‘Tunataka utekelezaji kwa vitendo’
Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe akisalimiana na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana (kulia) Ikulu jijini Dar es Salaam jana, kwenye mkutano wa viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani na Rais Samia Suluhu Hassan. Picha ya Ericky Boniphace
Muktasari:
- Viongozi wa vyama vya siasa nchini wamepongeza uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuondoa marufuku ya mikutano ya vyama vya siasa iliyowekwa mwaka 2016 huku wakitaka kuona ruhusa hiyo ikitekelezwa kwa vitendo.
Dar es Salaam. Viongozi wa vyama vya siasa nchini wamepongeza uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuondoa marufuku ya mikutano ya vyama vya siasa iliyowekwa mwaka 2016 huku wakitaka kuona ruhusa hiyo ikitekelezwa kwa vitendo.
Viongozi hao pia wamefurahishwa na uamuzi wa Rais Samia kuhusu suala la Katiba mpya ambalo limekuwa likidaiwa na wadau mbalimbali ambapo Rais amesema ataunda kamati maalumu itakayojumuisha wadau kutoka makundi tofauti ya kijamii.
Juzi, Rais Samia alitangaza kuondoa zuio la mikutano ya hadhara lililowekwa na hayati John Magufuli na kusababisha mkwamo wa kisiasa kwa vyama vya siasa kutotekeleza majukumu yao ya msingi ikiwemo kukutana na wanachama wao.
Alipoingia madarakani Machi 19, 2021, Rais Samia aliahidi kuleta maridhiano ya kitaifa na baadaye Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini iliunda Kikosi Kazi ambacho Rais Samia alikipa jukumu la kuratibu maoni ya wanachi kuhusu demokrasia ya vyama vingi ambacho kilikabidhi ripoti yake Oktoba 21 ikiwa na mapendekezo mengi.
Baadhi ya mambo yaliyopendekezwa na kikosi kazi ni kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara pamoja na kuundwa kwa kamati maalumu itakayochambua maoni ya wadau kuhusu mchakato wa katiba mpya, mambo ambayo Rais Samia ameyatekeleza.
Katika hotuba yake jana alisema, tayari ameshazungumza na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro na kumueleza kuwa tayari sheria kadhaa ziko mbioni kurekebishwa.
“Juzi pia nilikuwa na kikao na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wenyewe pia wako mbioni kurekebisha sheria ya tume ya uchaguzi,” alisema Samia.
Alisema kwa upande wa wizara ya katiba na sheria kuna marekebisho ya sheria ya msajili wa vyama, sheria yenyewe ya vyama vya siasa na nyingine ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi huku akieleza wakati zikifanyiwa kazi kunapaswa kuwapo ushiriki mpana wa vyama vya siasa, kijamii ili hoja zao za msingi ziingizwe katika sheria.
Wakati vyama vikiwasilisha maoni yake mbele ya kikosi kazi, Chama cha ACT- Wazalendo kilitoa mapendekezo 25 yanayoifuta Sheria ya Vyama vya Siasa sura 258 ili kuandaa mpya.
Marekebisho hayo pia yanakwenda sanjari na marekebisho ya Sheria zote zinazosimamia chaguzi chini ya Tume mbili; ZEC ya Zanzibar na NEC kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu alisema mapendekezo hayo yanalenga kupunguza mamlaka ya msajili wa vyama vya siasa na kuondoa udhaifu katika mchakato wa usajili ikiwamo muda wa usajili, uendeshaji wa vyama.
“Hali ilivyo sasa msajili wa vyama sio msajili tu ila ndiye kiongozi anayeamua kila kitu kwa chama cha siasa,” alisema Ado.
Chadema wao walitoa maoni yao nje ya Kikosi Kazi wakitaka mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa bila kusubiri mabadiliko ya kanuni za mwaka 2019, bila kusubiri mabadiliko ya Sheria ya Jeshi la Polisi.
Lakini pia yapo mapendekezo mengine yaliyowasilishwa mbele ya kikosi kazi yakitaka itungwe sheria ya kusimamia shughuli za Tume ya Taifa Uchaguzi, kuwepo na sheria moja ya uchaguzi itakayotumika kusimamia uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani, badala ya kuwa na sheria mbili ambazo ni Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343 na Sheria ya Uchaguzi wa Madiwani, Sura 292.
Kauli ya Waziri Ndumbaro
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro alisema wamepokea maelekezo ya Rais Samia ya kwenda kuzifanyia mabadiliko sheria mbalimbali zinazohusu masuala ya siasa na tayari wameanza na sheria ya vyama vya siasa.
Alisema leo atakutana na Tume ya Marekebisho ya Sheria ili kujadiliana namna ya kukamilisha kazi hiyo kama walivyoelekezwa na Rais Samia kwenda kuzifanyia mabadiliko sheria na kanuni zinazokwamisha shughuli za kisiasa.
“Kwa bahati nzuri tuna Tume ya Kurekebisha Sheria, kesho (leo) nitaonana nao kwa ajili ya hili. Kwa hiyo, sheria zote zinazogusa eneo hili, tunakwenda kuzifanyia kazi, tayari tumeanza na Sheria ya Vyama vya Siasa,” alisema Dk Ndumbaro.
Kauli za wadau
Wakizungumzia uamuzi wa Rais Samia kwenye mikutano ya hadhara na mchakato wa Katiba mpya, viongozi wa vyama vya siasa wamempongeza kwa hatua hiyo wakieleza hilo ni jambo walilokuwa wakilipigania kwa muda mrefu.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa, alisema si maboresho ya sheria katika vyama vya siasa pekee yanayohitajika bali sheria nyingi nchini zinahitaji maboresho.
“Si eneo hilo tu, sheria mbalimbali za nchi zinahitaji marekebisho, ili kuepuka kufanya marekebisho kila wakati ni vyema tuanze na suala la Katiba mpya ili baada ya miaka miwili tuweze kufanya mabadiliko ya sheria zetu zote ziendane na katiba,” alisema
“Siyo leo tunafanya mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa, kesho tufanye mabadiliko haya, Katiba mpya ndiyo itarekebisha sheria mpya kwa ujumla, hatutakuwa na haja ya kufanya kitu kimoja kimoja.”
Wakili Onesmo Kyauke, alisema sheria ya tume ya uchaguzi na vyama vya siasa ingebadilishwa baada ya kupatikana kwa katiba mpya.
“Nadhani Katiba ije halafu ndipo sheria zibadilishwe kulingana na sheria, ingekuwa rahisi tuanze na Katiba ndipo yale mambo mengine yafuate, kama Katiba itapatikana kabla ya 2025 ni vyema tuanze nayo kama hakuna uhakika itapatikana lini tunaweza kufanya mabadiliko hasa kuwa na tume huru ya uchaguzi na changamoto zingine zinazojitokeza kwenye uchaguzi,” alisema.
Alichokisema Mbowe
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyekuwa miongoni mwa viongozi waliokuwa Ikulu alisema wanapokea uamuzi wa Rais Samia kwa tahadhari kubwa kwa sababu mikutano ya hadhara kurejeshwa ni haki ya vyama vya siasa iliyocheleweshwa.
“Tunataka kuona utekelezaji wa hili kuanzia ngazi ya taifa, ngazi ya mikoa, ngazi ya wilaya hadi kwenye kata. Isije ikawa demokrasia inatolewa huku juu lakini inanyimwa huko chini, jambo hili linahusisha watu wengi wakiwemo jeshi la polisi,” alisema Mbowe.
Kuhusu suala la kupata katiba mpya ambalo chama chake kimekuwa kikipigania, Mbowe alisema wamelipokea kwa hisia chanya kwa sababu kwenye majadiliano yao wamekuwa wakishauri kuundwa kwa chombo ambacho hakitahodhiwa na kundi fulani.
“Tumezungumza kwamba mchakato wa Katiba ni wa sasa, lazima uanze sasa. Tuliona kwamba tuwe na chombo ambacho hakitahodhiwa na chama kimoja au kundi la watu, tulishauri hili kupitia mazungumzo mbalimbali na wenzetu.
“Nampongeza Rais Samia kwamba ameliona hilo na amelizungumza kwenye hotuba yake,” alisema Mbowe ambaye chama chake hakikwenda kutoa maoni mbele ya kikosi kazi lakini kimekuwa na mazungumzo na CCM.
Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alisema uamuzi wa Rais Samia utafungua ukurasa mpya wa demokrasia, hivyo anampongeza kwa uamuzi huo ambao haukuwa mwepesi, bali ulijawa na maneno mengi.
Zitto alisema Rais Samia ametembea kwenye maneno yake kama alivyoahidi wakati anaingia madarakani Machi 19, 2021.
Alisisitiza anafarijika na mambo matatu ambayo Rais Samia ameyafanyia uamuzi ya mikutano ya hadhara, mabadiliko ya sheria na mchakato wa katiba.
“Huu ni mwaka wa mageuzi ya kisiasa, ni mwaka wa demokrasia. Ni kupitia majukwaa pekee wananchi wanaweza kuwasikiliza viongozi wao wa vyama vya siasa,” alisema Zitto ambaye alikuwa mjumbe wa kikosi kazi.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatibu alimpongeza Rais Samia kwa kufanyia kazi maoni ya wadau waliyoyatoa mbele ya kikosi kazi na baadaye kuwasilishwa kwake.
“Wengi tulitamani kuona mikutano ya hadhara ikiendelea lakini ikazuiliwa. Sasa Rais amesikiliza kilio cha wadau akaamua jambo hili nifike mwisho, ni jambo la kumpongeza sana,” alisema Khatibu ambaye pia ni mwenyekiti wa Ada-Tadea.
Akiwa na mtazamo kama huo, mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hashim Rungwe alisema hilo ni jambo la kufurahisha kwa sababu kwa muda mrefu hawajafanya mikutano ya hadhara ambayo imeruhusiwa kisheria.
“Tunakwenda kufanya mikutano ya hadhara tuone kwenye practice (utekelezaji) tunakwendaje, je, polisi wamemwelewa Rais kama sisi tulivyomwelewa au tumeelewana tofauti?” alisema Rungwe.
Makamu mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Joseph Selasini alisema kiongozi mwenye busara huwa hakurupuki katika kushughulikia jambo, hivyo alimpongeza Rais Samia kwa kuonyesha uongozi bora katika kushughulikia jambo hilo.
“Ninawaomba wenzangu wa vyama vya siasa, twendeni tukafanye siasa za kistaarabu kama alivyosema Rais, kwa kuzingatia katiba, sheria na utamaduni wetu,” alisema Selasini wakati akizungumza na Mwananchi.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa ADC, Hamad Rashid alisema Rais Samia ametekeleza mapendekezo ya kikosi kazi ambayo yalitokana na maoni ya wadau, hivyo ni hatua nzuri ya kupongeza na wao kama chama cha siasa wanakwenda kufanya mikutano kistaarabu.
“Tunaahidi kwamba tutafanya mikutano kistaarabu kwa kuzingatia sheria na utamaduni wetu. Niwaombe na wenzangu wa vyama vingine, tushirikiane pamoja kuijenga nchi na siyo kuleta mifarakano ya kisiasa,” alisema Rashid.
Imeandikwa na Peter Elias, Baraka Loshilaa na Aurea Simtoe