Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Tuliahidiwa kulipwa Sh17 milioni kila mmoja’ nilipanda gari ya Msuya’

Muktasari:

  • Jana tulikuletea ushahidi wa shahidi wa 10 wa upande wa Jamhuri, Sajenti Atway ambaye ni miongoni mwa makachero waliokuwa chini ya Inspekta Maimu, ambao jukumu la timu yao ilikuwa kuwasaka na kukamata wauaji wa Bilionea Msuya.

Jana tulikuletea ushahidi wa shahidi wa 10 wa upande wa Jamhuri, Sajenti Atway ambaye ni miongoni mwa makachero waliokuwa chini ya Inspekta Maimu, ambao jukumu la timu yao ilikuwa kuwasaka na kukamata wauaji wa Bilionea Msuya.

Katika simulizi yake alielezea namna Oktoba 5, 2013 walivyomkamata mshtakiwa wa 7, Ally Mussa maarufu ‘Mjeshi’ ambapo alimpeleka mahabusu katika kituo cha Polisi Kigoma na baadae akapewa jukumu la kuandika maelezo yake.

Baada ya kueleza hivyo, wakili mwandamizi wa Serikali, Abdalah Chavula, alimuomba Jaji atoe amri ya wazee washauri wa mahakama kuondoka ndani ya chumba cha mahakama akisema kuna hoja za kisheria zinatarajia kuibuka.

Akiendelea kuongozwa na wakili wa Serikali, Kassim Nassir, shahidi huyo alisema baada ya kupewa kazi ya kuandika maelezo hayo, alitafuta chumba chenye nafasi na kuandaa karatasi na kalamu na kwamba hakuwa na silaha yoyote wakati huo.

“Baadae nilikwenda mahabusu na kumchukua mtuhumiwa na kumleta katika chumba nilichoandaa kwa mahojiano. Tulikuwa wawili tu. Hapo nilijitambulisha naitwa sajenti Atway na niko pale kwa ajili ya kuandika maelezo yake ya onyo,” alieleza.

Baada ya kumuonya na kumpa haki zake zote, alianza kuandika maelezo hayo saa 2:30 asubuhi na kazi hiyo ilichukua takribani saa tatu na baada ya kumaliza alimsomea maelezo hayo na kukubali ni maelezo yake na kusaini na yeye kusaini.

“Nikiona hayo maelezo nitayatambua kwa sababu yana mwandiko wangu na ya na majina matatu ya mshtakiwa, kuna tarehe ambayo ni 5.10.2013 na yana saini ya Ally Majeshi. Ninaomba kuyatoa maelezo hayo kama kielelezo,” alisema Atway.

Mawakili wavutana kortini

Wakili Lundu alipinga kutolewa kwa maelezo hayo, akisema mteja wake anasema aliteswa mara tu baada ya kukamatwa na wakati anahojiwa aliteswa na pia shahidi hakuzingatia sheria wakati akichukua maelezo hayo kutoka kwa Majeshi.

Akijibu hoja hiyo na nyingine, wakili Chavula alisema ni msimamo wa sheria kuwa pale suala la kutoa au kutotoa maelezo kwa hiyari linapojitokeza ili kufanya kesi ndani ya kesi (trial within trial) kupima kama yalichukuliwa kwa hiyari ama la.

Hata hivyo katika uamuzi wake mdogo, Jaji Maghimbi, aliamuru kufanyika kwa kesi ndani ya kesi na baada ya kesi hiyo maahakama ilikubali kupokea kielelezo hicho ambapo shahidi huyo alitakiwa kusoma maelezo hayo neno kwa neno.

Malipo ya Sh17 milioni

Akisoma maelezo hayo, shahidi ambaye ndiye aliyeyaandika akiwa kituo cha Polisi Kigoma, Oktoba 5, 2013, alisema mshtakiwa alimueleza waliahidiwa kulipwa Sh17 milioni kila mmoja kwa kumuua Bilionea Msuya.

Kwa mujibu wa maelezo hayo, mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Sharifu Mohamed, ndiye aliyesimamia mpango huo na ndiye aliyewakodi kwa ahadi ya kuwalipa kiasi hicho.

Mshtakiwa huyo amenukuliwa akisema Agosti 2013 akiwa nyumbani kwake Babati, alipigiwa simu na mshtakiwa wa pili Shaibu Jumanne akimtaka aende Jijini Arusha, ambapo alikutana na Sharifu, Shwaibu na Jalila.

Siku iliyofuata aliongezeka mshtakiwa wa sita, Sadik Mohamed ‘Msudan’ ambapo Sharfu aliwajulisha juu ya mpango wa kumuua mfanyabiashara huyo.

Katika maelezo hayo alisema yeye alipangiwa kazi ya kwenda hoteli ya SG inayomilikiwa na marehemu ili kumuuzia madini aina ya Tanzanite ambayo yangemvuta kuingia katika mtego.

“Baada ya kufika, nilimuuzia jiwe moja kati ya matatu niliyopewa na Shariffu kwa Sh3 milioni nikamwambia yaliyobaki niko na mwenzangu na tukakubaliana kufanya biashara kesho yake,”anasema.
Bilionea Msuya alivyouawa.

“Tarehe 7.8.2013 nilipangiwa kumtoa Msuya kutoka ofisini kwake hadi maeneo ya KIA (uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro) eneo la Mjohoroni ambako tungefanya biashara,”

Siku hiyo, mshtakiwa huyo aliondoka Arusha akiwa na Jabir na Sadik wakitumia gari aina ya Toyota Noah ikiendeshwa na mshtakiwa wa tatu, Mussa Mangu hadi maeneo ya KIA ambapo walimshusha ili kumsubiri Erasto.

Akiwa hapo, marehemu alifika na akaingia kwenye gari yake aina ya Range Rover na kuondoka kuelekea mji wa Bomang’ombe wilayani Hai ili kumfuata mshtakiwa wa tano, Karim Kihundwa.

Hata hivyo ananukuliwa akisema walipofika Bomang’ombe hawakumkuta Karim na alipowasiliana naye, alimweleza kuwa tayari alikuwa ameshafika eneo la Mjohoroni ambako Msuya aliuawa.

Msuya alipoona SMG alijaribu kukimbia

“Tulimkuta Karim pale Mjohoroni akiwa amevaa fulana nyekundu na suruali ya Khaki akiwa ame park (ameegesha) pikipiki kama meta 100. Erasto aliteremka na kumfuata Karim,”anaeleza Majeshi.

Anaeleza kuwa baada ya kukutana na Karim, walikubaliana warudi kwenye gari kwa ajili ya kufanya biashara na Msuya alipogeuka ili aanze kwenda kwenye gari, Karim alitoa bunduki aina ya SMG.

“Msuya alipomuona Karim ametoa bunduki alijaribu kukimbia kuelekea kwenye gari lakini Karim alifanikiwa kumfyatulia risasi nyingi,”ananukuliwa mshtakiwa huyo katika maelezo hayo.

Anasema baada ya kumuua marehemu, yeye na Karim waliondoka kwa kutumia usafiri wa pikipiki aina ya Toyo, lakini pikipiki hiyo ikapata pancha ambapo alifika Sanyajuu na kukodi pikipiki nyingine.

Alipoulizwa katika maelezo hayo ni kiasi gani walilipwa kwa kazi hiyo, mshtakiwa huyo alijibu kuwa kila mmoja alikuwa ameahidiwa kulipwa Sh17 milioni lakini hadi anatoa maelezo hayo Oktoba 5,2013 hakuwa amelipwa chochote.

Katika maelezo hayo anasema alikuwa hajui sababu kwanini Msuya aliuawa na kwamba katika kufanikisha mpango huo, Sharifu alinunua pikipiki na pia kuwapa kila mmoja simu mpya na laini.

Baada ya kumaliza kusoma maelezo hayo, wakili wa Serikali, Kassim Nassir alifunga kumhoji shahidi huyo ambapo mawakili wa utetezi walipata fursa ya kumhoji na mahojiano yalikuwa ifuatavyo:-

Wakili Ndusyepo: (akirejea maelezo ya mshtakiwa), Naomba fungua ukurasa wa sita. Ni kweli wakati unamuuliza maswali akikujibu ndicho ulikuwa unaandika?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili Ndusyepo: Je, kuna swali uliuliza “baada ya kufika marehemu akakuchukua hapo KIA mlienda wapi”. Ni kweli uliuliza hilo swali?

Shahidi: Ni kweli

Wakili Ndusyepo: Ufahamu wa kuuliza “alipokuchukua hapo KIA mlienda wapi”, uliupata wapi?

Shahidi: Alinijibu mwenyewe.

Wakili Ndusyepo: Unasema nini tukikuambia tayari ulihusika katika mahojiano mengine na ulikuwa unampandikizia majibu mshtakiwa utasemaje?

Shahidi: Hilo sio kweli.

Wakili Magafu: Kati ya Majeshi, Karim na Sadick ni yupi mliyeanza kumkamata?

Shahidi: Karim na Sadick ndio walianza kukamatwa.

Wakili Magafu: Unaweza kukumbuka Sadick na Karim walikamatwa Kaliua (Tabora) lini?

Shahidi: Tarehe 13.9.2013.

Wakili Magafu: Mlifanikiwa kuwahoji mlipowakamata?

Shahidi: Mimi sikuwahoji.

Wakili Magafu: Uliwahi kuwasikia walichokuwa wanakisema kwenye mahojiano?

Shahidi: Hapana.

Wakili Magafu: Utakubaliana na mimi kuwa katika maelezo yako ulisema mliwahoji?

Shahidi: Ni pale tulipowakamata.

Wakili Magafu: Ni nani alikuambia Ally Majeshi aliwahi kukamatwa na kupelekwa Gerezani hadi umuulize hilo swali?

Shahidi: Ni yeye mwenyewe aliniambia.

Wakili Magafu: Hebu soma hilo swali ulilomuuliza.

Shahidi: Nilimuuliza katika shughuli zako za kilimo uliwahi kukamatwa na kupelekwa gerezani.
Wakili Magafu: Kabla ya hilo swali ulimuuliza swali gani?

Shahidi: Alinieleza alimaliza darasa la saba lakini hakufaulu.

Wakili Magafu: Nenda kwenye lile swali linalohusu taarifa za mauaji ya Erasto Msuya.

Shahidi: Nilimuuliza “ulipata wapi taarifa za mpango wa kumuua Erasto Msuya?”

Wakili Magafu: Hilo swali ni nani alikuambia mshtakiwa wa saba alihusika katika mauaji hadi umuulize hilo swali?

Shahidi: Yeye mwenyewe ndiye alisema hivyo.

Wakili Magafu: Uliwahi kumuuliza mtuhumiwa kwa nini waliamua kumuua marehemu?

Shahidi: Alisema hata yeye hajui.

Wakili Magafu: Ulimuuliza ni kwanini hakuwauliza wenzake sababu za kumuua marehemu?

Shahidi: Wala sikumuuliza.

Wakili Magafu: Je unajua sababu ya mauaji ya Msuya?

Shahidi: Sijui.

Wakili Safari: Nikikuambia habari hizo ulizoandika uli take advantage (fursa) ya kile alichokueleza Jalila kwa sababu ni ndugu na Majeshi?

Shahidi: Sikumuhoji Jalila.

Wakili Safari: Uliwahi kumuuliza pesa ya Msuya aliyokuwa anunulie madini ilienda wapi?

Shahidi: Sikuuliza hilo.

Wakili safari: Marehemu alikuwa anaenda kufanya biashara, kwanini hukuuliza hilo swali?

Shahidi: Sikuuliza.

Wakili Safari: Nikikuambia hayo uliyoandika uliambiwa na mabosi zako baada ya kuchukua pesa ya marehemu utasemaje?

Shahidi: Sio kweli.

Wakili Safari: Kwa kutoongelea pesa ya marehemu, unakubaliana na mimi wakati wote uliowataja kwenye hayo maelezo uliyoyaandika, ulifanya hivyo kwa maelekezo ya Samweli (shahidi wa tisa)?

Shahidi: Sio kweli.

Kesho usikose kufuatilia simulizi ya kesi hii katika tovuti hii na gazeti la Mwananchi.