‘Wanaume teleza’ waundiwa mkakati Kigoma, wazee wahusishwa

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Emmanuel Maganga amewaomba wazee wanaoishi katika manispaa ya Kigoma Ujiji  kushirikiana na jamii kuwataja ‘wanaume teleza’ ambao hujipaka oil na kuwabaka wanawake kwa maelezo kuwa wanaishi katika nyumba zao

Kigoma. Si jambo geni kusikia habari za wanaume wanaojipaka oil chafu maarufu ‘wanaume teleza’ kisha kuwabaka wanawake mkoani Kigoma.

Jana jioni Ijumaa Mei 24, 2019 mkuu wa Mkoa huo, Emmanuel Maganga amewaomba wazee wanaoishi katika manispaa ya Kigoma Ujiji  kushirikiana na jamii kuwataja wanaume hao kwa maelezo kuwa wanaishi katika nyumba zao.

Alitoa kauli hiyo katika futari aliyoiandaa nyumbani kwake na kuwaalika wakazi wa Kigoma, wakiwemo wazee.

Amebainisha kuwa jamii ikitoa ushirikiano vijana hao watakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na wakikutwa na hatia wataishia gerezani.

Amewataka wakazi wa Kigoma kuacha uoga kwa kuficha taarifa kuhusu unyama unaofanywa na vijana hao.

Diwani wa Mwanga Kusini, Musa Maulidi aliiambia Mwananchi kuwa ikiwa jamii itakuwa tayari kutoa taarifa Polisi tatizo la ‘wanaume teleza’ litakwisha na watu kuishi kwa amani.

Vitendo mbalimbali vinavyofanywa na ‘wanaume teleza’ mkoani humo vimezungumzwa mara kadhaa na Mei 20, 2019 bungeni jijini Dodoma mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo),  Zitto Kabwe alitoa maelezo kuhusu vitendo vinavyofanywa na kundi hilo ikiwa ni pamoja na kubaka, kujeruhi na kuiba.

Zitto alisema shirika lisilo la kiserikali la Tamasha, wamekusanya matukio ya wanaume teleza na kubaini matukio kama 43.

Alichokisema Lugola kuhusu teleza

Akijibu hoja ya Zitto bungeni, Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola alisema ubakaji ni kosa la jinai na linaadhibiwa kisheria na kwamba vitendo hivi vya makosa ya aina hii vimekuwa vikitokea si Kigoma tu hata maeneo mengine na vimekuwa vikidhibitiwa.

“Kwa mkoa wa Kigoma, matukio aliyosema Zitto ni kweli vinadhalilisha na walikuwa wanajikuta mtu ambaye haonekani kwa macho na mwanamama anajikuta sehemu zake za siri amelowa,” amesema Lugola na kuongeza kuwa mwanamke akitaka kumshika mtu huyo analeteza.

“Vitendo hivi vimeendelea kudhibitiwa na nilipopata taarifa kutoka kwa Zitto na mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze. Lakini jambo hilo si kubwa kwa kiasi hicho, kama anavyosema Zitto, tukiangalia taarifa katika vitabu vyetu pale Kigoma, hakuna taarifa zilizoripotiwa mpaka leo,” amesema waziri huyo ambaye pia ni mbunge wa Mwibara (CCM).

Amesema katika kipindi cha mwaka mmoja, hakuna tukio lolote lililohusisha mwanamke kubakwa isipokuwa yapo matukio matatu ya kubakwa yanayohusisha wanawake kujeruhiwa katika nyumba zao.

Waziri Lugola amesema yawezekana katika kujeruhiwa hawakufikia kiwango cha kutenda kosa.

“Kwenye maeneo mbalimbali katika nchi yetu, kuna baadhi ya taasisi au mtu mmoja mmoja, wanakuza mambo na kujenga hofu, niseme bayana, taasisi ambazo zinakwenda kufanya tafiti na kukuza mambo, tumeanza kuziorodhesha na hatua zitaanza kuchukuliwa,” amesema Lugola.

Wakati wote huo, Zitto alikuwa akisimama mara kwa mara kutaka kuzungumza lakini Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga alimzuia akimtaka kusubiri waziri amalize kisha atampa nafasi ya kuzungumza.

“Kama Zitto una taarifa hizo, niko tayari kwenda Kigoma na nitachukua hatua,” amesema Waziri Lugola.