Mwanzo mpya ushirikiano Tanzania, Msumbiji sekta ya dawa
Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Mavere Tukai (kulia), akimkabidhi zawadi Waziri wa Afya wa Msumbiji, Ussene Isse, leo Juni 25, 2026, alipotembelea makao makuu ya MSD jijini Dar es Salaam akiwa na ujumbe wake kujionea utendaji wa taasisi hiyo.
Muktasari:
- Ushirikiano katika mifumo mzima ya uendeshaji wa taasisi, huduma na matibabu pamoja na upatikanaji wa bidhaa.
Dar es Salaam. Tanzania kupitia Bohari ya Dawa (MSD) na Wizara ya Afya ya Msumbiji zimejadili ushirikiano mpya katika sekta ya dawa utakaowezesha kubadilishana uzoefu wa uendeshaji wa sekta, uongozi na minyororo mzima wa ugavi wa dawa.
Hatua hiyo inafuatia ziara ya Waziri wa Afya wa Msumbiji Ussene Isse, leo Juni 25, 2026 aliyoifanya makao makuu ya MSD jijini Dar es Salaam akiwa na ujumbe wake kujionea utendaji kazi wa taasisi hiyo.
Akizunguza baada ya majadiliano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, amesema wamejadili ushirikiano katika mifumo mzima ya uendeshaji wa taasisi, huduma na matibabu pamoja na upatikanaji wa bidhaa.
“Tumeangalia maeneo gani tunaweza tukashirikiana kutengeneza mifumo endelevu (ile ya kusaidiwa na wafadhili na ya kujiendesha), muundo wa biashara wa kufanyia kazi wa hizi taasisi za dawa.
“Kuna maeneo ambayo sisi tumeboresha zaidi kwenda kibiashara kushirikiana na sekta binafsi, ukuaji wa taasisi katika mapato miundombinu na dijitali,” amebainisha.
Amesema Waziri wa Afya wa Msumbiji amewakaribisha MSD kwenda nchini humo kujifunza, kuwapa uzoefu na kushirikiana kwa pamoja.
Kongole Tanzania
Kwa upande wake, Waziri Isse ameeleza kuvutiwa na mafanikio yaliyofikiwa na MSD katika usimamizi wa dawa na vifaa tiba, akisema uzoefu wa Tanzania unaweza kusaidia kuimarisha mfumo wa afya nchini humo.
Waziri huyo amesema nchi nyingi za Afrika zinakabiliwa na changamoto za afya kutokana na kupungua kwa rasilimali za kifedha huku idadi ya watu ikiendelea kuongezeka.
Pamoja na magonjwa ya kuambukiza, bara la Afrika sasa linakabiliwa na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza, matatizo ya afya ya akili na majeraha yanayohitaji huduma bora za matibabu na upatikanaji wa dawa.
“Uhitaji wa dawa katika bara letu unaendelea kuongezeka. Ndiyo maana tumeshiriki mkutano wa kimataifa kuhusu magonjwa yasiyoambukiza na matumizi ya teknolojia za kidijitali katika sekta ya afya, lakini pia tumepata fursa ya kutembelea MSD ili kujifunza mambo wanayofanya,” amesema.
Waziri huyo amefurahishwa na mafanikio yaliyofikiwa na MSD, akieleza kuwa taasisi hiyo imeonyesha mfano mzuri wa namna mifumo ya usambazaji wa dawa inaweza kuimarishwa kwa kutumia mbinu za kisasa za usimamizi.
Amebainisha Tanzania na Msumbiji zimekuwa na uhusiano wa karibu kwa zaidi ya miaka 50 na kwamba ushirikiano huo unatoa fursa ya nchi hizo kujifunza na kusaidiana katika sekta mbalimbali ikiwemo afya.
Kwa mujibu wa waziri huyo, dira ya MSD inaendana na malengo ya Msumbiji ya kuboresha huduma za afya na kuhakikisha wananchi wanapata dawa na huduma bora kwa wakati.
“MSD ina uzoefu mkubwa katika eneo hili. Ingawa mifumo yetu inaweza kutofautiana, tunaamini kuna mambo mengi tunayoweza kujifunza na kuyatumia nchini Msumbiji,” amesema.
Amesema lengo kuu la nchi za Afrika ni kuboresha ubora wa huduma za afya na kuhakikisha wananchi wanapata matibabu bora, huku dawa zikiendelea kuwa sehemu muhimu ya kuokoa maisha na kuimarisha afya za watu.
Naye, Balozi wa Msumbiji nchini Tanzania, Ricardo Mtumbuida amesema hatua hiyo haiishii kwenye dawa tu bali kuimarisha diplomasia ya mataifa hayo mawili.
“Yapo mambo mengi yanafanana kati yetu lakini Waziri akaona aje kuona na kujifunza ukirejea leo Juni 25, ni siku ya uhuru wa Msumbiji,” amesema.