‘Watuhumiwa ripoti ya CAG watajwe’

Dar/mikoani. Moto uliowashwa na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), unaendelea kusambaa nchini, safari hii wananchi mbalimbali wamecharuka wakitaka majina ya wanaotajwa yawekwe hadharani.

Wakizungumza na gazeti hili jana, wananchi katika mikoa mbalimbali wamelipongeza Bunge kwa maazimio ya kutaka waliotajwa washughulikiwe, lakini hawafurahishwi na majina yao kufanywa siri.

Jumamosi iliyopita, Bunge lilipitisha maazimio ya kamati tatu za Bunge za hesabu (PAC), Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) na Serikali za Mitaa (LAAC), kuhusu ripoti ya CAG kwa mwaka 2021/2022, likitaka wote waliotajwa kuhusika na wizi na ubadhirufu wa fedha za umma, wajitafakari wenyewe au washughulikiwe.

Baadhi ya wabunge waliochangia walienda mbali na kupendekeza mawaziri, makatibu wakuu na watendaji wakuu wa taasisi za Serikali na mashirika ya umma waliotajwa wajitafakari kabla mamlaka ya uteuzi haijachukua hatua dhidi yao.

Maazimio na mapendekezo hayo ndio yaliyowaibua wananchi katika mikoa mbalimbali, baadhi wakisema Bunge ni kama ‘limewauzia mbuzi kwenye gunia’.
Kwa mujibu wa wananchi hao, Bunge limetimiza wajibu wake wa kikatiba chini ya ibara ya 63(2), ambayo inalipa mamlaka ya kuisimamia na kuishauri Serikali, hivyo kilichobaki ni mhimili wa Serikali kuchukua hatua stahiki.

Mkazi wa jijini Arusha, Getrude Kaaya alitaka waliohusika kuchukuliwa hatua, kwani haiwezekani kila mwaka ripoti ya CAG kuibuke wizi na hakuna hatua ambazo zinachukuliwa huku mwananchi aliyejitambulisha kwa jina la Ally akisema maazimio ni mazuri ila wanaopaswa kuwajibika lazima wajulikane.

Huko Moshi, mkoani Kilimanjaro Renalda Evance mkazi wa Kiborloni alisema hajaridhishwa na mijadala aliyoifuatilia bungeni, akisema Bunge halikupaswa kuazimia kuwa waliotajwa wajitafakari, bali kuwawajibisha.

“Kwanza ni kama tumeuziwa mbuzi kwenye gunia, kwa sababu katika azimio lao wala hawajatutajia hao mawaziri, makatibu wakuu au wakuu wa mashirika waliofanya hayo madudu ni kina nani. Tunataka tuwafahamu,” alisema Evance.

Mkazi wa Bomang’ombe wilayani Hai, Agnes Urio alitaka waliotajwa na CAG kufisadi fedha za umma wasinyongwe kama baadhi ya wabunge walivyopendekeza, bali warejeshe fedha hizo na kushitakiwa.

Sebastian Swai ni mkazi wa Manzese Dar es Salaam, alisema hatua hiyo ya Bunge kutoa maazimio ni muhimu lakini haamini juu ya utekelezwaji wake kwa kuwa kumekuwepo ripoti lukuki za CAG lakini wahusika hawakuwahi kuwajibishwa.

"Mimi naona kama siasa na maigizo tu kwa sababu si CAG huyu tu aliyeleta taarifa kama hiyo, mambo yamekuwa oya oya (yasiyoeleweka) bungeni. Kelele zinazopigwa na wabunge hazina nguvu kwa kuwa wengi ni chama kimoja,” alisema

Dereva Bodaboda mkoani Mbeya, Joseph Aloyce alisema wahusika watajwe na kuchukuliwa hatua haraka.

“Kimsingi, tunaomba waliohusika watajwe kama kwenye halmashauri, taasisi za Serikali zitajwe hadharani kwani watanzania wamechoshwa na ubadhirifu wa fedha za jasho la mlipa kodi mnyonge katika taifa la Tanzania,” alisema Aloyce.

Furaha Onesmo ambaye ni mkazi wa Mission, mkoani Geita alisema kinachofanywa na wabunge, ni jambo sahihi kwa kuwa wametumwa na wananchi lakini yanayojadiliwa hayatakuwa na maana kama hakutakuwa na utekelezaji wa maazimio hayo.

Kwa upande wake, Joseph Amos dereva bodaboda kijiwe cha Bomani, alidai ripoti za CAG zimekuwa zikijadiliwa bungeni lakini ni kama Serikali haina meno ya kuwashughulikia kishera wanaodaiwa kufunja fedha za umma.

Mkazi wa Kibirizi, mkoani Kigoma, Pascal Noah alisema wananchi wanawategemea wabunge kama chombo ambapo kinawakilisha watu wengi nyuma yake, hivyo kuwawajibisha watu hao itasaidia wananchi wanyonge. Ripoti kama hiyo Mei mwaka 2012 ilipojadiliwa bungeni, ulitokea mtikisiko mkubwa uliowang’oa mawaziri sita na manaibu wawili.

Waliong’olewa ni Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara), Omary Nundu (Uchukuzi), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Mustafa Mkulo (Fedha) na William Ngeleja (Nishati na Madini) na manaibu waziri wawili; Athumani Mfutakamba (Uchukuzi) na Dk Lucy Nkya (Afya).


Imeandikwa na Daniel Mjema, na Fina Lyimo, Mussa Juma, Hawa Mathias, Rehema Matowo, , Happines Tesha na Juma Isihaka