Waziri asimulia alivyosaidiwa kusomeshwa na Sokoine

Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Longido, Mkoa wa Arusha.

Muktasari:

 Moja kati ya changamoto kubwa iliyokuwa ikiwakabili jamii ya wafugaji wa Kimasai ni watoto kutokwenda shule na wengine kutopenda kusoma

Arusha. “Siku zote nimekuwa nikiamini huyu baba mzalendo wa kweli amekuwa na dhamana kubwa katika maisha yangu, naona Mungu alimtuma ninyanyuke katika familia yetu ya watoto saba,  hakuna mwingine aliyeenda shule zaidi yangu.”

Ni nadra kwa kiongozi ambaye amepata mafanikio ya kielimu, kiuchumi na kisiasa kuelezea mapito aliyopitia, lakini si kwa Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa ambaye anasema bila Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Sokoine asingefika alipo.

Dk Kiruswa ambaye pia ni mbunge wa Londigo, anasema bila Sokoine wala asingeona darasa lakini sasa ana elimu kutoka chuo kikuu.

Moja kati ya changamoto kubwa iliyokuwa ikiwakabili jamii ya wafugaji wa Kimasai ni watoto kutokwenda shule na wengine kutopenda kusoma badala yake baadhi ya wazazi na watoto wa jamii hiyo kupendelea zaidi shughuli ya kuchunga ng’ombe.

Hivi karibuni,  Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha, Isack Amani akizungumza katika kumbukumbu ya miaka 40 ya kifo cha Sokoine alisema kiongozi huyo kwa namna ya pekee alikuwa chachu ya kusaidia jamii ya Kimasai kuwa na mwamko wa elimu.

Ni kutokana na waandishi wa vitabu kutambua changamoto hiyo, mwandishi Henry R. ole Kulet aliandika kitabu ‘Is it possible?’ akielezea kuwa mtoto wa Kimasai anaweza kupata elimu na bado akawa morani, akibeba mkuki na kuwa shujaa wa Kimasai.

Simulizi ya mwandishi wa kitabu hicho, inaakisi maisha ya Dk Kiruswa anayetokea jamii ya wafugaji akielezea namna watendaji wa Serikali walipofika katika familia yao na kueleza kuwa inahitaji mtoto mmoja tu, kati ya saba apelekwe shule.

“Kura ya nani aende shule kwenye familia ikaniangukia mimi, wale waliokuwa wameachwa walifurahi maana hakuna aliyekuwa anataka kwenda shule. Hata mimi nililia kwa sababu sikujua umuhimu wa kwenda kusoma,” anasema Dk Kiruswa.

Aprili 12, mwaka huu kulifanyika kumbukumbu ya miaka 40 tangu kifo cha Sokoine,  yalizungumzwa mambo mengi ikiwamo mchango wake wa kusaidia jamii ya kifugaji ipate elimu ya darasani.

Dk Kiruswa aliyezaliwa Februari 2, 1963 katika Kijiji cha Ngosuak, Kata ya Engarenaibor wilayani Longido, anasema jamii ya Kimasai ilikuwa inaachwa nyuma na haikuthamini elimu na walikuwa wako tayari kuficha watoto wao ili wasiende shule.

Dk Kiruswa anasema jamii ya wafugaji wa Kimasai walikuwa wakiamini elimu itawatoa kwenye mstari wa mila, desturi na tamaduni zao za wafugaji, dhana iliyokuwa imejengeka sio kwa wafugaji tu wa Longido, karibu nchi nzima.


Kwa nini ni Edward Sokoine?

Dk Kiruswa anasema bila hayati Sokoine pengine kizazi chao wasingewahi kwenda shule na kupitia operesheni iliyofanyika kuwasaka watoto wa jamii ya kifugaji ya Kimasai wapelekwe shule, ndio iliyosababisha na yeye kuwa miongoni mwa walioenda shule.

Naibu waziri huyo wa madini anasema kupitia utaratibu huo wa kuchukua mtoto mmoja katika kila familia, walipofika kwenye familia yao ambayo yeye ni mtoto wa sita kati ya saba, kura ya kupelekwa shule ilimuangukia yeye.

Dk Kiruswa anasema wenzake sita walioachwa walifurahi kwa kuwa hakuna aliyekuwa anataka kwenda shule na kuwa hata yeye alilia kwa kuwa, hakujua umuhimu wa elimu lakini wazazi wake walimfariji na kumsihi kwenda shule.

“Lakini kulikuwa na suala la umri linaangaliwa. Kaka zangu watano walishavuka ule umri nilikuwa na dada wawili mmoja alivuka ule umri na mdogo alikuwa hajafikia umri huo, ikaonekana mimi ndiyo natakiwa kwenda shule,”anasema Dk Kiruswa.

“Nakumbuka nilikuwa na miaka tisa na nilikuwa na uwezo wa kwenda kuchunga mifugo porini mwenyewe,”anaeleza Naibu waziri akisimulia safari ya maisha yake.

“Kwa jinsi Sokoine alivyokuwa anapenda wananchi wake na alivyokuwa anajua mila na desturi za jamii ya Kimasai kuwa ina mgawanyo wa majukumu na majukumu ya watoto wa kiume ni kuchunga mifugo, alitengeneza mazingira ya sisi kwenda shule.


Simulizi alivyoanza shule

Dk Kiruswa anasema alipoanza Shule ya Msingi Longido mwaka huo, aliugua malaria iliyosababisha kurudishwa nyumbani na kukaa kwa muda kabla ya kurejea miaka kadhaa baadaye.

Anasema  baada ya kupona  alisoma katika Shule ya Msingi Engarenaibor.

“Ile shule sisi ndiyo tulikuwa waanzishili na nikiwa pale nilikuwa kaka mkuu hadi nilipomaliza darasa la saba. Nakumbuka nikiwa darasa la tano  Sokoine akiwa Waziri Mkuu alikuja  shule kwenye ziara, nikawa na heshima ya kumvalisha skafu maana nilikuwa kamanda wa kikundi cha chipukizi, nikampokea mzee,” anasema Dk Kiruswa.

“Lakini haikuishia hapo nilipomaliza kidato cha nne wakati nasubiri matokeo na kwenda kidato cha tano, nilikuwa nimeshafikisha umri wa kwenda jandoni, nikasuka nywele za Kimasai, nikaingia kwenye mila na desturi kama mtu ambaye hajawahi kwenda shule.”

Anasema katika kipindi hicho, Mwenge wa Uhuru ukafika kijijini kwao huku majina ya waliochaguliwa akiwamo yeye kujiunga na kidato cha tano yakiwa yametoka.

“Wazazi wangu wakataka kuniombea lifti kwenye gari lake (Sokoine) wanipeleke shule lakini nilikuwa nimesuka nywele, akasema huyu kijana anyolewe nywele na kesho nipelekwe shule na apate taarifa za mimi kwenda shule,”anasema Dk Kiruswa.

“Na kweli nikanyolewa nikaenda shule, nakumbuka mwaka 1984 kabla ya ile ajali alipita shuleni na nilionana naye.”

Sokoine alifariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea Aprili 12, 1984 eneo la Dakawa Morogoro wakati akirejea kutoka Dodoma.

Kwa nini anaamini ni mzalendo?

Katika mahojiano hayo maalumu na Mwananchi Digital, Naibu waziri huyo anasema kwa jinsi ambavyo Sokoine aliwapenda Watanzania wapate elimu, anaamini alikuwa mzalendo aliyetukuka.

“Katika hayo mazingira nimekuwa nikiamini kwamba huyu baba mzalendo wa kweli aliyependa Watanzania waendelee, amekuwa na dhamana kubwa katika maisha yangu.

 “Yaani naona yeye ndiyo Mungu alimtuma ili mimi ninyanyuke katika ile familia ya watoto saba, niliendelea kusoma hadi hapa nilipofika naamini bila yeye nisingekuwa hapa.”

Dk Kiruswa alifundisha vyuo vikuu kadhaa kikiwamo Chuo Kikuu cha Regent Marekani alikopata shahada zake za uzamili na uzamivu kabla ya Chuo Kikuu cha Daystar nchini Kenya alikopata shahada yake katika maendeleo ya jamii na usimamizi wa biashara na kufundisha Kituo cha Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa (Ms TCDC) Arusha.

Pia, alifanya utafiti baada ya udaktari kuhusu mabadiliko ya matumizi ya ardhi na maisha katika Afrika Mashariki kupitia Chuo Kikuu cha London (UCL).

“Miaka 40 imepita hatujamsahau na wala hatutakaa tumsahau tutaendelea kumuenzi maana yeye ndiye alifungua pazia la jamii ya wamasai kuona shule,”anasema Dk Kiruswa.

Anasema katika kumuenzi Sokoine, ameanzisha shule wilayani Longido na anahamasisha jamii kuchangia kwa hali na mali uanzishwaji wa shule shikizi na za msingi katika vijiji ambavyo havikuwa na shule na kuwa mwamko wa elimu umekua zaidi.

“Mimi mwenyewe nimeanzisha shule ya msingi ya mfano na nimehamasisha jamii kuchangia kwa hali na mali uanzishwaji wa shule shikizi,”amesema Dk Kiruswa.