Vijana watuzwa Sh30 milioni bunifu za kukabili upotevu wa nishati
Miongoni mwa Vijana walioshinda mashindano hayo.
Muktasari:
- Washindi hao ni Chap Solutions, Sems Innovators na Maji Guard, ambapo kila kikundi kilipokea Sh10 milioni pamoja na mwongozo wa kitaalamu na fursa ya kuunganishwa na taasisi za fedha ili kuendeleza bunifu zao kutoka hatua ya majaribio hadi matumizi ya kibiashara.
Dar es Salaam. Vikundi vitatu vya wabunifu vinavyotoa suluhisho za kupunguza upotevu wa nishati na maji vimeibuka washindi wa Mashindano ya Kitaifa ya Ubunifu wa Ufanisi wa Nishati 2026 na kujinyakulia jumla ya Sh30 milioni.
Washindi hao ni Chap Solutions, Sems Innovators na Maji Guard, ambapo kila kikundi kilipokea Sh10 milioni pamoja na mwongozo wa kitaalamu na fursa ya kuunganishwa na taasisi za fedha ili kuendeleza bunifu zao kutoka hatua ya majaribio hadi matumizi ya kibiashara.
Mashindano hayo yamefanyika chini ya Mradi wa Ushirikiano wa Kijani unaofadhiliwa na Ubalozi wa Ireland, yakitekelezwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) na Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO), yakilenga kuhamasisha matumizi bora ya nishati na kutambua bunifu zinazotoa suluhisho kwa changamoto za kijamii.
Akizungumza katika hafla ya utoaji wa tuzo, Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO, Profesa Mkumbukwa Mtambo, amesema ubunifu haupaswi kuishia kwenye mawazo pekee bali unapaswa kuungwa mkono na teknolojia zinazofaa, utafiti wa vitendo na ushirikiano wa karibu na sekta ya viwanda.
“Ufanisi wa nishati unahitaji teknolojia zinazofaa kwa mazingira yetu, utafiti uliotumika na ushirikiano imara na sekta ya viwanda. Tutaendelea kuwasaidia wabunifu kujaribu, kuboresha na kuimarisha suluhisho zinazokidhi changamoto halisi za nishati nchini,” amesema.
Meneja wa Programu zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi, mazingira, nishati na uchumi wa buluu katika Ubalozi wa Ireland, Fazal Issa, akizungumza wakati wa hafla ya kuwapatia tuzo vijana walioshinda shindano la mawazo bunifu yanayotatua changamoto za kijamii nchini. Hafla hiyo ilifanyika jana jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake, Meneja wa Mpango anayemwakilisha Balozi wa Ireland, Fazal Issa, amewapongeza washindi hao akisema bunifu zao zinaonesha uwezo mkubwa wa vijana wa Kitanzania katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kuchochea maendeleo endelevu.
Mtaalamu wa Programu wa UNDP, Dk. Abbas Kitogo, amesema ufanisi wa nishati ni njia muhimu ya kupunguza gharama za matumizi, kuimarisha usalama wa nishati, kupunguza uzalishaji wa hewa chafu na kuharakisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
Amesema mashindano hayo yalipokea zaidi ya maombi 170 kutoka maeneo mbalimbali nchini, ambapo baada ya mchujo timu tano zilichaguliwa kushiriki kambi maalumu ya siku tatu iliyowajengea uwezo wa kiufundi, biashara na uandaaji wa mifano ya bunifu zao kabla ya kuwasilisha mbele ya majaji.
Katika bunifu zilizoshinda, Chap Solutions walitengeneza mfumo mahiri unaotumia vihisi vya watu na mazingira kudhibiti matumizi ya taa katika vyuo na majengo ya umma, hatua inayosaidia kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya umeme.
Sems Innovators walibuni mfumo wa kusimamia na kuboresha matumizi ya umeme katika maeneo ya pamoja, ikiwemo vyuo na hosteli za wanafunzi, kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji na kuhamasisha matumizi endelevu ya nishati.
Kwa upande wa Maji Guard, walitengeneza mfumo unaotumia akili bandia (AI) na vihisi vya sauti vya gharama nafuu kugundua uvujaji wa maji chini ya ardhi, hatua inayolenga kupunguza upotevu wa maji na nishati inayotumika katika usambazaji wake.
Mbali na fedha za ushindi, timu hizo zitaendelea kupata msaada wa kiufundi, ushauri wa kitaalamu na fursa za ushirikiano na taasisi mbalimbali ili kuendeleza bunifu zao na kuzifikisha sokoni.
Mashindano ya Ubunifu wa Ufanisi wa Nishati 2026 yanaonesha dhamira ya pamoja ya Wizara ya Nishati, TIRDO, UNDP na Ubalozi wa Ireland ya kuimarisha mfumo wa ubunifu nchini, kuwawezesha vijana na kuharakisha upatikanaji wa suluhisho za vitendo kwa matumizi bora ya nishati na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.