Unyanyasaji mitandaoni watajwa kushika kasi

Muktasari:
- Wakati jitihada zikifanyika kukabiliana na vitendo vya vipigo na unyanyasaji wa kingono kwa wanawake, imebainika kuwa sasa ukatili wa kijinsia kwenye mitandao ya kijamii umekuwa changamoto kubwa kwa wasichana.
Dar es Salaam. Wakati jitihada zikifanyika kukabiliana na vitendo vya vipigo na unyanyasaji wa kingono kwa wanawake, imebainika kuwa sasa ukatili wa kijinsia kwenye mitandao ya kijamii umekuwa changamoto kubwa kwa wasichana.
Miaka ya karibuni, baadh ya watu wamekuwa wakitumia vibaya mitandao hiyo kwa kuwadhalilisha wanawake na wasichana kwa kuwekwa picha chafu na video zao za faragha.
Akizungumza na mabinti katika maadhimisho ya Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, mtetezi wa haki za binadamu, mwanasheria Anagrace Rwehumbiza alisema ni kitend cha kushangaza kuona kuwa jamii imeruhusu ukatili huo kuota mizizi.
Alisema kuwa sheria ya makosa ya mtandao haitaweza kufanya kazi kukabiliana na ukatili wa kijinsi mitandaoni endapo jamii haitoona kuwa hilo ni tatizo kubwa.
“Mabinti wanakumbana na udhalilishaji huu, lakini jamii haioni kama ni tatizo ndio kwanza wanashiriki kusaka kuziona hizo picha badala ya kupambana na wanaozisambaza.
Mwanasheria huyo alisema ni muhimu kwa wazazi na wanajamii kumsaidia binti aliyekutana na ukatili huo ili kufikisha kwenye vyombo vya kisheria kwa hatua zaidi, badala ya kumuongezea maumivu muathirika wa tukio hilo.
“Wazazi tuwape elimu watoto wetu kuhusu matumizi ya mtandao na hatari yake endapo itatumika vibaya, tunavyoendelea kufumbia macho na kuona ni jambo la kawaida ndivyo hatari inavyozidi kuongezeka,” alisema.
Kwa upande wake. mwanasheria Anna Matui alisema hakuna sababu ya msichana au mwanamke aliyepitia ukatili huo kukata tamaa ya maisha hadi kufikia uamuzi wa kujitoa uhai wakati vyombo vya sheria vipo.
“Usikubali mtu aharibu maisha yako ukajiona wewe sio sehemu ya jamii au hata kufikia kujia. Ikikutokea suala hili simama, jiamini sheria ipo fikisha mahali panapohusika,” alisema Anna.
Ofisa mradi msaidizi wa asasi ya Dignity Kwanza inayotoa msaada wa kisheria kwa wakimbizi, Gladness Muyaga alisema wamekuwa wakipata kesi nyingi za wasichana waliofanyiwa udhalilishaji mtandaoni na kubaini kuwa kuna haja kubwa ya kuelimisha jamii.