Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

14 wamepandikizwa uume Hospitali ya Benjamin Mkapa tangu 2023

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya Benjamini Mkapa, Dk Abdalla Baja akizungumza jijini Dodoma leo, Picha na Elidaima Mangela.

Muktasari:

  • Imeelezwa mbali na mafanikio hayo kumekuwa na uzito kwa wenye tatizo hilo kujitokeza kutokana na hofu.

Dodoma. Takribani wagonjwa 14 wamefanikiwa kufanyiwa upandikizaji wa uume katika Hospitali ya Benjamin Mkapa tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo mwaka 2023.

Takwimu hizo zimetolewa leo Alhamisi Juni 25, 2025 na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamini Mkapa, Dk Abdalla Baja wakati akizunguza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dodoma, ambapo amesema huduma hiyo imekuwa ikitolewa na wataalamu wa ndani kwa viwango vinavyokubalika kitaalamu.

Dk Baja amesema wagonjwa hao wamepatiwa huduma kwa gharama ya wastani wa Sh10 milioni kwa mgonjwa mmoja, ikilenga kuwasaidia watu wenye changamoto mbalimbali zinazohitaji matibabu hayo maalumu.

“Mpaka kufikia sasa tumefanikiwa kuhudumia wagonjwa 14, ambao wamepona kabisa tatizo hili ambalo limeonekana kuwa janga katika jamii likileta athari katika eneo la ndoa, watu wanapona kabisa na tungeomba wenye matatizo wasisite kujitokeza,” amesema Dk Baja.


Jinsi uume unavyopandikizwa

Huduma hiyo hutolewa kwa mgonjwa kuwekewa vipandikizi vya plastiki vinavyoitwa silicone kwenye uume, hivyo kuwa na uwezo wa kushiriki tendo la ndoa kama kawaida.

Akizungumza na Mwananchi mwaka 2023, Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa mkojo na uzazi wa Hospitali ya MDM Specialized, Deogratius Mahenda alisema vipandikizi hivyo vinasaidia misuli ya uume kuwa imara.

Vipandikizi hivyo ambavyo ni plastiki vinaingizwa kwenye misuli ya uume na vitaendelea kuwapo kwa maisha yote ya muhusika. Upasuaji hufanyika kwa muda wa saa moja na nusu.

Akifafanua zaidi Dk Baja amesema baada ya upasuaji huo, siku saba za awali zinakuwa za uponyaji na muhusika anatakiwa asubiri kwa mwezi mmoja ndipo aanze kushiriki tendo la ndoa.

“Mwanamume aliyewekwa vipandikizi, hisia zake zitabaki palepale…kama atahitaji kupata watoto ataweza kwa kuwa utoaji wa mbegu hauathiriwi.”

Amefafanua kuwa mwanamume aliyewekewa vipandikizi hategemei mtu amvutie hisia au kuguswaguswa ndipo uume usimame.

"Mwanamume aliyewekwa vipandikizi akitaka kufanya tendo la ndoa anainyoosha, akikubaliana na mwenza wake inatosha, uume anaupindisha.

“Vipandikizi havisababishi maumivu, muhusika anaweza kushiriki tendo hilo kadiri anavyotaka kwa sababu vinauwezesha uume usimame wakati wote,” anasema na kuongeza kuwa akimaliza tendo kuna namna ya kuuweka uume usionekane kama umesimama.

Awali Dk Baja amesema kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya uwekezaji unaofanywa katika sekta ya afya ukilenga kuwezesha utoaji wa huduma maalumu, ambazo hapo awali hazikuwepo ndani ya nchi na zilikuwa na gharama kubwa nje ya nchi.

“Niwasihi watu wenye tatizo hili kuwa wawazi ili kurahisisha utoaji wa huduma hii kwao, kwani wengi wanaofika hapa wanakuwa wazito kujieleza jambo linalochelewesha mchakato wa matibabu kuanza haraka,” amesema.

Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya ndani kutoka hospitali hiyo, Dk Ayubu Mashamba amewahimiza wananchi kupima afya mara kwa mara kuliko kusubiri wanapougua kwani wakiwahi kubaini shida walizonazo na kuanza matibabu mapema, inapunguza gharama na mgonjwa anapona haraka.

Dk Mashamba amesema kitendo hicho kitawawezesha kupata ushauri wa kitaalamu, hatua ya kutafuta ili kupata matibabu sahihi na kuanza matibabu mapema jambo litakalopunguza gharama za matibabu na muda wa kutengamaa.

Naye Daktari bingwa wa magonjwa ya damu, Dk Happiness Igogo, ametoa wito kwa Watanzania wenye uwezo kuchangia mfuko wa matibabu ya figo na selimundu ulioanzishwa na hospitali hiyo kusaidia wagonjwa wasiojiweza ili waweze kupata huduma za matibabu.

Dk Igogo amesema upandikizaji uroto kwa mgonjwa mmoja hufikia takribani Sh75 milioni, huku upandikizaji figo ukigharimu wastani wa Sh45 milioni kiwango ambacho wengi wanashindwa kupata huduma kutokana na hali za vipato vyao.

Amesema hospitali imeanzisha mfuko huo kutokana na gharama hizo kuwa kubwa kwa wananchi wengi, hivyo wameamua kuweka wazi ili Watanzania wenye nia waweze kuchangia ili kuongeza fursa za wagonjwa kupata matibabu kwa wakati na kuokoa maisha yao.