja wanakiasi wakifurahia.

Nani wa kuirejesha nchi mstarini?

Shujaa wa Uingereza, aliyeiongoza nchi hiyo kushinda vita vingi kabla kuuawa katika vita ya Napoleon, Horatio Nelson alipata kusema: “Uingereza inatarajia kila mmoja atatimiza wajibu wake.”

Hivyo, ni wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha Tanzania inabaki ileile ya umoja na watu wake wanaendelea kuwa wazalendo.

Haitakiwi wawepo watu wa kusema wengine wafanye. Tanzania inatarajia kila Mtanzania atatimiza wajibu wake.

Katika siku za mwisho za kuelekea uhai wake, Balozi Job Lusinde, waziri wa mwisho kufariki dunia katika Baraza la Mawaziri la kwanza la Tanganyika, alisema akimshukuru Mungu kwa uhai mrefu, halafu akaeleza kuwa aliamini Mungu alimuacha hai ili asaidie kuwaweka sawa viongozi vijana pale ambapo wangepotoka. Vilevile kukumbusha nchi ilipotoka.

Balozi Lusinde hayupo hai, ila maneno yake yanaishi hata sasa. Kwamba viongozi wastaafu tulionao leo, wanao wajibu wa kuiweka sawa nchi pale wanapoona haiendi vizuri, vilevile kukumbusha mahali ambapo nchi ilitoka.

Marais wastaafu, mawaziri wakuu na viongozi wengine ambao hawapo kwenye jukwaa la siasa, wanapaswa kutazama picha ilivyo na kuisema katika namna ya kujenga. Hivyo ndivyo kutimiza wajibu kama alivyosema Horatio Nelson, ndicho alimaanisha Balozi Lusinde kuwa ukiwa mzee kwenye nchi, unakuwa na jukumu la kushauri vijana, kuiweka sawa nchi, vilevile kukumbusha misingi ya nchi na ujenzi wake kupitia historia.

Wakenya wanavyojisahihisha

Machafuko au migogoro yenye kuibuka mara kwa mara kipindi cha uchaguzi ni sababu ya Uhuru na Raila kuketi, kama Wakenya, wenye kuipenda Kenya na kuitakia kesho njema, wakazungumza na kuzika tofauti zao kisha kupata mawazo yaliyofanikisha ripoti ya BBI.

Baada ya mazungumzo ya Uhuru na Raila, kiliundwa kikosi kazi cha wajumbe 14, kikapewa agenda tisa.

Kikazunguka majimbo 47 ya Kenya ili kupata mawazo ya namna Wakenya wangependa nchi yao iwe.

Agenda tisa ni mosi; jinsi ya kumaliza mgawanyiko wa kikabila. Pili; ushirikishwaji wa vyama vya upinzani katika muundo wa Serikali, tatu; jinsi ya kutatua misuguano ya uchaguzi, nne; ulinzi na usalama, tano; namna ya kupambana na rushwa.

Sita ni jinsi ya kushughulikia ukosefu wa moyo wa utaifa kwa wananchi, saba; haki na uwajibikaji, nane; mgawanyo sawa wa matunda ya nchi na tisa; ni kutanua nguvu ya mamlaka kwa wananchi na uwakilishi.

Agenda hizo zilisababisha kikosi kazi cha BBI kije na mapendekezo ya mabadiliko ya vifungu vya Katiba ya Kenya ya mwaka 2010, vipo vinapendekezwa vifutwe, vingine kubadilishwa matamshi na vipo vitakavyoongezwa.

Kwanza ni pendekezo la kuwa na Rais wa muhula mmoja wa miaka saba, bila nyongeza. Ukurasa wa 19 wa ripoti ya BBI utetezi wa hoja hiyo umetolewa kwa mifano dhahiri na kwa hakika inaeleweka na kuridhisha.

Wanataka Rais akiingia madarakani asiwe na nafasi ya kugombea muhula wa pili, kwamba kihistoria, kila mara Rais aliye madarakani anapogombea muhula wa pili, ndipo migogoro na machafuko hutokea.

Wametoa mifano ya ghasia za uchaguzi 1991/92 na 1997 kipindi Daniel Moi alipokuwa akigombea kuongeza muhula wa uongozi, machafuko ya mwaka 2007/8 Mwai Kibaki alipogombea muhula wa pili, vilevile mivutano na uchaguzi kurudiwa mara mbili mwaka 2017 Uhuru alipogombea muhula wa pili.

Mifano mingine ni hali ya amani ilivyokuwa mwaka 2002 na 2013. Ni kipimo kuwa marais wawapo madarakani husababisha ghasia kwa kutaka ushindi wa kufa au kupona.

Ipo hoja nyingine ya matumizi ya fedha. Kwamba Rais aliye madarakani anapokuwa anagombea kuongeza muhula wa uongozi, hujiwezesha kwa fedha za umma ili kugharamia uchaguzi.

Sababu ya msingi nyingine ni kuwa Rais anapokuwa ana matarajio ya kuwania muhula wa pili, miaka miwili ya kwanza anapoingia madarakani huitumia kulipa fadhila kwa waliomsaidia na mitatu inayofuata hujifanyia maandalizi ya uchaguzi, hivyo muda wa kutoa huduma huwa mdogo.

Rais wa Kenya hatakuwa mtendaji, bali mkuu wa nchi mwenye wajibu wa kuliunganisha Taifa. Rais atateua Waziri Mkuu kutoka kwenye chama chenye wabunge wengi. Waziri Mkuu ndiye atakuwa Mkuu wa Serikali.

Hiyo ni tafsiri kuwa Kenya inahama kutoka kwenye muundo wa Serikali ya Urais kama ilivyokuwa na kupewa mkazo na Katiba ya mwaka 2010, sasa inakaribisha muundo wa Serikali ya Bunge.

Waziri Mkuu atakuwa na manaibu watatu ambao watashirikiana kuendesha Serikali. Kati ya hao watatu, wawili ni kutoka vyama vya upinzani.

Kwa maana hiyo, Kenya hakutakuwa na siasa za kutoana roho, kwa sababu wanaoshinda na wanaoshindwa watakwenda kushirikiana kuihudumia nchi.