Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Teknolojia inavyoweza kuwa silaha kupambana na bidhaa bandia sokoni

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, akizungumza na wadau katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kudhibiti Bidhaa Bandia Duniani  Kitaifa yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Imeelezwa matumizi ya teknolojia ya kisasa ni miongoni mwa mbinu muhimu zinazoweza kusaidia kudhibiti bidhaa bandia, hasa katika kipindi hiki ambacho biashara nyingi zinafanyika kupitia majukwaa ya kidijitali.

Dar es Salaam. Katika kuimarisha mapambano dhidi ya bidhaa bandia nchini, Tume ya Ushindani Tanzania (FCC) imetakiwa kuanzisha na kupanua matumizi ya teknolojia ya kisasa katika uchunguzi, ufuatiliaji na udhibiti wa bidhaa bandia, hususan katika masoko ya kidijitali.

Wito huo umetolewa leo Juni 25, 2026, na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, alipokuwa mgeni rasmi akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kudhibiti Bidhaa Bandia Duniani yaliyofanyika jijini Dar es Salaam na kuwakutanisha wadau mbalimbali, wakiwemo wafanyabiashara.

Mapunda amesema matumizi ya teknolojia ya kisasa ni miongoni mwa mbinu muhimu zinazoweza kusaidia kudhibiti bidhaa bandia, hasa katika kipindi hiki ambacho biashara nyingi zinafanyika kupitia majukwaa ya kidijitali.

“Matumizi ya teknolojia ya kisasa ni mbinu sahihi inayoweza kusaidia kudhibiti bidhaa bandia, hususan katika masoko ya kidijitali. Ni muhimu kupanua matumizi ya teknolojia hiyo katika uchunguzi na udhibiti wa bidhaa bandia hadi kwenye mipaka ya nchi ili kubaini mianya inayotumiwa kuingiza bidhaa hizo,” amesema.

Ameitaka FCC kuongeza kasi ya uratibu na ushirikiano wa karibu na taasisi nyingine za udhibiti, vyombo vya dola pamoja na mamlaka za forodha ili kuhakikisha taarifa zinashirikishwa kwa wakati na hatua stahiki zinachukuliwa haraka dhidi ya wahusika wa bidhaa bandia.

Amesema umuhimu wa FCC kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya bidhaa bandia kwa afya, usalama wa watumiaji na uchumi wa Taifa.

“FCC iendelee kuendesha kampeni za kitaifa za uhamasishaji zinazolenga kuwahamasisha wananchi kutumia bidhaa bora na salama kwa ajili ya kulinda afya zao,” amesema.

Mapunda ameongeza tume hiyo inapaswa kuendelea kujenga ushirikiano na taasisi mbalimbali za biashara ili kuboresha mifumo ya utambuzi wa bidhaa bandia, utoaji wa taarifa na ushauri wa kitaalamu wakati wa ukaguzi.

Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha uwezo wa rasilimali watu kupitia mafunzo yatakayoongeza ufanisi katika ukaguzi, uendeshaji wa mashauri na utekelezaji wa sheria dhidi ya watu wanaojihusisha na biashara ya bidhaa bandia.

“Ni lazima rasilimali watu iendelee kuimarishwa kupitia mafunzo ili kuongeza ufanisi katika ukaguzi, uendeshaji wa mashauri na utekelezaji wa sheria dhidi ya wale wanaobainika kuvunja sheria kwa kuingiza au kusambaza bidhaa bandia,” amesema Mapunda.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Hadija Ngasongwa amesema mapambano dhidi ya bidhaa bandia yanahitaji ushiriki wa wadau wote na jamii kwa ujumla ili yaweze kuleta mafanikio.

Amesema FCC imekuwa ikiendesha programu mbalimbali za elimu kwa wafanyabiashara na wadau wengine ili kuongeza uelewa kuhusu madhara ya bidhaa bandia kwa uchumi wa nchi na ustawi wa wananchi.

“Tumekuwa tukiwafikia wafanyabiashara na wadau wengine kwa kuwapa elimu kuhusu madhara ya bidhaa bandia kwa uchumi wetu. Miezi miwili iliyopita tulikamata viwanda bubu vilivyokuwa vikizalisha pombe, sigara na vilainishi bandia,” amesema.

Ngasongwa amesema juhudi hizo zinalenga kuwalinda Watanzania dhidi ya athari na hatari zinazoweza kusababishwa na matumizi ya bidhaa bandia, sambamba na kulinda uchumi wa Taifa na biashara halali.

Amesema mafanikio katika vita dhidi ya bidhaa bandia yanategemea ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za serikali, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla.