Watakiwa kuhamasisha utamaduni wa uchangiaji damu kwa hiari
Muktasari:
- Wadau wa afya wanaamini kuwa ushirikiano kati ya hospitali, taasisi za dini, mashirika ya kijamii, kampuni binafsi na wananchi unaweza kuongeza kiwango cha damu kinachokusanywa nchini na hivyo kupunguza changamoto ya uhaba wa damu inayojitokeza mara kwa mara katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Tanga. Wadau wa afya wameeleza kuwa kujenga utamaduni wa wananchi kujitolea kuchangia damu mara kwa mara pamoja na taasisi za umma na binafsi kuweka ratiba endelevu za uchangiaji damu, ni miongoni mwa njia muhimu za kukabiliana na changamoto ya uhaba wa damu katika bohari za damu nchini.
Wamesema hatua hiyo inaweza kusaidia kuongeza akiba ya damu inayohitajika kuokoa maisha ya maelfu ya wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo kila siku, wakiwamo wanawake wanaopoteza damu wakati wa kujifungua, waathirika wa ajali za barabarani, watoto wenye upungufu wa damu na wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji katika hospitali mbalimbali.
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo ni miongoni mwa vituo vya afya vinavyokabiliwa na changamoto ya upungufu wa damu kutokana na mahitaji makubwa yanayozidi kiwango kinachopatikana kupitia uchangiaji wa hiari.
Mkuu wa Idara ya Maabara katika Hospitali hiyo, Sinde Simon akizungumza leo Alhamisi, Juni 25, 2026 hospitalini hapo, amesema hospitali hutumia wastani wa chupa za damu kati ya 650 na 700 kwa mwezi, huku kiwango kinachopatikana kwa sasa kikiwa kati ya chupa 450 na 500 pekee.
Simon anatoa kauli hiyo wakati uchangiaji wa damu unaendelea Mission Tanga katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo unaendelea.
Uchangiaji huo unadhaminiwa na Bilal Muslim, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kumbukumbu ya shahada ya Imam Hussein bin Ali (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), aliyeuawa katika tukio la Karbala nchini Iraq mwaka 61 Hijria.
Akizungumzia hali ya upatikanaji wa damu, Simon amesema huduma ya damu salama inategemea kwa kiwango kikubwa ushiriki wa wananchi katika uchangiaji wa hiari.
“Huduma ya damu salama hupatikana pale jamii inapojitokeza kuchangia damu. Sisi kama watoa huduma tungependa kuona wananchi wanajitokeza wakati wote ili damu ipatikane muda wote, kwa sababu wanaohitaji damu wapo kila siku,” amesema Simon.
Amesema damu ni rasilimali muhimu ambayo haiwezi kutengenezwa viwandani wala kupatikana kwa njia nyingine isipokuwa kupitia watu kujitolea kuichangia.
“Damu hainunuliwi wala haiuzwi mahali popote. Mimi na wewe tukijitolea kuchangia damu tunawezesha taasisi zetu za afya kuwa na benki imara za damu zinazookoa maisha ya watu wengi,” amesema.
Simon amesisitiza umuhimu wa viongozi wa dini, kisiasa na kijamii kushiriki katika kuhamasisha uchangiaji damu ili kujenga utamaduni endelevu wa utoaji damu nchini.
“Itapendeza kuona kila kiongozi wa dini, wa kisiasa au wa kijamii akitumia nafasi yake kuhamasisha watu wake kuchangia damu. Hii itasaidia kujenga utamaduni wa kudumu wa uchangiaji damu nchini,” amesema.
Ameongeza kuwa taasisi mbalimbali zinaweza kuweka ratiba maalumu za uchangiaji damu kama sehemu ya shughuli zao za kijamii ili kusaidia kuongeza akiba ya damu katika hospitali na vituo vya afya.
“Mfano mzuri ni Bilal Muslim Mission ambao kila mwaka wameweka ratiba ya kuchangia damu. Hii inatupa uhakika kwamba kila mwaka wanakuja kuongeza akiba ya damu. Taasisi nyingine zinaweza kuiga mfano huu kwa manufaa ya jamii,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mawasiliano na Mahusiano wa Bilal Muslim Mission Tanga, Sheikh Sajad Ngao amesema taasisi hiyo imeendelea kushiriki shughuli za uchangiaji damu kama sehemu ya kuenzi mafundisho ya kujitolea na kuwajali wengine yaliyoachwa na Imam Hussein bin Ali (AS).
“Imam Hussein (AS) alijitoa kwa ajili ya kutetea haki na maslahi ya watu. Sisi tunajitolea damu kwa lengo la kuwasaidia wagonjwa na wenye uhitaji wa huduma hiyo, kama sehemu ya kuendeleza ujumbe wa kujitolea kwa ajili ya wengine,” amesema Shehe Ngao.
Mmoja wa washiriki katika utoaji damu, Ayub Said amesema ameamua kuchangia damu kwa kutambua umuhimu wake katika kuokoa maisha ya watu wenye mahitaji mbalimbali ya kiafya.
“Hakuna kiwanda kinachozalisha damu. Damu inatoka kwa binadamu wenyewe. Kama jamii itajitokeza kwa wingi kuchangia damu, tunaweza kuondoa kabisa changamoto ya uhaba wa damu katika hospitali zetu,” amesema Said.