Vijana wabunifu wanavyogeuzwa kuwa wataalamu wa teknolojia
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk Amos Nungu, akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Ujuzi wa Vijana Duniani yaliyofanyika leo, Julai 15, 2026, katika ukumbi wa Buni Hub uliopo ndani ya Costech, jijini Dar es Salaam. Maadhimisho hayo yaliwakutanisha wanafunzi wabunifu kutoka shule za sekondari na vyuo mbalimbali nchini.
Muktasari:
- Safari ya Tanzania kuwawezesha vijana wabunifu ikiwemo programu mbalimbali za ubadilishwaji taka za kieletroniki kuwa fursa ya uzalishaji bidhaa pamoja na kuwadhamini wanafunzi kusoma sayansi, teknolojia ya akili unde (AI).
Dar es Salaam. Tanzania imebainisha utekelezaji wa programu za kiteknolojia ikiwemo ya ubadilishwaji taka za kieletroniki kuwa fursa ya uzalishaji bidhaa pamoja na kuwadhamini wanafunzi kusoma sayansi, teknolojia ya akili unde (AI) ikiwa ni sehemu ya kukumbatia vijana katika ubunifu.
Kadhalika, kuzalisha wataalamu wenye maarifa ya kupambana na mabaya ya teknolojia kama AI, uelewa wa kutosha na wataalamu wa mifumo ya kisasa.
Hayo yamebainishwa leo Jumatano, Julai 15, 2026 kwenye siku ya ujuzi wa vijana duniani iliyofanyika ukumbi wa Buni Hub uliopo Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) Dar es Salaam. Maadhimisho yaliyohusisha wanafunzi wabunifu wa sekondari na vyuo hapa nchini.
Wanafunzi kutoka shule za sekondari na vyuo mbalimbali wakifuatilia maadhimisho ya Siku ya Ujuzi wa Vijana Duniani yaliyofanyika leo, Julai 15, 2026, katika ukumbi wa Buni Hub uliopo ndani ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), jijini Dar es Salaam.
Akidadavua zaidi, Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dk Amos Nungu, amesema mwaka jana wizara ya elimu ilizindua programu maalumu ya kuwapa nafasi vijana kusoma masomo ya sayansi kupitia udhamini wa Samia Scholarship.
Amesema tukio hilo la kusherehekea ujuzi wa vijana wanalifungamanisha na miaka 40 ya sayansi pamoja na ubunifu wa Costech ambapo taasisi hiyo imekua mstari wa mbele kuhakikisha mfumo wa ubunifu nchini unaimarika.
“Ndio maana kuna programu maalumu inayoratibiwa ya Samia Scholarship ili kuwawezesha vijana waliofaulu sayansi na hesabu kwenda kusomea masuala ya sayansi na AI. Vijana wameenda kusoma nje na wanalipiwa na Serikali asilimia 100.”
“Kati ya vijana 50 walioenda chuo cha Nelson Mandela mwaka jana, 16 wameenda kusoma Afrika Kusini, 32 wameenda Ireland na wawili wanasema huko nje, kwa hivyo vijana waelewe inawezekana,” amebainisha.
Wanafunzi kutoka shule za sekondari na vyuo mbalimbali wakifuatilia maadhimisho ya Siku ya Ujuzi wa Vijana Duniani yaliyofanyika leo, Julai 15, 2026, katika ukumbi wa Buni Hub uliopo ndani ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), jijini Dar es Salaam.
Amesema hata katika Dira ya 2050 suala zima la ubunifu limepewa kipaumbele hivyo kinachofanyika sasa ni kuishi mwongozo huo. Wapo vijana wengi wamepita Buni Hub vivyo tunaendelea kushirikiana na vijana.
Katika tukio hilo, Mkurugenzi wa Dar Teknohama Bussiness Incubator, Kituo cha Biashara (DTBI), Patience Karua amesema vijana wanajifunza sehemu mbalimbali za kompyuta na namna ya kutumia kompyuta zilizokwisha tumiwa kutengeneza masuluhisho mbalimbali.
Mkurugenzi wa mawasiliano kampuni ya Airtel, Beatrice Singano amesema nia na madhumuni ni kuona vijana wengi zaidi wanafanikiwa katika eneo hilo la ubunifu kwenye teknolojia.
Mmoja washiriki wa programu ya kubadilisha taka za kielekroniki kuwa bidhaa, ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Kijitonyama amesema amejifunza kutumia keyboard na kazi zake.