‘Utekaji’ watikisa ziara ya Makonda

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda akizungumza na wananchi wa Maswa mkoani Simiyu baada ya kupokelewa mkoani humo katika mwendelezo wa ziara yake ya mikoa 20. Picha na CCM

Muktasari:

  • Makonda alitoa machozi aliposikiliza simulizi ya kupotea John Chacha.

Simiyu. Ziara ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda katika mikoa mitatu kati ya kumi imeibua malalamiko ya matukio ya watu kupotea na kutekwa kwenye mazingira ya kutatanisha wakiwamo wafanyabiashara.

Makonda alianza ziara Januari 19, mwaka huu mkoani Dar es Salaam, baadaye Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Tabora, Shinyanga, Simiyu na Singida.

Katika mikutano ya hadhara Singida, Simiyu na Shinyanga baadhi ya ndugu na jamaa wa watu waliopotea walipaza sauti wakiwasilisha malalamiko yao kwa matukio yaliyotokea mwaka 2021, 2022 na 2023.

Mbali na hilo, mmoja wa wananchi waliopaza sauti zao, alidai kusababishiwa ulemavu na polisi na kuporwa Sh19 milioni.

Makonda alitoa machozi aliposikiliza simulizi ya kupotea John Chacha.


Malalamiko Singida

Januari 28 mwaka huu, mkazi wa Wilaya ya Singida, Mwanahamisi Sombi alimuomba Makonda kuingilia kati kuhusu kutoweka Haruna Iddi (50) na Juma Iddi (45), ambao ni wafanyabiashara wa mbao.

Alidai kuwa ndugu hao walipotea katika mazingira yenye utata Desemba 28, mwaka jana, saa 10 jioni katika maeneo ya Mwenge na Mghanga.

Mwanahamisi ambaye ni mke wa Haruna, amesema ana watoto saba anaoshindwa kuwapeleka shule kutokana na hali ngumu, hivyo amemuomba Makonda aingilie kati mumewe na shemeji yake wapatikane.

"Mume wangu na shemeji yangu walitekwa Desemba 28, hadi sasa hawajapatikana. Tumeenda kwa RPC (Kamanda wa Polisi Mkoa) na kwa mkuu wa mkoa wanasema hawajui. Nina watoto saba wakiwamo wa shemeji yangu na hawajaenda shule, hali ya maisha ni mbaya naomba unisaidie," amesema Mwanahamisi.

Mkuu wa Wilaya wa Singida, Moses Machali amesema wanalifahamu suala hilo na wameliagiza Jeshi la Polisi kuendelea na upelelezi kuhakikisha watu hao wanapatikana na taarifa zitolewe.

"Taarifa hizi zilifika katika ofisi zetu na mazingira ya upoteaji wa ndugu hao ni kwamba waliaga wanakwenda kazini hawakurudi, tuliliagiza Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi kuhusu kupotea kwa ndugu hao," amesema Machali.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba amesema: "Jambo hili nalifahamu sana, mtu huyo amekuja ofisini kwangu mara mbili, baadaye nikamjumulisha RPC ambaye amemjulisha Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camillius Wambura waliwatafuta kwenye vituo vyote vya polisi nchini hawakufanikiwa. Hatujajua hadi leo, RPC anashughulikia suala hili."

Makonda amesema suala hilo ni la kiusalama, hivyo hawezi kuingilia wakati Polisi ikiendelea na taratibu zake.

Awali, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Stella Mutabihirwa alisema wameshafanya taratibu zote za kipolisi na kuziwasilisha makao makuu.


Mkoani Shinyanga

Akiwa ziarani mkoani Shinyanga Makonda alipokea malalamiko ya aina hiyo kutoka kwa wanawake watatu waliodai waume na watoto wao wametoweka katika mazingira tofauti.

Makonda aliyesimama eneo la Tinde akitokea Kahama, alipokea malalamiko kutoka kwa mkazi wa Majengo, wilayani humo, Nyangeta Malawa akisema mumewe John Chacha alitoweka Desemba 7, 2021 akiwa Kata ya Mongolo.

Amesema tukio hilo lilitokea katika ofisi za ardhi za kata hiyo, ambako alipewa taarifa na ofisa mtendaji kata kuwa mume wake amechukuliwa na watu wasiojulikana.

Malawa amesema tukio hilo lilitokea siku ya mwisho ya kutafuta suluhisho la mgogoro baina ya Chacha na mlalamikiwa (jina limehifadhiwa kwa sasa).

"Tulifanya jitihada kufuatilia suala hilo hadi sasa hatujui hatima yake, hatukuridhika na upelelezi ngazi ya wilaya tukaamua kuja mkoani, kesi yetu ilifuatiliwa na RPC, ilipatikana simu ya mume wangu, tuliitwa kuitambua,” amesema Malawa.

"Tulibaini ni yenyewe, lakini tangu tuitambue hatujawahi kupata taarifa yoyote ya kinachoendelea. Mtu tuliyekuwa na mgogoro naye amefanya uwekezaji kwa kujenga kiwanda cha unga, naomba unisaidie kufahamu mume wangu alipo."

Ufafanuzi wa RPC

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi alitakiwa na Makonda kutoa ufafanuzi ili umma ujue kuhusu madai hayo.

"Ni kweli tukio hili lilitokea Desemba 7, 2021, nilikuwa sijahamia hapa Shinyanga. Nilipofika Agosti 2023 nilikuta malalamiko haya na aliyekuwa anakuja ofisini ni shemeji yake, aliyenipa malalamiko,” amesema Kamanda Magomi.

 "Aliniambia wakati wanaenda Baraza la Ardhi Kahama kabla ya uamuzi haujatoka, lilikuja gari, ghafla Chacha alichukuliwa ambaye bado hajapatikana. Nilichukua jalada na kufuatilia, nilikuta mlalamikiwa alishakamatwa na wenzake saba."

Amesema alipeleka jadala la shauri hilo kwa mwendesha mashtaka aliyesema watashindwa kutoa mashtaka ya mauaji kwa sababu hawajaona mwili wa marehemu na kutoa maelekezo kwa Jeshi la Polisi kuhusu Chacha.


Eneo lenye mgogoro

Baada ya maelezo hayo, Makonda alikaa kimya kidogo, akasema suala hilo ni zito.

Akamhoji Malawa: "Mume wako hajulikani alipo na polisi wanaendelea na upelelezi wewe ungekuwa mimi ungenishauri nifanye nini."

Malawa amesema anamkabidhi suala hilo yeye amsaidie.

Makonda amesema mtu ametekwa na eneo wanalogombea limefanyiwa maendeleo kwa kujengwa kiwanda na watumishi wa Serikali walialikwa kukifungua bila kujua kuna damu ya mtu inalia.

"Vitabu vyote vitakakatifu vimetukataza dhuluma, lakini utashangaa unaalika viongozi wa Serikali wanakwenda pale na kumpongeza, kumbe hapo kuna damu ya mtu ndiyo maana mara ya kwanza nilipomsikiliza nilishindwa nikajikuta nalia hadi nikaona kazi hii ngumu," amesema Makonda.


Kuporwa fedha, ulemavu

Diana Pamba, alidai alipeleka malalamiko kwa RPC wa Shinyanga kuhusu kutekwa na askari mkoani humo aliyechukua Sh19 milioni kutoka kwake na kumsababishia ulemavu wa mguu, akishirikiana na mtu mwingine (jina limehifadhiwa).

Diana amesema aliitwa kufanya biashara ya madini, waliomwita waliposhindwa kununua katika eneo la Korandoto walimpeleka mjini kituo cha polisi, alikofunguliwa kesi ya wizi wa Sh8 milioni lakini hawakuwa na ushahidi.

"Nilipelekwa mahakamani nikashinda kesi, nikamfuata Kamanda Janeth akaniambia atanisaidia, akaanza kunipa na nauli karibu mara nne,” amesema Diana.

"Nilivyoshinda kesi kwa mara ya pili, nikamwambia afande Janeth nisaidie ili Sh19 milioni zirudi kwa sababu nina watoto saba nasomesha, baadaye IGP Wambura alimwambia kuwa anisaidie, nikaenda hadi kwa Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa), alitoa maelekezo kuwa nilindwe.”

Alidai anapofuatilia polisi anatishwa na kutukanwa akiambiwa amfuate Majaliwa.

“Nilikufuata Singida sikufanikiwa kukuona, nimekuja Shinyanga kukufuata, namlilia RPC wa Shinyanga," amesema.

Makonda alimtaka Kamanda Magomi kutoa ufafanuzi, ambaye alisema anamfahamu Diana aliyekwenda ofisini kwake kumlalamikia askari ambaye ameshafukuzwa kazi kwa utovu wa nidhamu na jalada lake limepelekwa kwa mwendesha mashtaka wa Mkoa wa Shinyanga.

"Walitoa hati ya mashtaka kuhusu wizi huu wa Sh19 milioni zilizochukuliwa wakati wa ukamataji, nilimpeleka Kennedy mahakamani na kesi ilifutwa kwa kukosekana mashahidi. Kwa sababu Diana analalamika hajapata haki yake polisi haijafungwa mikono, shauri limerudishwa mahakamani,” amesema Kamanda Magomi.

Kamanda amesema, "Shauri namba 1629 limesomwa mahakamani upya litarudishwa kesho (jana). Nimuombe ndugu yangu aende mahakamani kutoa ushahidi."

Diana ambaye ni mchimbaji mdogo wa madini hakukubaliana na maelezo ya Kamanda Magomi akisema kesi hiyo ni mara ya nne inafunguliwa na mara ya kwanza alielezwa mwanasheria ndiye atakayeifungua.

"Hiyo ni longolongo kama mmepeleka mahakamani kwa nini mliomba akaunti namba ya benki? Hawanipi ushirikiano naomba unisaidie," amesema Diana.

Makonda amesema suala hilo lina ukweli ndiyo maana alitekwa, kunyanga'nywa fedha na kuumizwa mguu.

Amesema kitendo cha Jeshi la Polisi kumfukuza askari wake walijiridhisha kuwa mtumishi huyo amekwenda kinyume cha sheria.

"Nilisema mkutano huu unafuatiliwa na IGP amempigia simu RPC, akimtaka ampe maelezo ya kesi hii, naomba mridhie jambo moja, kamanda aongee na Wambura ili apokee maelekezo,” amesema Makonda.

 "Naomba mridhie jambo moja, RPC nimuache na Diana, vumilia maelekezo ya bosi wake wakimaliza watatoa majibu na tutakuja kwako kwa hatua zaidi."


Kijana kupotea

Mariam Ndala, amesema tangu Novemba 25, 2022 kijana wake, Issa Hamis amepotea.

Amesema amekwenda polisi lakini hakuna ushirikiano, licha ya kudai Kamanda Magomi kuwa rafiki yake na mwanaye.

Kamanda Magomi kwa maelekezo ya Makonda ametoa ufafanuzi akisema wana taarifa ya kupotea kwa Issa, ambaye ni fundi magari.

Amesema siku ya tukio walikuwa wawili yeye na mwenzake.

“Jeshi la Polisi kupitia mitandao ya kijamii tulifungua taarifa na tumeendelea kufuatilia katika mitandao, simu yake ilizimikia wapi na tulipeleka taarifa kwa kampuni za simu lakini hajufanikiwa,” amesema kamanda.

Mariam alidai Kamanda Magomi anaundanganya umma kuhusu suala hilo, akidai siku moja kabla ya tukio walikuwa wote na mwanaye akimtengenezea gari.

“Naumia sina haki wala pa kwenda maana huyu mama (RPC) alinifukuza ofisini kwake, niliwaambia kama mwanangu amekufa waniambie ili nijue,” alidai Mariam.

Kamanda Magomi alidai kuwa hamfahamu Issa na taarifa za kupotea kwake zilitolewa kituo kikuu cha polisi na ofisini kwake lilikwenda jalada. Mariam alishikilia msimamo kudai Kamanda Magomi anadanganya.

Katambi aingilia kati

Makonda alimuambia Mariam mbunge wa Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi ameingilia kati suala hilo kwa kumtafuta Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni ili kuongeza nguvu ya kumtafuta mwanaye.

"Waziri ameagiza IGP Wambura asimamie kufuatilia, tuvumilie," amesema Makonda.

Awali, Hussein Hamis, mdogo wa Issa alieleza namna walivyomtafuta ndugu yao bila mafanikio mpaka sasa.

Amesema awali walihisi ameenda kwa ndugu na jamaa, wakauliza kwa takribani wiki mbili hawakupata majibu.

Baadaye waliamua kutoa taarifa kituo cha polisi Shinyanga.

"Tulipata fununu kuwa ndugu yetu anashikiliwa na vyombo vya usalama kwa ajili ya uchunguzi ila hatukujua ni uchunguzi wa nini na baadaye tukaambiwa kesi yake iko hapa mkoa, RCO anazo taarifa lakini kila tukitafuta ukweli kutoka kwa RCO hakuonyesha ushirikiano,” alidai.

Ibrahim Hamis, mdogo mwingine wa Issa, baada ya mkutano wa Makonda amesema mama yake amekwenda Dodoma kuonana na Waziri Masauni kupata ufumbuzi wa jambo hilo.


Mke alalamika mume kutoweka

Makonda akiwa Maswa mkoani Simiyu, alipokea malalamiko kutoka kwa Eliwaza Makwale kwamba, Desemba 23, 2022 mume wake alitoweka saa 10 jioni, akichukuliwa na watu wasiojulikana akiwa eneo lake la biashara.

Baada ya kupokea taarifa amesema alikwenda kituo cha polisi kutoa taarifa.

"Nilipofika kituoni nikaambiwa nisubiri dakika 10 kama wamemkamata watamleta, nikawaambia basi zuieni hata njiani kama kuna watu wasio wazuri wamemchukua maana sehemu aliyoelekea ni huku wakasema hapa hadi ifike saa 24,” amesema.

Amesema kwa zaidi ya mwaka mmoja amehangaika hajui alipo mume wake. Makonda alipomuita Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Maswa (OCD), Maganga Ngosha amesema amefika wilayani humo mwaka jana, na amekuta jalada la suala hilo na polisi wanaendelea kulifanyia kazi.

Akijibu swali la Makonda iwapo anahisi kuna jambo limesababisha tukio hilo amesema, "yeye ni mfanyabiashara angekuwa anatoka labda wiki hayupo sawa lakini kila siku yupo, ninafanya naye biashara ya nafaka, tulibandika matangazo yake, lakini yakaondolewa sijui kinachoendelea."

OCD Ngosha amesema yapo matukio mawili ya watu kupotea.

"Kwa mafunzo yako unahisi nini kinaendelea kwenye eneo lako la utawala," alihoji Makonda.

Ngosha amesema huenda kuna uhasama katika masuala ya biashara ndiyo maana polisi inaendelea kuchunguza. Alimtaka Makwale kutoa ushirikiano.

"Haipendezi mtu kuona au kusikia mtu amepotea halafu hakuna majibu tunaomba ushirikiano wa familia, lakini polisi wekeni jitihada, tumetoka Shinyanga kila anayesimama anasema ametoweka ameenda polisi hapati majibu,” amesema Makonda.

"Nimeanza kuogopa, mikoa mingine yote niliyopita huu ni wa 10, lakini kati ya hiyo Shinyanga na Simiyu kila mwanamama akisimama anamtafuta mume, mna shida gani? Maana kuna jambo linaloendelea kati ya Shinyanga na Simiyu."