Wakulima Iringa walivyogeukia kilimo cha maharagwe Jesca

Wakulima wa maharagwe Jesca, wakiwa kwenye maonesho ya kilimo Kijiji cha Kiponzelo mkoani Iringa.

Muktasari:

  • Wataalamu wa lishe wamesema maharagwe Jesca yana virubisho vingi

Iringa. Wakulima wa vijiji vya tarafa ya Kiponzelo mkoani Iringa wamechangamkia kilimo cha maharagwe lishe maarufu kwa jina la Jesca ambayo mbali na fursa za kiuchumi, pia yanadaiwa kutibu magonjwa mbalimbali ikiwamo kisukari na nguvu za kiume.

Wataalamu wa lishe wameiambia Mwananchi kuwa ni kweli maharagwe hayo yana virubisho vingi, pia uwepo wa madini chuma na zinki ya kutosha yamefanya yaitwe maharagwe dawa.

Hivi karibuni, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari), Kituo cha Uyole, mkoani Mbeya walikiri kuwa maharagwe hayo yanatibu matatizo mengi ikiwamo kisukari na changamoto ya nguvu za kiume.

Katika maonyesho ya siku ya wakulima yaliyoandaliwa na Shirika la World Vision Tanzania katika Kijiji cha Kiponzelo, wilayani Iringa, wakulima walionyesha maharagwe Jesca waliyokuwa wameweka kwenye vifungashio vya kuanzia kilo moja.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Kilimo cha Kanyaga Twende, Kijiji cha Kidilo, wilayani Iringa, Elizabeth Mwamba amesema tayari wameshavuna zaidi ya kilo 300 za maharagwe na wanasubiri kuyafikisha sokonoi.

Amesema tangu wajikite kwenye kilimo hicho, hali ya maisha imebadilika kutokana na uwepo kwa sababu kila wanapovuna wana uhakika wa kuuza.

“Tumevuna wiki iliyopita, tulipewa mbegu kama kikundi, tumelima mara mbili na kwa sasa kila mmoja amepewa kilo tatu za mbegu akapande shambani kwake. Maharagwe ni matamu na hayasumbui kuiva,” amesema.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Kanyaga Twende, Rajab Mtasiwa amesema kila mwanakikundi amepanda maharagwe hayo baada ya kubaini sifa zake.

“Mafanikio ni makubwa tangu tuanze kulima maharagwe lishe, tumeona mabadiliko kiuchumi na hata kwenye lishe. Kwa wakulima walioshindwa kulima mmoja mmoja wamelima kupitia vikundi vya kiuchumi,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, leo Mei 10, 2024, Mtaalamu wa Afya na Lishe wa Shirika la World Vision, Kanda ya Kati na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Salome Mtango amesema uwepo wa virutubisho hivyo ndio uliofanya wagawe mbegu kwa wakulima wa vijiji vya Kiponzelo kupitia kupitia mradi wa Kihanga kama njia ya kupambana na udumavu lakini, kukuza kipatocha kaya.

“Ni maharagwe lishe, hata mjamzito anaweza kutumia kwa sababu yanaongeza damu kutokana na madini yaliyomo. Tuliwapatia mbegu wakulima, na wamewekeza kwenye kilimo kwa bidii kubwa,” amesema.

Ametaja sifa nyingine ya maharagwe hayo ni kuiva haraka, radha nzuri na hayana gesi kiasi kila mtu anaweza kuyatumia kwa mlo.

Meneja wa Mradi wa Kihanga, Antony Emmanuel amesema awali waligawa kilo 800 kwa wakulima hao wakitaka wazalishe ili yaendelee kuwasaidia kiafya na kiuchumi.

Ofisa Kilimo wa Kata ya Kihanga, Paul Msogole amesema kutokaana na sifa nyingi za maharagwe hayo, mahitaji yamekuwa makubwa baada ya wananchi kuchangamkia fursa ya kilimo hicho.

“Maharagwe haya yamekuwa kama tiba ya udumavu Kiponzelo, binafsi naendelea kuhamasisha kilimo hiki na napita shambani kutoa utaalamu wa kilimo ili wakilima wasipate hasara,” amesema Msogole.

Mfanyabishara wa maharagwe katika Soko Kuu la Manispaa ya Iringa, Jakob Mgeni amesema kilo moja ya maharagwe hayo kwenye vijiji hivyo ni Sh3,000 lakini yakifika sokoni hupanda mpaka Sh4,500 na wakati mwingi, hayapatikani.

“Ni nadra kuyapata maharagwe haya sokoni lakini hata ukipata soko lake lipo juu kutokana na namna wataalamu walivyo elezea sifa zake. Nashauri wakulima waendelee kulima,” amesema Mgeni.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Kheri  James amewapongeza wakulima hao kwa kuona fursa na kuchangamkia kwa kuwekeza kwenye maharagwe lishe ambayo, wameyaongezea thamani.

“Nimeona mmeweka kwenye vifungashio kabisa, hii itaongeza thamani sokoni na niwapongeze sana kwa kuona fursa, lakini pia, World Vision ambao wameleta bidhaa hizi kijijini,” amesema James.