Vifo vya wajawazito na watoto vyapungua Manyara

Mkurugenzi wa miradi bunifu wa Pharm Access, Zamaradi Mbega akizungumza kwenye ufungaji wa mradi wa Mom Care uliofanyika mji mdogo wa Katesh Wilaya ya Hanang' mkoani Manyara. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

  • Kupitia mradi wa kumjali mama wa Pharm Access unaomaliza muda wake,  vifo vya wajawazito vimepungua  kutoka wanane hadi wawili kwa mwaka mkoani Manyara.

Babati. Idadi ya vifo vya wanawake wajawazito mkoani Manyara,  imepungua kutoka wanawake wanane kwa mwaka hadi wawili kwa mwaka kutokana na mafunzo ya elimu ya uzazi na vifaa kwa wajawazito.

Hayo yameelezwa leo Machi 14, 2024 na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Hanang (DMO), Dk Mohamed Kodi wakati wa kuhitimisha mradi wa Mom Care wa shirika la Pharm Access katika mji mdogo wa Katesh.

Dk Kodi amesema wakati shirika hilo likianza mradi huo mwaka 2019,  idadi ya vifo vya wanawake waliokuwa wanaojifungua watoto ilikuwa asilimia nane ila hivi sasa ni asilimia mbili.

Amesema mbali ya faida hiyo,  mradi huo pia umesaidia kutoa elimu na kufanikisha asilimia kubwa ya wanawake wajawazito kutojifungua nyumbani na kwenda kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitalini.

"Kupitia mradi huu tuliwafuatilia kwenye mfumo kinamama walio karibu kujifungua na kuhimiza waende hospitali na vifaa vya kujifungulia walipata kwa wakati pindi wakihitaji," amesema Dk Kodi.

Mmoja kati ya wanawake waliojifungua watoto kupitia mradi huo, Pendael Gwaltu amesema Pharm Access imefanikisha wanawake wengi wajawazito kutojifungua nyumbani.

"Binafsi kupitia mradi huu nimenufaika kwa kupata vifaa vya kujifungulia na elimu ya uzazi kabla na baada ya kujifungua watoto," amesema Gwaltu.

Mkurugenzi wa miradi bunifu wa Pharm Access, Zamaradi Mbega,  amesema mradi huo ulianza mwaka 2019 na kuhudumia wilaya za Hanang' na Babatii ukiwa na mafanikio mengi.

Mbega ametoa wito kwa halmashauri hiyo kusimamia mambo yote mazuri yaliyoanzishwa na mradi huo,  ili yaweze kudumu na kuwa faida kwa jamii.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang' Francis Namahungo amewataka waganga na wauguzi kusimamia ubora wa huduma ili vifo visijirudie

Namahungo amesema mradi huo uliomalizika wa Pharm Access, umekuwa na manufaa makubwa kwa jamii.

Amesema pamoja na kupunguza vifo kwa kina wanawake wajawazito, jamii imekuwa na uelewa mpana kwa kufuata huduma za afya kwenye maeneo rasmi.