Wanawake 400 kuhamasisha utalii wa ndani Hifadhi ya Nyerere

Kamanda wa Uhifidhi Kanda ya Kusini, Steria Ndaga, akizungumza na waandishi wa habari. Kushoto ni  dereva wa treni ya Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (Tazara),  Judithi Ligenzi.

Muktasari:

 Wakati Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yakifanyika Machi 8 ya kila mwaka, wanawake 400 hapa nchini wanatarajiwa kutembelea Hifadhi ya Taifa Nyerere kuhamasisha utalii wa ndani

Dar es Salaam. Zaidi ya wanawake 400 wanatarajiwa kutembelea Hifadhi ya Taifa Nyerere, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake inayoadhimishwa Machi 8 ya kila mwaka.

Kamanda wa Uhifidhi Kanda ya Kusini, Steria Ndaga amesema safari hiyo itakayofanyika Machi 2, 2024 imeandaliwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) kwa kushirikiana na Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (Tazara).

Akizungumza jana Februari 19, 2024, Kamanda Steria amesema mbali na safari hiyo kulenga wanawake kusheherekea siku yao, pia ni mkakati wa kuhamasisha wanawake na Watanzania kufanya utalii wa ndani.

"Tunatumia haya maadhimisho kuwahamasisha watu hususani wanawake kufanya utalii wa ndani kwa kuwa bado hali si nzuri kwa Watanzania kutembelea vivutuo mbalimbali ya utalii nchini.

"Pia, ni katika kuutangaza utalii wa mikoa ya kusini ambayo kwa muda mrefu watu hawakuwa wakijua kuwa kuna vivutio vya utalii," amesema kamanda huyo.

Kuhusu gharama za safari, Kamanda Steria amesema kila mwanamke atalipia Sh200,000 na atapata huduma zote vikiwamo vyakula na vinywaji, ukiacha usafiri wa kumpeleka na kumrudisha mbugani.

Judithi Ligenzi ambaye atakuwa dereva wa treni ya Tazara siku hiyo, amewahakikishia wanawake watakaojitokeza kufika salama safari yao.

Judithi amesema wakati wa safari hiyo pia watapata wasaa wa kubadilishana mawazo, ikiwamo kuwaeleza kwa kina wale wanaotamani kuwa madereva kama yeye au wenye watoto wa kike wanaotamani kazi hiyo.

"Nitumie nafasi hii kuwaambia wanawake wenzangu hakuna kazi iliyopangwa kwa ajili ya mwanamke, hivyo kama una ndoto za kuwa dereva kama mimi au una mtoto mwenye ndoto hiyo, siku hiyo tutazungumza mengi wapi upite, ili kufikia ndoto zao," amesema dereva huyo.