VITA VYA KAGERA: Jeshi la Tanzania laingia Kampala – 21

Muktasari:

  • Katika toleo lililopita tuliona maandalizi ya Jeshi la Tanzania kuuvamia na kuumamata mji wa Kampala, Uganda. Hali ya hewa ilikuwa mbaya lakini askari walifanikiwa kukabiliana nayo.
  • Brigedi za 201, 207 na 208 zilijipanga kwa kazi muhimu. Wakati mipango ya kuiteka Kampala ikifanyika katika Ikulu ya Entebbe, Iddi Amin naye alikuwa mjini Kampala na maofisa wa jeshi lake wakipanga namna ya kuulinda mji huo. Hata hivyo mipango yao haikufanikiwa na Kampala ilitekwa. Endelea…

Ingawa Iddi Amin alijiandaa kikamilifu kuilinda Kampala isitekwe na Tanzania, lilikuwa ni suala la muda tu kabla majeshi ya Tanzania hayajauteka mji huo. Brigedi ya 208 ilikuwa ikisonga mbele kuelekea katika mji huo kutokea Kusini.

Luteni Kanali Benjamin Msuya alikuwa akiongoza mapambano hayo akiwa na askari kiasi cha 800. Hawa walikuwa wakielekea katikati ya Kampala. Wakati huo, Brigedi ya 207 ilikuwa inashambulia kutokea Magharibi mwa Kampala wakati Brigedi ya 201 ikiweka vizuizi Kaskazini kuwakabili wanajeshi wa Amin waliokuwa wanakimbia. Upande wa Mashariki uliachwa kuruhusu Walibya kukimbilia Jinja na kuondoka Uganda.

Mashambulizi ya mji wa Kampala yalianza asubuhi ya Jumanne ya Aprili 10, 1979. Majeshi ya Tanzania yalifanikiwa kushinda kila aina ya upinzani wa majeshi ya Amin waliokutana nao, licha ya kukabiliana na hali mbaya ya hewa.

Aprili 10 ni siku ya kihistoria Tanzania na Uganda. Inapaswa kuandikwa katika vitabu vya historia kwa ajili ya vizazi vijavyo vya Waganda.

Majeshi ya Amin yaliyojaribu kupambana na majeshi ya Tanzania yalijikuta yakielemewa. Kwa mfano, katika eneo moja la Barabara ya Jinja, wanajeshi wa Amin waliojaribu kupambana na majeshi ya Tanzania kuvuka vizuizi vilivyowekwa na Brigedi ya 201 iliyokuwa ikiongozwa na Brigedia Imran Kombe, walidhibitiwa. Hadi kufikia jioni askari wanane wa Amin walikuwa wameuawa na magari yao kadhaa yaliharibiwa.

Kutokea upande wa Magharibi mwa Kampala, Brigedi ya 207 iliyokuwa chini ya Brigedia John Butler Walden ilikuwa inaukaribia mji wa kampala. Ilipofika asubuhi kikosi cha Brigedia Walden kikawa tayari kimeteka mji wa Natete na sasa kilikuwa kinaelekea Rugaba. Maeneo ya Kilima cha Kasubi na makaburi ya Kabaka nayo yakawa yametumbukia mikononi mwa majeshi ya Tanzania.

Wakati Luteni Kanali Msuya akijiandaa kupeleka vikosi vyake kupita barabara kuu ya kuelekea Kampala kutokea Kusini, vikosi vingine vya Brigedi ya 208 tayari vilikuwa njiani kuelekea Kampala kupitia Port Bell na gereza lililokuwa na sifa mbaya la Luzira.

Wakati huo mvua ilikuwa imepungua na angalau mawingu mazito nayo yalikuwa yameanza kupungua na anga kufunguka.

Kadiri Kampala ilivyokaribiwa, ndivyo—kwa mara ya kwanza—raia walivyokuwa wakiongezeka na kuwa makundi makubwa barabarani huku wakiwa na majani na matawi ya miti wakiwapungia wanajeshi wa Tanzania waliokuwa wakielekea katikati ya jiji la Kampala. Walijua kuwa mara baada ya Kampala kutekwa, enzi ya Amin Uganda ingekuwa imefikia mwisho.

Luteni Kanali Msuya alikuwa na wasiwasi kuwa katikati ya Jiji la Kampala kwenye majengo marefu huenda kungekuwa na wadunguzi. Hata hivyo, hakuwa na la kufanya kwa sababu raia wengi walikuwa wanaingia mitaani kuwalaki wanajeshi wa Tanzania.

Walipokaribia mzunguko wa Makindye, karibu na Gereza la Makindye lililotumiwa na Amin kama kambi ya mateso, umbali wa kilomita mbili kutoka katikati ya kampala, adui walishambulia. Wakati makundi ya raia wakishangilia, ghafla zilisikika risasi za SMG.

Katika hali ya kushtukiza namna hiyo ilikuwa ni vigumu kwa raia na wanajeshi kupata mahali pa kujificha. Kwa hiyo raia walibaki wakishangaa kinachoendelea. Wanajeshi wengi waliwahi kujificha kwenye mitaro ya maji machafu.

Milio ya risasi iliendelea kuongezeka. Pamoja na mashambulizi hayo, mara moja Luteni Kanali Msuya alitoka na mkuki wake kwa kasi kuelekea mbele bila kujikinga. Alipofika mstari wa mbele kabisa alielezwa kuwa risasi hizo zilielekezwa kwa wanajeshi wa Tanzania kutokea nyuma ya soko lililokuwa eneo hilo. Hata hivyo, hakuna mwanajeshi wala raia aliyepatwa na risasi hizo.

Wakiwa wanatafakari hilo, mara wakaona gari aina ya Mercedes Benz likija kwa kasi kuingia barabarani kuelekea walipokuwa wanajeshi wa Tanzania. Ndani ya gari hilo kulikuwa na askari watano waliokuwa wamevalia kiraia, mmoja ndiye aliyekuwa akiendesha na wengine wakiwa wamening’inia kwenye madirisha ya gari huku wakifyatua risasi.

Ni dhahiri kwamba askari hao walikuwa wamejitoa mhanga. Haikujulikana hasa kwa nini hao wanaume watano waliamua kupambana na jeshi la zaidi ya askari 800 lenye vifaru na silaha nyingine nzito za kivita.

Hata hivyo ndani ya sekunde chache walikuwa tayari wameuawa na wanajeshi wa Tanzania kabla hata hawajaufikia mzunguko wa Makindye kwa gari lao kulipuliwa katika mapigano yaliyodumu kwa dakika 10 tu.

Muda mfupi baadaye askari wachache walitumwa kwenda kupekua eneo la soko ambamo gari lile lilitokea. Lakini hawakukuta chochote cha kutiliwa shaka. Wanajeshi wa Tanzania wakaanza kuimba “Kamata Kampala” ... “Kamata Kampala”, kisha wakaanza tena kutembea kuelekea katikati ya Jiji la Kampala. Raia walirejea tena kwenye makundi yao na kuungana na wanajeshi wa Tanzania na ‘gwaride’ likaanza tena kuelekea Kampala kana kwamba hakuna lolote lililotokea.

Kabla ya kufika katikati ya Kampala kulikuwa na matukio kadhaa ambayo askari wa Amin katika maeneo fulanifulani walijaribu kuwarushia risasi askari wa Tanzania kabla ya kukimbilia mafichoni. Lakini katika matukio yote haya hakuna risasi iliyompata hata mmoja.

Ilipofika saa 11 jioni askari wa JWTZ wakafika eneo la Clock Tower katikati ya Kampala. Hili ni eneo ambalo Septemba 1977 Amin aliwaua kwa kuwapiga risasi watu 12 wa kabila la Langi na Acholi—akiwamo Askofu Janani Luwumu—akiwatuhumu kula njama za kuipindua serikali yake.

Luteni Kanali Msuya na wapiganaji wake hawakuwa na ramani ya kampala, na sasa zilikuwa zimebakia saa mbili tu kabla giza halijaingia. Jambo la kwanza ambalo alipanga kulifanya ni kukiteka kituo cha Redio Uganda.

Itaendelea….