‘Walimu wa sayansi wapo mitaani hawana ajira’

Dar es Salaam. Wakati ufaulu hafifu ukioonekana katika masomo ya sayansi na hesabu kama ilivyobainika katika matokeo ya mitihani ya Taifa ya kidato cha pili na darasa la nne, huku uhaba wa walimu ukitajwa kuchangia hali hiyo, wadau wamesema walimu wa sayansi wapo mitaani ila hawana ajira.
Pia kukosekana kwa maabara, vifaa vya kufundishia na kujifunzia vimetajwa kuwa moja ya sababu ya ufaulu duni kwa kidato cha pili.
Wameyasema hayo ikiwa ni siku moja tangu Baraza la Mitihani Tanzania kutangaza matokeo ya upimaji kidato cha pili na darasa la nne, ambapo asilimia 81.79 ya wanafunzi wamepata daraja F katika somo la fizikia. Asilimia 66.55 walipata F katika somo la kemia huku asilimia 53 wakipata F somo la biolojia.
Akizungumza na Mwananchi, Dk Luka Mkonongwa, ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) alisema walimu wapo mtaani ila hawana ajira.
“Walimu wanaohitimu vyuo wapo wengi, wapo mitaani, kwa sababu tumeona huu upungufu tutafute namna ya kuuondoa. Ikiwa hawatoshi Serikali kwa kushirikiana na vyuo kungekuwa na utaratibu wa kutoa motisha kwa watu watakaoingia katika hiyo mikondo.
“Kuwe na utaratibu wa kuwasaidia kusoma kwa ada nafuu, ili tuweze kupata idadi kubwa ya watu watakaofundisha masomo hayo.
Katika somo la fizikia alisema hali ni mbaya zaidi kuliko hesabu katika siku za hivi karibuni, huku akitaka utafiti kufanyika ili kupata majibu ya kutosha. Alisema katika somo hilo hata wakufunzi katika vyuo hawatoshi na hata wanafunzi wanaochagua kuwa wabobezi katika somo ni wachache.
Mdau huyo pia alishauri Serikali iboreshe maabara za masomo ya sayansi.
“Kama haiwezekani kujengwa maabara kila shule basi ziwepo maabara zinazotembea, ili shule zilizo karibu ziweze kuzitumia.”
Mdau wa elimu, Godfrey Telli alisema njia pekee inayoweza kukuza ufaulu wa wanafunzi katika masomo hayo, ni kufanya wanafunzi wayapende, yawavutie na wayachukulie muda na walimu watumike katika kuwasaidia kufanya vyema zaidi.
Pia alishauri kuwapo kwa maabara, vitabu na kila kitu ambacho kitamfanya mwanafunzi asome na kuelewa.
Lakini alinyooshea kidole mitaala inayofundishwa shuleni kuwa imepitwa na wakati kwani marekebisho yake yalifanyika zaidi ya miaka 20 na tayari kuna mabadiliko makubwa yamefanyika.
“Wanayofundishwa wanafunzi na uhalisia katika jamii iliyopo hakuna uwiano, wakati mitaala inazalishwa kulikuwa hakuna mitandao ya kijamii, simu za mkononi, kulikuwa na kalamu na karatasi na notebook,” alisema Telli.
“Mitaala inatakiwa iendane na uhalisia wa kawaida, ili mwanafunzi afaulu masomo yake hasa ya sayansi unatakiwa kumsaidia ayapende na ayatumie mara kwa mara shuleni, nyumbani akikaa badala ya kuangalia kitu kinachohusiana na kitu cha kijamii aangalie kitu kinachokuvutia katika mitaala.
Akizungumza na mwananchi mmoja wa walimu ambaye hakutaka kutaja jina alisema umefika wakati sasa kwa serikali kuongeza walimu ili kuwapunguzia mzigo wa ufundishaji.
“Shuleni kwetu mimi ni mwalimu pekee wa fizikia, unaweza kuona mzigo nilionao katika ufundishaji hata ule ufanisi unakuwa si kwa kiwango kinachotakiwa, liangaliwe, maabara pia hakuna ni ngumu kuweka maneno katika sehemu inayohitaji vitendo,” alisema Mwalimu huyo kutoka mkoani Morogoro.