Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wizara ya Afya yawapa ‘kibarua’ wanasayansi

Mkurugenzi wa Mafunzo na Maendeleo ya Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Afya, Dk Saitore Laizer, akizindua Kongamano la Tano la Kisayansi la Chuo cha Sayansi za Afya cha Mtakatifu Fransisko Ifakara (SFUCHAS). Picha na Hamida Shariff.

Muktasari:

  • Kongamano hilo linatarajiwa kuwa fursa muhimu ya kujadili matokeo ya tafiti, kubadilishana uzoefu na kuibua ubunifu utakaosaidia kuimarisha huduma za afya, kuchochea maendeleo ya kisayansi na kuchangia ustawi wa jamii kwa ujumla.

Morogoro. Mkurugenzi wa Maendeleo ya Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Afya, Dk Saitore Laizer amesisitiza umuhimu wa kuwakutanisha wanasayansi, watafiti na wataalamu wa sekta mbalimbali ili kujadili masuala ya kisayansi yatakayochangia kupatikana kwa suluhisho, bunifu na kuboresha huduma za afya nchini.

Dk Laizer ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Juni 25, 2026, wakati akifungua kongamano la Tano la Kisayansi la Chuo cha Sayansi za Afya cha Mtakatifu Fransisko Ifakara (SFUCHAS), linalolenga kuchochea mafanikio katika kufikia Lengo la Tatu la Maendeleo Endelevu (SDG 3) kupitia ujumuishaji wa tafiti, teknolojia na suluhisho za afya zinazotokana na jamii.

Akizungumza katika kongamano hilo, Dk Laizer amesema mijadala ya kisayansi inayowakutanisha wataalamu kutoka nyanja mbalimbali ni muhimu katika kutafuta majibu ya changamoto zinazoikabili sekta ya afya na jamii kwa ujumla.

“Nasisitiza umuhimu wa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwakutanisha wanasayansi, watafiti na wataalamu mbalimbali kwa lengo la kujadili masuala ya kisayansi yatakayosaidia kuibua suluhisho bunifu katika kuboresha huduma za afya nchini,” amesema.

Wadau mbalimbali wakishiriki Kongamano la Tano la Kisayansi la Chuo cha Sayansi za Afya cha Mtakatifu Fransisko Ifakara (SFUCHAS), lililolenga kuchochea mafanikio ya kufikia Lengo la Tatu la Maendeleo Endelevu (SDG 3) kupitia ujumuishaji wa tafiti, teknolojia na suluhisho za afya zinazotokana na jamii (Generating Impact for SDG 3: Integrating Research, Technology and Community-Based Health Solutions), lililofanyika leo. Picha na Hamida Shariff.


Aidha, ameipongeza SFUCHAS kwa kuendelea kuandaa makongamano ya kisayansi na kuitaka kuongeza wigo wa shughuli hizo ili kufikia kiwango kikubwa zaidi cha kitaifa.

Amesema makongamano hayo yana mchango mkubwa katika kutambua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii na kusaidia kupatikana kwa njia bora za kuzitatua kupitia tafiti na ubunifu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kukipa SFUCHAS hadhi ya kuwa chuo kikuu huru cha afya kutokana na mchango wake katika utoaji wa elimu ya afya na ongezeko la mahitaji ya huduma zake za elimu.

Kyobya amesema idadi ya wanafunzi wanaojiunga na chuo hicho kutoka maeneo mbalimbali ya nchi imekuwa ikiongezeka, jambo linaloonyesha umuhimu wake katika kuzalisha wataalamu wa afya wanaohitajika nchini.

Pia amekipongeza kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuandaa kongamano hilo, akieleza kuwa limekuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wataalamu wa afya, watafiti na wanasayansi kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na maarifa.