Zingatia haya wakati wa hedhi

Zingatia haya wakati wa hedhi

Mei 28 ya kila mwaka ni Siku ya Hedhi Duniani ambayo imeadhimishwa mwezi uliopita.

Wakati wa hedhi mwili wa mwanamke huambatana na matatizo ya kimwili na kisaikolojia, ndiyo maana kipindi hiki baadhi ya wanawake hupata maumivu makali kiasi cha kushindwa kufanya majukumu ya kila siku, huku wakipata hisia hasi ikiwamo hasira, kukosa raha na huzuni.

Pia, wanawake wenye kifafa au kipandauso (migraine) yaani maumivu makali ya kichwa, ni kawaida kipindi cha hedhi matatizo haya kulipuka zaidi.

Viashiria na dalili zinazojitokeza wakati wa siku za hedhi (periods) zinaweza zikamsababishia mwanamke kutoweza kufanya shughuli zake za kila siku, ikiwamo nyumbani, darasani, viwandani na maofisini.

Ni vizuri mwanamke kuzingatia yafuatayo ili kuufanya mwili wake kuwa msafi, kufifisha maumivu ya chini ya tumbo na vile vile kudhibiti damu ya hedhi inayotoka.

Wanawake wengi huwa na kawaida ya kukimbilia dawa za maumivu wanapokuwa kipindi hiki na kuzitumia kiholela bila hata ya kuandikiwa na daktari.

Wengine hukimbilia pedi za mtaani zisizoeleweka baada tu ya kuona tangazo mitandaoni au mtaani kuwa pedi hizo zina dawa za mitishamba ndani yake ambayo hupunguza maumivu na wingi wa damu ya hedhi.

Ieleweke kuwa dalili za kabla ya hedhi hazizuiliki, lakini yapo mambo ambayo yakifanywa na mwanamke aliye hedhini humsaidia kufifisha makali ya dalili mbaya.

Mwanamke atapaswa kutumia taulo ya kike, yaani pedi au vitambaa maalumu visafi na salama kwa ajili ya kumkinga asichafuke.

Taulo ya kike ndiyo hutumiwa na wanawake wengi wa kisasa kwasababu ya ubora na ufanisi wake.

Huhitajika kubadilishwa kila baada ya saa 4 hadi 8 na zilizotumika zihifadhiwe katika vyombo maalumu na kuchomwa.

Itahitajika kuendelea kufanya shughuli za kila siku, ikiwamo kazi za ndani na za kiuchumi pamoja na kufanya mazoezi mepesi kama kutembea, kuruka kamba, kufanya yoga, kucheza mziki na kusingwa (massage).

Ulaji mlo kamili unaozingatia kanuni za afya, epuka unywaji wa pombe, vitu vyenye caffeine ikiwamo kahawa, epuka mlo wenye chumvi na sukari nyingi.

Kujiepusha na mifarakano ya kimaisha inayoweza kuleta msongo wa mawazo, kupumzika na kulala saa 6-8 kwa usiku mmoja.

Kutumia taulo ya kike yenye uvugu vugu ili kukupa utulivu, kutumia mpira maalumu ulio kama chupa bapa ambayo huwa na maji moto ili kukanda chini ya tumbo na pia kulalia tumbo juu ya mto laini.

Jifunze kwa wengine mbinu zinazowasaidia kuleta utulivu wakati wa hedhi.

Dawa za maumivu zinaweza kutumika kabla na baada ya hedhi kwa ajili ya kupunguza maumivu ya chini ya tumbo, mgongo, kichwa na kiuno, ila ni vizuri kutumia dawa baada ya kushauriwa na daktari.

Endapo maumivu yatakuwa makali yasiyovumilika, homa kali, kutoka hedhi zaidi ya siku 5-7, nyepesi inayolowanisha pedi chapa chapa au kubadili taulo ya kike zaidi ya mara nne mwone daktari kwa ushauri zaidi.

Usichoke kujitafutia elimu ya afya ya uzazi ili kujenga ufahamu mkubwa zaidi.