Wanasheria watoa maoni tofauti mapendekezo kamati ya Mwakyembe

Muktasari:
- Baadhi ya wanasheria wamekubaliana na mapendekezo yaliyotolewa na kamati iliyoongozwa na Dk Harisson Mwakyembe yakiwamo ya mwanafunzi kupata uzoefu wa mahakamani au kwenye kampuni za uwakili kabla ya kujiunga na Shule ya Sheria Tanzania (LST).
Dar es Salaaam. Baadhi ya wanasheria wamekubaliana na mapendekezo yaliyotolewa na kamati iliyoongozwa na Dk Harisson Mwakyembe yakiwamo ya mwanafunzi kupata uzoefu wa mahakamani au kwenye kampuni za uwakili kabla ya kujiunga na Shule ya Sheria Tanzania (LST).
Itakumbukwa hivi karibuni, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro aliunda kamati ya wajumbe saba kwa lengo la kutafuta chanzo cha kufeli kwa wanafunzi wengi kwenye mitihani ya LST na juzi Dk Mwakyembe alikabidhi ripoti yake.
Hatua hiyo ilikuja baada ya malalamiko na kelele za wanafunzi na wananchi kufuatia hoja iliyoibuliwa na gazeti hili kuhusu idadi kubwa ya waliofeli mitihani ya mwisho ya kumaliza mafunzo hayo yanayowapa sifa ya kuwa mawakili.
Kwa nyakati tofauti, wakizungumza na Mwananchi baada ya ripoti hiyo kuwasilishwa serikalini kwa hatua zaidi, wanasheria waliunga mkono mapendekezo yaliyotolewa na kamati hiyo.
Akizungumzia hilo, Dk Nshala Rugemeleza alisema amekubaliana nayo kwa kiasi kikubwa ingawa hana uhakika kama yatakuwa mwarobaini wa kutibu tatizo bali yatasaidia kuboresha ufundishaji na kuimarisha fani sheria nchini.
“Sasa mpira upo kwa Serikali katika kuyafanyia kazi mapendekezo ya kamati maana imeainisha makosa yanayosababisha wanafunzi kufeli yakiwamo ya kimfumo. Lakini, LST nao wanapaswa wasahihishe mitihani mapema ili wanafunzi wayapate matokeo yao haraka,” alisema Dk Nshala aliyewahi kuwa rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Mmoja wa wanafunzi wa LST ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alikubaliana na mapendekezo ya kamati ya Dk Mwakyembe akisema yamegusa maeneo mengi muhimu kuhusu fani yao na iwapo yatafanyiwa kazi, yatakuwa msaada mkubwa.
Mwanasheria mwingine, Jebla Kambo alisema anakubaliana na mapendekezo ya kamati hasa kuwapo kwa uwiano wa kusoma shahada ya sheria na sifa za kusomea kwani ni muhimu kwamba ndio maana Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimekuwa kikisimamia suala hilo.
“Muhimu kuweka viwango na sifa ili mwisho wa siku kupata wanasheria bora. Wanasheria ni watu muhimu kwenye jamii kama hawana sifa wala viwango wanaweza kulitumbukiza Taifa katika hasara kubwa.”
“Mfano mazingira ya kesi ya ardhi, kama wakili hana sifa anaweza kusababisha mtu kufungwa au kukosa haki yake, muhimu sana mwanasheria awe bora, mwenye akili na maadili ili ufikie viwango vinavyostahilina kukubalika,” alisema Kambole.
Wakili Kambole alisema taaluma ya sheria haikuwekwa kwa ajili ya kila mtu kuisoma bali kwa watu maalumu na itaendelea kuwa hivyo kwa kuwa ni lazima kuwapo mipango mizuri. Kuhusu mapendekezo ya rufaa kwa wanafunzi wasioridhika na matokeo alisema ni mazuri lakini ni vema eneo hilo likaboreshwa.
“Ila hawajafanya kazi kuhusu sifa za walimu wanaofundisha LST na vigezo vyao, hili linapaswa kuzingatiwa kwa umakini hasa kuangalia uwezo wao, uzoefu na nia ya dhati ya kufundisha. Tumewalaumu sana wanafunzi bila kuwaangalia walimu na muda sahihi,” alisema Kambole.
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Wakili Onesmo Ole Ngurumwa alisema hakubaliani na kufufuliwa kwa Baraza la Elimu ya Sheria (CLE) badala yake alishauri LST kujengewa uwezo kusimamia kazi hizo.
“Taifa halina fedha, hapa utahitaji kuunda sekretarieti. Ni bora kazi hii ipewe LST ishirikiane na TCU kusimamia masuala ya sheria. Pia vyuo vinavyotoa shahada viwafundishe wanafunzi masomo ya LST ili wakifika wafanye kwa vitendo zaidi,” alisema.
Mwenyekiti wa Mawakili Vijana kutoka TLS, Edward Heche alisema kamati ilipaswa kuendesha kazi yake kwa uwazi huku akisema tatizo hilo linawagusa mawakili na Watanzania wote kwa ujumla.
“Kamati imejiridhisha vipi kama kampuni za mawakili zinaweza kumudu wanafunzi wote ambao wamemaliza shahada ya kwanza? Pili, hoja hii haina mashiko kwa sababu bado itaondoa dhana ya shule ya sheria kwa vitendo, kwa mfano kunakuwa na wahitimu 600 kwa mwaka, je tuna kampuni za kuwabeba hawa wote kwa mwaka na hii ni asilimia ya chini sana tumechukua. Kwa hiyo pendekezo kama hili halitekelezeki,” alisema Heche.
Alisema kamati imependekeza chuo kipokee maombi ya waliomaliza shahada ya kwanza na kupita katika kampuni za mawakili jambo alilosema ni la kibaguzi.
(Nyongeza na Hadija Jumanne)