Wawili wakamatwa wakisafirisha wahamiaji haramu 20

Muktasari:
- Madereva wawili wa malori yaliyokuwa yakitoka Dar es Salaam kwenda DRC Congo wamekamatwa mkoani Songwe baada ya kukutwa wakiwasafirisha wahamiaji haramu 20 kutoka Somalia na Ethiopia.
Songwe. Madereva wawili wa malori yaliyokuwa yakitoka Dar es Salaam kwenda DRC Congo wamekamatwa mkoani Songwe baada ya kukutwa wakiwasafirisha wahamiaji haramu 20 kutoka Somalia na Ethiopia.
Afisa Uhamiaji mkoani humo, Creti Mumwi amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Jumapili Machi 27, 2022 katika operasheni maalumu eneo la Nanyala wilayani Mbozi.
Amesema Daniel Mwakasege amekamatwa akiwa anawasafirisha wahamiaji 5, na Peter Edward wahamiaji 10 lakini dereva ambaye jina lake halijafahamika amekimbia baada ya kukutwa anasafirisha wahamiaji 5.
Amesema Malori hayo ni Mali ya Kampuni ya AK Transport ambayo yamebeba Salfer kuelekea Congo.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari mmoja wa madereva hao, Peter Edward amedai wahamiaji hao waliwapakia eneo la Chalinze mkoani Pwani wakidai wanaenda Tunduma, hawakujua kama ni wahamiaji haramu.