'Tusikimbie tunapohamasishana kujenga kanisa la Mungu'

Muktasari:

  • Waamini wa kanisa katoliki Jimbo la Geita wameaswa kujitoa kwa moyo wa upendo ili kufanikisha ujenzi wa makanisa unaoendelea hivi sasa parokia mbalimbali Jimbo la Geita.

Sengerema. Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Geita, Flavian Kasala amewataka waamini wa kanisa hilo wasikimbie na kuacha kusali kutokana na michango waliyopangiana katika suala zima la ujenzi wa Kanisa la Mungu.

Kauli hiyo ameitoa leo Jumamosi  Machi 23, 2024 wakati akitoa mahubiri kwenye Misa ya harambee ya ujenzi wa kanisa jipya parokia ya Bikra Maria afya ya wagonjwa iliyoko Kata ya Mishine mjini Sengerema.

Kanisa hilo   linalojengwa la Parokia ya Bikra Maria afya ya wagonjwa mjini Sengerema litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kubeba waumini 1,600 kwa wakati mmoja.

Akizungumza katika misa hiyo Askofu Kasala amesema katika kumtumikia Mungu watu wote wanapaswa kujitoa kwa moyo ili kanisa lisonge mbele, maana hakuna wa kuyafanya hayo kama sio waamini.

"Leo ndiyo maana mnamuona hapa kanisani  Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko amekuja kutushika  mkono kwenye harambee yetu ili tukamilishe ujenzi wa nyumba ya Mungu hivyo tushirikiane wote kwa pamoja.

Kwa upande wake Katibu wa ujenzi wa kanisa hilo, Joseph Mashinji amesema kazi ya ujenzi ilianza mwaka 2011 na hadi sasa haujakamilika licha ya kutumika Sh1.7 bilioni.

"Fedha zote ni michango ya waamini na wahisani mbalimbali ndiyo limefikisha hapa lilipo na tuko hatua za ukamilishaji,” amesema Mashinji.

Amos John ni muumini katika kanisa hilo,  amesema mshikamano na umoja wao ndiyo silaha ya mafanikio yaliyosababisha kufikia   hatua hiyo.