Vifungashio vya bahasha vyenye siri za watu vinapotapakaa mtaani

Dar es Salaam. Umewahi kukunjua bahasha uliyofungiwa bidhaa dukani kujua nini kimeandikwa katika karatasi zilizotumika? Kama bado anza kuchunguza leo.
Baadhi ya bahasha hizo zimekuwa zikibeba taarifa za muhimu zikiwemo siri za watu kama nakala ya vitambulisho vya taifa, karatasi za urejeshaji wa laini za simu zilizopotea na hata vyeti vya shule, vyakuzaliwa na mitihani mbalimbali.
Kuibuka kwa vifungashio hivyo kulitokana na kupigwa marufuku kwa mifuko ya plastiki na kufanya watu wengi kubuni namna wanayoweza kuwafungia wateja wao bidhaa, ndipo wakaja na ubunifu wa bahasha hizo.
Lakini utengenezaji wa bahasha hizo haujazingatia namna wahusika wanaweza kukwepa kusambaza taarifa binafsi au za siri za watu na taasisi mbalimbali.
Licha ya wahusika kuamini kuwa taarifa hizo zimeisha matumizi lakini huweza kuwa hatari ikiwa zitatumika kinyume na ilivyokusudiwa wakati wa kuzikusanya.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umebaini baadhi ya bahasha hizo zimekuwa zikibeba taarifa za muhimu, mfano halisi ni tukio moja ambapo ilikutwa nakala ya cheti cha kuhitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Jambo hili lilibua hisia tofauti miongoni mwa watu huku baadhi wakidai huenda matukio ya utapeli kwa njia ya simu, ya watu wenye msema maarufu ‘tuma kwenye namba hii’ yanakithiri kutokana na taarifa za watu kusambaa kiholela.
“Sasa kama huyu alikuwa anarejesha laini yake, kaweka namba za watu wake wa karibu nne sijui tatu ukijumlisha na yake tapeli si anazitumia vile anavyotaka bila shida,” alisema Yassin Kombo, mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam.
Akiwa ni mfanyabiashara wa duka, Kombo anasema wakati mwingine analazimika kuzikagua bahasha hizo nje na ndani kwa kile alichokihofia kuwa anaweza kuuza taarifa zake mwenyewe au za mtu wake wa karibu na kuleta shida.
“Sasa kama mtu yupo huko hajui kama copy (nakala) ya kitambulisho chake mtu kafungiwa maandazi, hata wewe unaweza kujikuta copy ya kitambulisho chako iko hapa,” alisema mfanyabiashara huyo akisisitiza kuwa jambo hilo ni hatari.
Maua Athuman anaungana na Kombo akisema jambo hilo linapaswa kuangaliwa vizuri na masharti yawekwe hususani katika matumizi ya karatasi zilizo na taarifa nyeti.
“Vinginevyo, kutakuwa hakuna usiri wa taarifa zetu, umeenda kutafuta huduma kwa nia nzuri umehudumiwa baadaye badala ya taarifa zako kutunzwa au kuharibiwa zinauzwa kama uchafu kwa watu wenye matumizi mengine,” alisema Maua.


Ni biashara nzuri
Mmoja wa watengenezaji wa bahasha hizo, Geofrey Mzurikwao alisema ununuaji wa karatasi husika kutoka kwa watu tofauti hufanyika kwa kupima kilo, hivyo ni ngumu kuanza kukagua moja baada ya nyingine kujua ipi haistahili kutumika.
“Sasa mtu umeuziwa kilo 30, utaanza kukagua mojamoja kujua ipi utumie ipi usitumie, kweli? Ni vigumu, hata hao wanaouza maana yake hawana matumizi nayo tena, wanasafisha ofisi,” alisema.
“Ingekuwa ni vyema kila ofisi kulingana na ‘unyeti’ wa huduma wanazotoa watafute namna ya kuharibu taarifa za wateja baada ya kuzitumia badala ya kuruhusu ziingizwe mtaani kama karatasi chakavu.
Mmoja wa watu ambao taarifa za urejeshaji laini yake zilikuwa katika bahasha alishangaa huku akieleza kuwa hajui chochote.
“Hadi nimeshasahau, ilikuwa mwaka 2019 leo hii taarifa zangu zinazunguka kwenye bahasha, kazi ipo, sasa siri zetu wateja itakuwaje,” alihoji dada huyo ambaye hakutaka kutajwa jina.


Mamlaka zatia neno
Novemba 27 mwaka jana, Rais Samia Suluhu Hassan aliwataka makatibu muhtasi kutunza siri za Serikali kwa uadilifu na weledi, kwani wasipofanya hivyo watadhulumu haki za watu.
Alitoa kauli hiyo kwenye mkutano mkuu wa 10 wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (Trampa) uliofanyika Arusha.
“Chukua picha wewe ni mtunza kumbukumbu kwenye sekta ya kilimo, kuna mambo ya ruzuku hufanyi uadilifu unaacha kompyuta, kaingia m…