Upelelezi kesi inayowakabili waliokuwa polisi wakamilika

Waliokuwa askari polisi watatu pamoja wafanyabiashara wawili wanaokabiliwa na kesi ya unyang'anyi wa kutumia silaha na kuiba Sh90 milioni, wakiwa chini ya ulinzi wa askari Magereza Mahakaka ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne

Muktasari:

 Tarimo na wenzake, wanadaiwa kutenda kosa eneo la Kurasani, karibu na ofisi za Uhamiaji

 Dar es Salaam. Serikali imesema upelelezi katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kuiba Sh90 milioni, inayowakabili watu watano wakiwamo waliokuwa askari polisi, umekamilika.

Wakili wa Serikali, Titus Aaron ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Aprili 2, 2024 wakati kesi hiyo ya jinai namba 197/2023 ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni waliokuwa askari kanzu watatu mwenye namba  F 7149 D/Coplo Ramadhani Tarimo (42) maarufu kama Rasta na mkazi wa Kipawa; G 7513 D/Coplo Majid Abdallah(35) na mkazi wa Kunduchi na WP  6582 D/ Coplo Stella Mashaka( 41) mkazi wa Railway.

Wengine ni wafanyabiashara Ashiraf Sango (31) na Emmanuel Jimmy (31), wote wakazi wa jiji hilo.

Wakili Aaron ametoa taarifa hiyo leo Aprili 2, 2024 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Amiri Msumi kuwa upelelezi umekamilika, huku akiomba tarehe nyingine kwa ajili ya kusomewa hoja za awali (PH).

"Hivyo tunaomba siku 14 za kazi ili tuweze kuandaa hoja za awali na kuja kuwasomea washtakiwa hao," amedai Aaron.

Aaron baada ya kutoa taarifa hiyo, mawakili wa upande wake wa  utetezi,  Gloria Ulomi na Mbaraka Kapera wameomba Mahakama itoe siku saba kwa upande wa mashtaka kuandaa hoja za awali na sio siku 14 kwa kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika.

Akijibu hoja hiyo, wakili Aaron amedai kuwa wanahitaji muda wa kutosha kuandaa hiyo PH.

"Mheshimiwa hakimu, tunaomba siku 14, kwa sababu kuandaa hoja za awali, sio jambo dogo, hivyo siku saba haziwezi kutosha kuandaa hoja za awali," amedai wakili Aaron.

Hakimu Msumi baada ya kusikiliza hoja za pande zote, alikubaliana na hoja za upande wa mashtaka za kuwapa siku 14 kuandaa hoja za awali.

" Wacha tuwape siku 14 upande wa mashtaka ili Aprili 15 wakija mahakamani hapa waje wamekamilika kwa ajili ya kuwasomea hoja za awali,” amesema hakimu Msumi.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 15, 2024, kwa ajili ya kusomewa hoja za awali na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka la unyang'anyi linalomkabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo, Agosti 28, 2023 eneo la Kurasani, karibu na ofisi za Uhamiaji, lililopo Wilaya ya Ilala na  waliiba Sh90 milioni kutoka kwa Grace Donald Matage.

Inadaiwa kabla na baada ya kufanya wizi huo, walimtishia Grace kwa bunduki ili waweze kujipatia fedha hizo bila kikwazo.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo, Oktoba 31, 2023 wakikabiliwa na shtaka moja la unyang'anyi wa kutumia silaha na kuiba.