Viongozi wanaoshinda baa kitanzini

Waziri wa Nchi, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene akifungua kikao kazi cha wachunguzi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, mkoani Arusha.

Muktasari:

Wachunguzi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma wameagizwa kufuatilia viongozi wanaojihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili na kuwachukulia hatua za kisheria na si kuishia kuwaonya.

Arusha. Wachunguzi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma wameagizwa kufuatilia viongozi wanaojihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili na kuwachukulia hatua za kisheria na si kuishia kuwaonya.

Waziri wa Nchi, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema wapo viongozi wa umma wanaolalamikiwa kujihusisha na vitendo vya mgongano wa masilahi wanapotimiza majukumu yao, ambao ametaka wachunguzwe na  watakaobainika wachukuliwe hatua za kisheria ili kuleta usawa, utoaji haki kwa wote na kudhibiti mmomonyoko wa maadili.

Amesema hayo leo Machi 18, 2024 kwenye kikao kazi cha wachunguzi wa sekretarieti hiyo waliokutana kujadili utekelezaji wa majukumu yao na changamoto wanazokabiliana nazo.

Simbachawene amesema taasisi hiyo ambayo ni jicho la Serikali katika kufuatilia tabia na mwenendo wa viongozi wa umma, ina jukumu kubwa la kuhakikisha Taifa linaongozwa na watu waadilifu, wanaofuata misingi ya maadili na utawala bora.

"Mbali hata na mgongano wa masilahi, unaweza kumkuta kiongozi wa umma anashinda baa muda wote na analewa hadi kupitiliza, ile si binafsi ni ukiukwaji wa maadili, wachukuliwe hatua za kinidhamu," ameagiza Simbachawene.

Amewataka wachunguzi hao kushughulikia maadili ya viongozi, kushirikiana na wananchi katika kufichua vitendo vya ukosefu wa maadili kwa viongozi, na kuwa wawazi dhidi ya hatua wanazochukua.

"Hata hivyo, mtumie weledi na busara mnaposikiliza malalamiko ya wananchi dhidi ya viongozi wa umma na mfanyie kazi kwa uadilifu mkubwa na ufanisi wa utendaji kazi wenu," amesema.

Awali, Kamishna wa Maadili, Jaji Sivangilwa Mwangesi amesema lengo la kuwakutanisha wachunguzi hao,  ni kujadili changamoto wanazokabiliana nazo katika kushughulikia maadili ya viongozi wa umma.

"Pia tumekutana kupeana mbinu na uzoefu wa namna ya kushughulika na malalamiko hayo, na jinsi ya kuyafanyia uchunguzi hadi kufanya maamuzi," amesema.

Katibu Msaidizi wa Sekretarieti hiyo, Fabian Pokea amesema suala la maadili ni mtambuka, hivyo katika kudhibiti mambo hayo wataendelea kutaja mali na madeni ya viongozi wa umma ili kujenga hofu ya ukiukwaji wa maadili.


"Jambo la maadili linahitaji vita ya kudumu na inataka ushirikishwaji katika kufuata maadili, na uzuri tunapiga hatua. Suala la kutamka mali na madeni ni moja ya mkakati wa kudhibiti na kupatikana uaminifu ili kudhibiti pia mgongano wa kimasilahi," amesema.