Wapo wanaozifahamu fursa zilizomo kwenye taka

Wakazi wa  Kirumba jijini Mwanza   wakiokota  taka mbalimbali vilizotupwa kwenye jaa  huku ndege wanaojulikana kwa jina la ‘mabwana afya’ nao wakiwania taka hizo. Picha na Michael Jamson

Muktasari:

Kwa mazoea ya wastaarabu wengi, wazoa taka huonekama kama watu wasiokuwa na akili timamu, walevi au wa hadhi ya chini kimaisha kutokana na aina ya shughuli wanayoifanya pamoja na mavazi wanayovaa.

Wengi huona magari ya taka yakikatiza mitaa tofauti hasa maeneo ya mjini lakini ni wachache wanaofahamu siri iliyopo nyuma ya biashara hiyo.

Kwa mazoea ya wastaarabu wengi, wazoa taka huonekama kama watu wasiokuwa na akili timamu, walevi au wa hadhi ya chini kimaisha kutokana na aina ya shughuli wanayoifanya pamoja na mavazi wanayovaa.

Licha ya mavazi yao, muonekano wa magari wanayotumia pia, ni kitu kingine kinachokatisha tamaa kwani baadhi huwa machafu pengine kuliko uchafu wenyewe huku yakitoa harufu mbaya.

Lakini, ipo siri ambayo wengi hawaijui. Taka hizi, ni chanzo cha fedha halali kwa baadhi ya wajasiriamali walioona fursa na wakawekeza au kujiajiri huko.

Majalala

Gazeti hili limezungumza na baadhi ya wanaojishughulisha nao na kugundua wapo watu wanaoshinda kwenye majalala makubwa wakiokota jaribu mabaki ya vitu mbalimbali vinavyoweza kuwaingizia kipato ya kuendesha maisha yao.

Amina Kizumba ni miongoni mwa wanaotumia fursa hiyo. Mkazi huyu wa Yombo kwa Limboa hukota taka anazozitaka katika dampo la jiji lililopo Pugu Kinyamwezi

“Huwa nakuja kuchambua taka kila asubuhi ili kupata chochote cha kuuza na kulisha familia yangu,” anasema Amina.

Anasema mara nyingi magari yanapokuja kumwaga uchafu katika maeneo hayo huweza kuokota vitu vidogo vidogo vinavyoweza kumuingizia hadi Sh10,000 kwa siku.

Anasema si wakotaji wa majalalani pekee wanaonufaika na taka kutoka majumbani, ofisini, sokoni, viwandani au kwenye maghala ya wafanyabiashara tofauti wanaotozwa fedha kwa ajili ya kuondoa mabaki ya vitu mbalimbali wasivyo na matumizi navyo tena.

“Sisi tunapata hela ndogo ila wanaokuja kumwaga kwa kutumia magari hupata fedha nyingi kwa sababu wao wanachambua kabla ya kuja kuzimwaga huku,” anasema Amina

Baada ya muda mfupi tukiwa jalalani hapo linatokea gari ya kampuni ya Kajenjere lililokuja kumwaga taka hivyo kumashawishi mwandishi kuzungumza na vijana wanne waliokuwamo kwenye gari hilo.

Kariakoo Shimo la Udongo ndiko zilipo ofisi za Kajenjere, kampuni inayofanya usafi katika Kata ya Mchikichini na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ambako mkurugenzi wake, Methew Andrew anazungumza na mwandishi wa makala haya.

Andrew anasema mtazamo uzoaji taka ni sekta inayokua na siku hizi baadhi ya wahitimu wanafanyakazi kwenye kampuni mbalimbali za usafi hivyo kuendesha maisha yao.

Anato mfano kampuni yake, kwamba kati ya watu 40 alionao wawili wana elimu ya chuo, 12 wamehitimu kidato cha nne.

“Kitu wasichojua wengi ni kuwa kutokana na takataka zinazozalishwa maeneo mbalimbali kuna watu hujiingizia kipato cha uhakika. Hii ni biashara isiyohitaji mtaji wala haina hasara,” anasema Andrew.

Anasema kitu muhimu ambacho watu hawakifahamu ni namna ya kuhifadhi tofauti kukidhi matumizi. Anasema kuhanganya taka sehemu moja ndiko kunakowakosesha wengi kipato kwani zinapoteza sifa ya kutumika tena.

Kuongeza thamani ya taka tofauti, Andrew anasema zinatakiwa kutofautishwa kwa kuwekwa kila aina sehemu yake.

“Kuna masoko mengi ya takataka ila wananchi hawayafahamu. Sisi huwa tunatoa elimu kwa watu wanaotuzunguka,” anaeleza.

Gari moja linalobeba kati ya tani 24 hadi 26, anasema vijana wake hujiingizia kati ya Sh150,000 hadi Sh300,000 kwa safari kila safari moja wanayofanya.

Wanachokifanya baada ya kuzikusanya, anasema ni kuzitofautisha kabla ya kuzipeleka kwa wateja wao ambao huzitumia kutengeneza bidhaa za aina tofauti.

Anasema kila taka hutumika kurejereza kitu kipya hivyo kinachohitajika ni usafi tu kuifanya ikidhi kutumika tena kwa manufaa yaliyokusudiwa.

“Maboksi yanatumika kutengeneza trei za mayai, karatasi nyeupe hutumika kutengeneza karatasi za chooni (tissue-paper) wakati vyuma mbalimbali hutengeneza nondo na mabaki ya vyakula, matunda na mbogamboga hutumika kutengeneza mbolea,” anasema.

Kwa kutambua tofauti hiyo, anasema wanapokusanya taka na kuzimwaga kwenye gari baadhi ya vijana huzitenganisha ili kutambua zipi zinastahili kupelekwa wapi na zipi ziende wapi.

Anasema hakuna taka ambayo haiwezi kununulika na kufichua kuwa endapo watu watatambua hili itasaidia kupunguza kuzagaa kwa takataka hata kiasi kinachopelekwa jalalani kwani watakuwa wanajiingizia kipato bila kutumia nguvu kubwa.

Fursa

Andrew anasema mwanzoni hata yeye hakuwa anajua matumizi mbadala ya takataka wanazokusanya lakini anashangaa kila wanapozimwaga baadhi ya watu walikuwa wakikizikimbilia na kuanza kuzichambua.

Hamad Aboubakar, ofisa afya wa Kampuni ya Kajenjere anasema si watu pekee, hata baadhi ya magari yalikuwa yakiingia dampo kubeba baadhi ya taka na kuzirudisha mji kuziuza ingawa hairuhusiwi kuurudisha uchafu mjini.

Kutokana na uzoefu huo, anasema walijiuliza kinawafanya watu hao wazirudishe mjini huku wengine wakishinda huko ama wakifukuafukua au wakisubiri gari lije kuzimwaga kisha wazichambue, waliamua kufuatilia na kugundua utajiri uliopo.

“Tunapoenda kuuza mazaga (taka zinazoweza kutengeneza kitu kipya) kila mtu anaweza kupata Sh50,000 hadi Sh60,000 kwa siku baada ya kugawana kwa safari moja tu,” anasema Aboubakar ambaye awali alikuwa mzoa taka mtaani.

Anasema fedha hizo humsaidia kuendesha maisha yake hata kusahau ualimu wa shule za msingi aliosomea na kutofanikiwa kupata ajira.

Anasema baada ya kuhangaika kutafuta ajira wa muda mrefu bila mafanikio alijiunga katika uzoaji taka akiwa hafahamu kama ataweza kutengeneza fedha za kutosha kwa mwezi tofauti na mshahara ambao angekuwa anapokea kila mwisho wa mwezi endapo angefanikiwa kuajiriwa.

“Kwa mwezi naweza kutunza mpaka Sh600,000 kwa sababu situmii Sh50,000 zote nazopata kwa siku,” anasema Aboubakar.

Ajira

Msimamizi wa kampuni hiyo, Hassan Buterabajuma anasema kwa kufahamu faida za taka, wanajitahidi kutoa elimu kwa wabanchi ili wanufaike nazo.

Kufanikisha hilo, anasema huwa wanakuwa makini kuhakikisha vijana wanaowaajiri ni makini wenye wadhamini na wanaotambulika kwenye ofisi za Serikali za mitaa ili kufuta picha kwamba kazi hiyo hufanywa na mateja au wavuta bangi.

“Lazima wakikidhi vigezo. Hatutaki walevi wa pombe au wavuta bangi kwa sababu watumiaji wa vilevi hivyo hutoa lugha zisizofaa kwa wateja,” anasema Buterabajuma.

Licha ya haiba mbele ya jamii, Aboubakar ambaye ni bwana afya wa kampuni hiyo anasema kujali afya binafsi. Anasema msisitizo uliopo ni watumishi kuvaa vifaa vya kuzuia maambukizi wakati wote awapo kazini.

“Kila asubuhi ni lazima tufanye ukaguzi kwa watu wote kuhakikisha kila mtu amevaa buti maalumu, kitu cha kuwakinga na vumbi, gloves, kofia na kiakisi mwanga,” anasema Aboubakar.

Wananchi

Elimu juu ya faida zinazoweza kupatikana kwenye taka bado ni changamoto kwa wananchi ambao wengi bado wana mtazamo hasi.

Mmoja wa wananchi jijini Dar es Salaam, Abuu Mkalatu anasema ili mtu aweze kufanyakazi ya kuzoa taka lazima awe akili zisizo za kawaida na mzima atakayefanya hivyo basi ndani ya muda mfupi lazima ataonekana kama aliyechanganyikiwa.

“Waangalie vizuri watu wanaopita kwenye magari ya taka, tuongee tu ukweli. Hata hiyo faida wanayoisema ni ngumu kuamini. Hata kama zinaweza kuzalisha vitu vingine uhifadhi wake ni wa muda mrefu na kusema kila taka ikae sehemu yake itakua ngumu kwani utahitaji vyombo vingi kuvitunza. Badala ya kuhifadhi tutakuwa tunasambaza taka,” anasema Mkalatu.

Kutokana na kuzagaa kwa taka zinazochafua mazingira, Halmashauri ya Ilala inatumia kampuni saba kuhakikisha usafi unadumishwa.

Ofisa habari wa manispaa hiyo, Tabu Shaibu anasema kampuni hufanya usafi katikati ya mji ila pembezoni mwa mji wanatumia vikundi mbalimbali.

“Kampuni zina uwezo mkubwa na vifaa vya kisasa kufanya usafi na hali ni tofauti na zamani. Ukiangalia Soko la Kariakoo usafi unaofanyika hivi sasa unaridhisha,” anasema Tabu

Hata eneo la katikati ya jiji, anasema mandhari ni nzuri kwani bustani zinatunzwa kwa ustadi kiasi cha kuvutia macho ya watu.

Akikiri elimu ya utumiaji wa taka kama chanzo cha mapato kutowafikia wengi, anasema ni jambo linalosababisha kuendelea kuwepo kwa utupaji hovyo wa mabaki ya vitu mbalimbali.

“Kama mtu akitambua fursa ya chupa ya plastiki, mfuko au boksi akahifadhi nyumbani, zikawa na zikawa na ujazo mkubwa unaoweza kumuingizia kipato ni ngumu kukuta zikitupwa hovyo. Elimu bado haijafika ila tunajitahidi kuifikisha,” anasema Tabu.