Wanaoombwa rushwa ya ngono kazini watakiwa kupaza sauti

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari wa Tanzania (Tamwa), Dk Rose Reuben (katikati) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumatano Novemba 22, 2023. Picha na Michael Matemanga.

Muktasari:

  • Wadau mbalimbali wameungana kupinga ukatili wa kijinsia ikiwemo rushwa ya ngono wakati dunia ikienda kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili huo kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 10. Maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka.

Dar es Salaam. Katika kuelekea siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia zitakazoanza Novemba 25, 2023, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), kimewataka waathirika wa vitendo vya ngono kwenye vyumba vya habari kupaza sauti.

Tamwa kwa kushirikiana na Mfuko wa Udhamini Wanawake Tanzania (WFT-T), Mtandao wa kupambana na rushwa ya ngono na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, (Takukuru), kwa pamoja wamesema suala la rushwa ya ngono halivumiliki na njia pekee ya kulimaliza ni waathirika  kupaza sauti.

Utafiti uliofanywa kwa udhamini wa WFT-T umebaini kuwapo kwa rushwa ya ngono kwenye vyombo vya habari, huku asilimia 48 ya wanawake wanahabari waliohojiwa ndio wana uwezo wa kusema wazi kuhusu madhila ya rushwa hiyo waliyopita.

Kwa maana hiyo, asilimia 52 ya wanahabari wanawake hawawezi kusema wazi kuhusu rushwa hiyo ambayo inavunja haki za binadamu, utu na kuua vipaji nchini.

Wakizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 22, 2023 jijini Dar es Salaam, wakuu na wawakilishi wa taasisi hizo wamesema kosa la rushwa ya ngono lipo kisheria halipaswi kufumbiwa macho.

Dk Rose Reuben, Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, amesema kupitia utafiti huo uliofanyika mwaka 2021 imebainika wanahabari wengi wameacha kazi kwa kuhofia udhalilishaji wa kijinsia na wanafunzi wa tasnia hiyo walioacha shule kwa kuombwa rushwa ya ngono.

"Imebainika wapo viongozi katika maeneo ya kazi wanaotoa kazi kwa kuomba rushwa ya ngono badala ya kuangalia uwezo, vipaji huku wakitumia nguvu kubwa kuficha ukweli wa uvunjifu wa maadili wanaoufanya.

"Tamwa na WFT tunaiomba Serikali kama ambavyo tayari imeshaanza kulichukulia kwa uzito suala hili, iendelee kuwawajibisha wanaoomba rushwa ya ngono kwa wanafunzi na wafanyakazi kwenye vyumba vya habari," ameongeza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa WFT, Rose Marandu amesema kutokana na utafiti ulofanywa na Tamwa kuwapo kwa rushwa hiyo kumebainika. "Ndio maana tukaamua kutoa fedha kwa ajili ya kutoa elimu kwa jamii ili ielewe rushwa ya ngono inavyojitokeza. Tunaipigia kelele aina hii ya rushwa kwa kuwa inahusisha utu wa mtu kuna watu hadi wantamani kujiua kwa sababu ya rushwa hii," amesema.

Naye Selemani Bishagazi kutoka Mtandao wa kupambana na rushwa ya ngono Tanzania, amesema shida iliyopo kwa waliopitia kadhia hiyo wanaogopa kusema kwa wenza wao kwamba wameombwa rushwa ya ngono.

Bishagazi amesema jambo lingine linaloleta ugumu ni suala la ushahidi ambao kuna ushahidi unaotaka mhusika akutwe chumbani na mtu aliyemdai rushwa hiyo ili akamatwe.

 Amesema kwa upande wa vyombo vya habari inawezekana kuna mtu ana uwezo mzuri wa kuwa mwanahabari, lakini akakosa kazi kwa sababu hajakubali kutoa rushwa ya ngono.

"Nitoe rai kwa Takukuru tutafute mbinu nyingine rahisi ya ushahidi kuliko hii ya kukutwa chumbani kwa kuwa inaleta ugumu," amesema Bishagazi.

Akipigilia msumari suala hilo, Ofisa Uchunguzi Mkuu wa Takukuru mkoa wa Kinondoni, Doroth Mrema amesema rushwa ya ngono imeharamishwa kwenye sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007. Amesema hivyo si tu kwa wanahabari bali kwa watu wote.

"Kupitia kifungu cha 25 kimeharamisha mtu yeyote mwenye mamlaka atakayetumia mamlaka hayo kudai rushwa ya ngono ama upendeleo mwingine wowote ili aweze kumpatia mtu katika masuala ya ajira, upandishwaji wa cheo au kumsaidia mtu apate haki yake," amesema.

Amesema rushwa ya ngono inasumbua watu katika sekta mbalimbali ikiwamo ya elimu, afya, ofisini na majumbani.

"Mapambano dhidi ya rushwa ili yapate matokeo chanya kwanza jamii lazima itambue kuwa kuna tatizo hilo kisha tuchukue tahadhari. Watu watoe taarifa wasikae kimya. Kwa jamii zetu ngono ni suala la aibu ndio maana watu wanaogopa kusema, lakini tunatoa elimu tunaitaka jamii ipaze sauti" amesema.

Amesema madhara ya rushwa ya ngono ni pamoja na magonjwa, watu wasio na vigezo kuajiriwa, kuongezeka watoto wa mitaani waliokataliwa.