Jaji Chande afafanua tuhuma matumizi ya silaha kwa Polisi
Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman akisoma Muhtasari wa Ripoti ya Tume hiyo, Ikulu jijini Dar es Salaam, Aprili 23, 2026.
Muktasari:
- Mwenyekiti wa Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 Jaji Othman Chande amesisitiza askari wa Jeshi la Polisi kuzingatia sheria ya matumizi ya silaha.
Dar es Salaam. Jaji Mohamed Chande amefafanua kuwa licha ya askari polisi kuruhusiwa kuwa na silaha, matumizi yake yanadhibiwa na misingi ya kisheria.
Jaji Chande ameyasema hayo akiwasilisha Ripoti ya Kuchuza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Katika vurugu hizo, kumekuwa na taarifa nyingi kwenye jamii wengi wakihoji waliohusika na vifo hivyo ambavyo vilihusisha vurugu za vijana na vikosi vya ulinzi na usalama ambavyo vilikuwa vikidhibiti vurugu hizo.
“Kwa mujibu wa mwongozo wa Jeshi la Polisi, (PGO 204) askari wa Jeshi la Polisi haruhusiwi kutumia silaha hiyo isipokuwa kwenye matumizi ya lazima ambayo sheria hiyo imeyaelekeza,” amefafanua Jaji Chande.
Katika maelezo yake, Jaji Chande ameeleza kuwa ushahidi uliotolewa na mashuhuda wa vurugu hizo, yapo maeneo ambayo watu wameeleza ndugu zao kuuawa kwa kupigwa risasi na askari wa Jeshi la Polisi.
“Serikali kupitia Jeshi la Polisi inao wajibu wa kulinda usalama wa raia na mali zao na pale inapotokea tatizo kuhakikisha hali hiyo inadhibitiwa,” amesema.
Akifafanua kuhusu waliohusika na matukio hayo ikiwemo kufadhili, kushawishi na kuchochea vurugu hizo, amesema tume hiyo haitatuhumu watu bila kuwapa nafasi ya kujibu, akisema ni takwa la kisheria.
“Tume zimezuiwa kisheria kutaja mtu bila kumpa nafasi ya kumsikiza. Sisi ni tofauti na nchi zingine, haki ya kumpa mtu nafasi ya kumsikiliza ni ya kikatiba,” amesema akifafanua kuwa uhalali wa matumizi ya nguvu na silaha upimwe kwa muktadha wa kila tukio moja.
Kwa ufafanuzi wake, amesema matumizi ya silaha yameripotiwa katika mazingira na namna tofauti akisisitiza kuwa kila tukio yafaa lichunguzwe kwa muktadha wake ili kupima usahihi wa nguvu iliyotumika.
“Tume imepokea madai ya matumizi ya silaha kutekeleza mauaji, napendekeza Tume ipewe nafasi kuendelea na uchunguzi ikiingia hatua ya kuchunguza waliohusika na kupendekeza hatua za uwajibikaji,” ameomba Jaji Chande.