‘Tungeweza, tungefuta maumivu ya Oktoba 2025’
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akipokea Ripoti ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025, kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Mohamed Chande Othman, Ikulu Jijini Dar es Salaam, Aprili, 23, 2026.
Muktasari:
- Rais Samia amesema licha ya baadhi ya mataifa na vyombo vya habari, hasa vya kimataifa, kuitazama Tanzania kwa jicho la lawama na kukosoa kwa ukali, hali hiyo haikushangaza kutokana na tofauti za mitazamo pamoja na kile alichokiita upotoshaji mkubwa wa taarifa.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 yameacha doa ambalo Watanzania wangetamani lisingekuwepo kabisa katika historia ya nchi.
Akizungumza wakati akipokea ripoti ya tume ya kuchunguza matukio hayo leo Aprili 23, 2026 Rais Samia amesema licha ya baadhi ya mataifa na vyombo vya habari, hasa vya kimataifa, kuitazama Tanzania kwa jicho la lawama na kukosoa kwa ukali, hali hiyo haikushangaza kutokana na tofauti za mitazamo pamoja na kile alichokiita upotoshaji mkubwa wa taarifa.
“Wapo waliotumia matokeo ya Oktoba 2025 kutusimanga na kutunyooshea vidole. Hatukushangaa sana kwa sababu mitazamo ya binadamu haifanani na kulikuwa na upotoshaji mkubwa wa habari za tukio hilo uliofanywa na vyombo vya habari, hususan vya nje,” amesema.
Rais Samia amesema kuwa, kwa desturi na utu wa Kiafrika, nyakati za majonzi na maumivu zinapaswa kuambatana na faraja, si lawama au kejeli, akibainisha kuwa walioumia zaidi na matukio hayo ni Watanzania wenyewe.
“Kwa desturi ya waungwana, linapotokea jambo la hasara na kuumiza mioyo, matarajio ni kufarijiwa badala ya kuzodolewa. Walioumizwa na tukio lile ni sisi Watanzania,” amesema
Ameongeza kuwa Taifa limepoteza watu wake wa karibu, watoto, ndugu, jamaa na marafiki na kusisitiza kuwa, hakuna mtu wa nje anayeweza kuwa na uchungu mkubwa kuliko Watanzania wenyewe walioguswa moja kwa moja na athari za matukio hayo.
“Ni sisi tuliopoteza watoto wetu, ndugu zetu na marafiki. Haiwezekani mtu mwingine asiye Mtanzania awe na uchungu zaidi kuliko sisi,” amesema kwa msisitizo.
Rais Samia amesema kama ingekuwa inawezekana, Taifa lingerudisha nyuma muda ili kuzuia kabisa yaliyotokea.
“Kungekuwa na uwezekano, tungetamani siku zirudi nyuma ili yaliyotokea Oktoba 2025 yawe hayajatokea na historia ijiandike upya, tuweze kufuta doa tuliloingia,” ameongeza.