Wamiliki shule wailima barua Necta

Wanafunzi wakifanya mtihani. Picha ya Maktaba

Dar es Salaam. Shirikisho la Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi (Tamongsco) limemuandikia barua Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kuhusu uamuzi wa kuzifungia shule 24 kuwa vituo vya mitihani huku ikitoa mapendekezo matano juu ya kushughulikia tatizo hilo.

Tamongsco iliandika barua hiyo ikiwa ni siku chache tangu wanafunzi 2,194 wa darasa la saba kutoka vituo hivyo waliofutiwa matokeo kufanya mtihani wa marudio.

Akizungumza na Mwananchi jana, Leonard Mao wa Tamongsco alisema waliandika barua hiyo Desemba mwaka jana kwa sababu kilichofanyika kinawaumiza wanafunzi wa madarasa ya chini kwa kuwanyima fursa ya kuendelea na masomo.

“Hatua hii pia itawakatisha tamaa watu na asasi zenye nia ya kuanzisha na kuendesha shule kwa lengo la kuunga mkono jitihada za Serikali kutoa elimu bora kwa Watanzania wote,” alisema Mao.

Alisema pamoja na kitendo hicho cha kuifungia shule kuwa kituo cha mitihani ambacho kitasababisha shule hizo kukosa wanafunzi, pia itaathiri maslahi ya Taifa kwa sababu wanafunzi waliokuwa wakisoma hapo watahamia shule nyingine na kusababisha uhaba wa miundombinu ya utoaji elimu kuendelea kushamiri.

“Hali hii itafubaza azma ya Serikali kuhakikisha miundombinu inakuwa sehemu ya kuimarisha ubora wa elimu,” alisema.

Akizungumzia barua hiyo, Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Athumani Amasi alisema hata kama imeandikwa watakaojibiwa ni Tamongsco.

“Kama wameandika majibu tutawapatia wao si wewe,” alisema Amasi alipozungumza na mwandishi kwa simu huku akieleza kuwa vituo vile 24 vinaendelea kufungiwa.

Wakati hayo yakifanyika, Tamongsco imetoa mapendekezo matano ikiwemo kanuni ya mitihani ya Taifa inayoelekeza shule ambazo zimejitokeza dosari za mitihani kufungiwa kuwa kituo cha mitihani ifutwe

“Pia mfumo wa malalamiko kuhusu dosari za mitihani uimarishwe, ili kuhakikisha taarifa zote zinazohusiana na dosari zipatikane kwa urahisi, kwa kulinda siri na usalama wa mtoaji na pia kuhakikisha wahusika wanapatikana haraka na hatua stahiki kuchukuliwa,” alisema Mao.

Kuhusu ushirikishwaji, Tamongsco wametaka washirikishwe katika hatua za kuboresha mifumo ya usimamizi wa mitihani kupitia Baraza la Taifa la Ushauri wa Elimu (NEAC) ambalo limetajwa na kifungu cha 6 na 7 cha Sheria ya Elimu ya Taifa, 1978.

Wizara iharakishe uteuzi wa Katibu Mkuu wa Elimu kama inavyoelekezwa na kifungu cha 2 na 60(e) cha Sheria ya Elimu ya Taifa, 1978.

Katika usimamizi, Serikali kuangalia namna sekta nyingine zinavyosimamiwa, ili Necta nayo iboreshe huku wakitolea mfano sekta ya usafirishaji ambapo dereva wa gari akifanya kosa huadhibiwa yeye huku gari ikiachwa kuendelea na safari kama kawaida, isipokuwa kasoro inapojitokeza kwenye gari yenyewe.

“Hivyo kama uchunguzi utabaini kwamba wamiliki wa shule wamehusika, basi waadhibiwe wao na si majengo wala wanafunzi walio madarasa ya chini ambao wanakosa sehemu ya kujifunzia,” alisema Mao.