Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

VIDEO: Hivi ndivyo watu wanavyotekwa na mahubiri ya mafanikio

Katika miaka ya hivi karibuni wameibuka watumishi wa Mungu waliojizolea wafuasi wengi kutokana na mahubiri wanayoyatoa.

Baadhi ya watumishi hao wamekuwa wakitoa mahubiri ya kutoa upako, utajiri na hata kuponya magonjwa mbalimbali.

Hali hiyo imewafanya kupata wafuasi wengi ambao hutafuta miujiza na majibu ya shida zao ndani ya muda mfupi.

Hatua hiyo imesababisha kila wanapotangaza kufanya mikutano au makongamano, watu wengi huenda na unapofika wakati wa kuombea wenye shida mbalimbali hujitokeza kwa wingi, ili waondokane na magumu yanayowakabili.

Wapo wanaoamini kuponywa maradhi baada ya kutafuta tiba hospitali bila mafanikio, kupata utajiri na miujiza ya aina mbalimbali katika maisha yao baada ya kuhangaika kwa muda mrefu.

Watu wanaoamini hayo hawapo Tanzania pekee au Afrika, bali katika maeneo mengi duniani na hunununia bidhaa zinazouzwa kanisani kama mafuta ya miujiza, maji, chumvi, fagio na fulana wakiamini zina nguvu ya uponyaji.

Miongoni mwa wahubiri wanaitoa huduma za aina hiyo ni Mtume Boniface Mwamposa ‘Bulldoza’ ambaye pamoja na huduma nyingine, hutoa ya kukanyaga ‘mafuta ya upako’.

Inadaiwa kuwa baada ya watu kukanganya mafuta hayo hupata miujiza kwa kupata utajiri, kazi, ndoa na kuponywa magonjwa.

Juzi wakati wa huduma hiyo mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, watu walisukumana na kukanyagana na kusababisha watu 20 kupoteza maisha na wengine 16 kujeruhiwa.

Tukio hilo limegusa watu wengi akiwamo Rais John Magufuli ambaye alitoa wito kwa Watanzania kuchukua tahadhari kwenye matukio yote yenye viashiria vya hatari ikiwamo mikusanyiko ya watu.

Wakati Rais Magufuli akitoa kauli hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira alisema hilo ni tatizo kubwa kwa kuwaamini watu kwamba watamaliza shida zao.

“Naamini hizi taasisi imara za dini zingetoa mafunzo mazuri, watu wasingekuja kusumbuliwa huku. Hawa ni wafanyabiashara. Kila kitu wanachofanya kinauzwa. Maji yanauzwa. Tumeona na itabidi tuchukue hatua.

“Dhana hii ya mafundisho ndio inaonekana ni tatizo na matokeo yake ndio haya,” anasema na kuongeza kuwa ingawa watu wanalalamika maisha ni magumu, lakini fedha wanazopata hupeleka katika huduma za aina hiyo.

Wachungaji wengine

Mbali na mtume Mwamposa, wapo watumishi wengine wanaotoa huduma kama hizo. Mfano Getrude Rwakatale ambaye hivi karibuni alisikika akitangaza kuwapo kwa huduma ya ‘upepo wa kisulisuli’.

Akiwa madhabahuni, Mchungaji Rwakatare wa Kanisa la Assemblies of God lililopo Mikocheni B jijini Dar es Salaam aliwaita wanawake na wasichana ambao hawajaolewa ili awafanyie maombi na watapata wenza wao kwa ‘upepo kwa kisulisuli’

“Nimefurahi maana nimeona ujumbe umefika kwenye jamii na umewagusa wanawake na wanaume kwa kuwa tatizo hilo lipo na pande zote zina uhitaji.”

Mwingine ni Mchungaji wa kanisa la Maombezi, Anthony Lusekeko ‘Mzee wa Upako’ ambaye alisema Mungu alimpa maono ya maombezi, miujiza na ishara na amekuwa akitumia vyombo vya habari vya TV, redio na magazeti kutangaza huduma zake.

Katika moja ya mahubiri yake, Mzee wa Upako amepata kunukuliwa akisema kuwa “kufa maskini ni ujinga, halafu ukute ulipata nafasi na fursa mbalimbali’

Naye Mchungaji Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima anatoa huduma zinazofanana na hizo na anafahamika kwa utajiri kiasi kwamba sasa anadaiwa kumiliki helikopta na aliwahi kudai kuwa na mpango wa kununua treni.

Alisema chanzo cha utajiri wake ni kusafiri nje ya nchi kutoa huduma na kwamba amekuwa akilipwa dola 1,000 za Marekani (Sh2.4 milioni) kwa saa moja.

“Nikienda Japan naweza kutoa huduma miezi mitatu sijawahi kusafiri na hela mfukoni, hela zote zinakuja kwa benki mpaka hapa” alisema.

Gwajima anatajwa kuwa na utajiri mkubwa akimiliki jengo lenye ghorofa nne maeneo ya Salasala jijini Dar. Pia anamiliki chopa kwa ajili ya kueneza Injili huku akiwa amepanga kuingiza ndege yake binafsi nchini.

Pamoja na hayo, Gwajima anamiliki magari ya kifahari kama Hummer H2, magari ya kawaida na mabasi yanayotumika kubeba waumini wake na ana mpango wa kujenga kanisa kubwa nchini Tanzania ambalo litakuwa kubwa kuliko yote Afrika.

Wengine na utajiri

Askofu Mkuu au Nabii George David ‘Geordavie’ wa Kanisa la Ngurumo ya Upako la jijini Arusha naye anadaiwa kuwa na utajiri akimiliki majumba ikiwamo ghorofa analoishi na familia yake lililopo Njiro jijini Arusha.

Eneo hilo analoishi limepewa jina la Mji wa Daudi kutokana na kujengwa kifahari. Mbali na mahekalu ya kifahari, pia Geordavie anayerusha vipindi vyake kupitia Televisheni ya Channel Ten, anamiliki chopa (helkopta) binafsi anayoitumia kwenye shughuli zake za kuhubiri neno la Mungu ndani na nje ya nchi.

Pia anamiliki kituo cha Redio cha Ngurumo ya Upako FM cha jijini Arusha, anasifika kwa kutembea na ulinzi mkubwa na msafara wa magari ya kifahari kama Rais wa nchi yakiwemo Toyota Land Cruiser V8 Super Charger, Range Rover Sport, Land Rover Discovery na mengineyo.

Nabii Josephat Mwingira wa Kanisa la Efatha Ministry lililopo Mwenge jijini Dar, naye anatajwa kumiliki jumba la ghorofa moja maeneo Mikocheni B jijini Dar.

Pia Mwingira anatajwa kuwa mmiliki wa iliyokuwa Benki ya Efatha ambayo ilisitishiwa usajili na Serikali iliyopo Mwenge jijini Dar. Anatajwa kuwa miongoni mwa watumishi wa Mungu mabilionea akimiliki baadhi ya viwanja na mashamba mkoani Pwani.

Askofu Zacharia Kakobe wa kanisa la Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, anatajwa kumiliki nyumba ya kawaida Kijitonyama jijini Dar es Salaam.

Inadaiwa ni mmoja wa wachungaji wenye utajiri na mwaka 2018 Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilimpekua na kueleza kuwa ilimkuta na kiasi kikubwa cha fedha alichokuwa amehifadhi kanisani badala ya benki.

Kakobe alipata kukaririwa akisema kuwa ana fedha nyingi kuliko Serikali na ana uwezo wa kumkopesha fedha waziri yeyote pindi akiombwa.

Nabii Nicolaus Suguye wa Kanisa la Huduma ya The Word of Reconciliation Ministries (WRM) la Kivule- Matembele jijini Dar es Salaam naye anadaiwa kumiliki magari na majumba ya kifahari.

Pia anamiliki kituo cha Televisheni cha WRM TV huku akidaiwa kuwa na mpango wa kuingiza ndege yake binafsi nchini.

Eliudi Isangya ni Askofu Mkuu wa Kanisa la International Evangelism lililopo Sakila wilayani Arumeru jijini Arusha.

Mchungaji Isangya anatajwa kumiliki kanisa hilo kubwa, majumba, magari na ndege binafsi. Kuna taarifa kuwa alitaka kujenga uwanja wake wa ndege eneo la Sakila, lakini alinyimwa vibali.

Wahubiri nje ya nchi

Nabii Mchungaji Shepherd Bushiri wa Malawi anadai kutenda miujiza na kuvutia maelfu ya waumini.

Nabii huyo wa kanisa la Enlightened Christian Gathering (ECG) anadai ana dawa ya walioathirika na virusi vya Ukimwi, anawaponya vipofu, maskini wanakuwa matajiri, na wakati mmoja hivi karibuni alidaiwa kuonekana akitembea hewani. Amekuwa akipata wafuasi kutoka ndani na nje ya Malawi.

Mhubiri huyu anafahamu kuhusu shutuma dhidi yake, kwani baadhi ya watu wanamuita msanii na mhubiri bandia, lakini amekua akizipuuzia.

‘’Kanisa langu si kwa ajili ya kila mtu, isipokuwa kwa wale wanaoamini,” alisema.

Mchungaji maarufu nchini Kenya Ng’ang’a wa kanisa la Neno Evangelist Ministry amekuwa akizua gumzo kutokana na aina ya huduma anazotoa.

Mchungaji huyo amekuwa akichapa makofi waumini wake na wakati mwingine alimuombea muumini mmoja kwa kumkaba kwenye shingo hadi kuzimia.

Joseph Prince, mchungaji kutoka Singapore anatajwa kuwa na utajiri wa Dola za Kimarekani Milioni 5. Hufanya ibada ambazo pia hurushwa moja kwa moja kwenye mtandao wa youtube, hivyo kupata umaarufu mkubwa.

T.B Joshua, ni mzaliwa wa Nigeria na anatajwa kuwa na utajiri wa Dola za Kimarekani Milioni 10.

Kwa Nigeria, mchungaji huyu ni maarufu kama Nabii na ana watu wanaomfuatilia kwenye mtandao wa Facebook zaidi ya Milioni 1.5.

Ingawa kuna uhuru wa kuabudu nchini, ni wakati sasa kwa Serikali kuwa makini kutokana na kushamiri kwa makanisa kila uchwao . Tahadhari ichukuliwe kabla hayajatokea majanga makubwa zaidi.