Ziwa Tanganyika lajaa maji, watu 540 wakosa makazi

Sumbawanga. Jumla ya Watu 540 wamelazimika kuzikimbia nyumba zao mkoani Rukwa baada ya Ziwa Tanganyika kujaa maji ambayo yamezingira nyumba hizo.

Maji hayo yameathiri nyumba 108 katika vijiji viwili vya Kirando kilichopo wilayani Nkasi na Kipwa kilichopo wilayani Kalambo mkoani hapa.

Katika siku za karibuni mvua zimekuwa zikinyesha kwa wingi takriban kila siku mkoani Rukwa na kusababisha Ziwa Tanganyika kujaa maji.

Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Julieth Binyura alisema jana kuwa mafuriko kama hayo yalikikumba kijiji cha Kipwa miaka 23 iliyopita wakati wa mvua za El Nino.

“Nyumba 90 za kijiji cha Kipwa zimefurika maji baada ya Ziwa Tanganyika kujaa maji na kufika yalipokuwa awali, familia za watu 400 hawana makazi, pia wamepoteza mali mbalimbali ikiwemo mifugo yao.”

“Taasisi mbili za umma ambazo majengo yake hayakuathirika ni shule ya msingi na zahanati,” alisema.

Akifafanua zaidi Binyura alisema baadhi ya watu wamehifadhiwa katika vyumba vya madarasa ya shule ya msingi wakati wengine wamekimbilia kwenye maeneo ya miinuko.

Alisema hakuna kifo chochote kilichoripotiwa na hata hasara halisi iliyosababishwa na mafuriko hayo haijafahamika huku kamati ya maafa ya wilaya ikiendelea kufanya tathmini.

Mbali na makazi ya watu, mafuriko hayo pia yamelikumba soko la kisasa la samaki lililopo kata ya Kasanga wilayani Kalambo ambalo pia limefurika maji na kusababisha shughuli katika soko hilo kusimama.

Mmoja wa waathirika wa mafuriko hayo alisema wanaiomba Serikali iwapatie misaada ya hali na mali ikiwemo makazi ya muda.

“Tumepoteza kila kitu tulichokuwa tukimiliki mashamba, nyumba, vyakula, nyumba za biashara, mifugo, nguo, mitumbwi na zana zote za uvuvi, hakika tumekuwa mafukara tunaiomba Serikali itupe msaada wa hali na mali,’’ alisema Peter Simtowe mkazi wa kijiji cha Kipwa.

Huko, wilayani Nkasi katika kata Kirando, diwani wa kata hiyo, Kakuli Seba amenukuliwa akisema kwamba maji ya Ziwa Tanganyika yamefika maeneo yalimokuwa miaka 30 iliyopita na kusababisha mafuriko.

Seba pia alisema kwamba majengo ya kituo cha mafuta, Hoteli ya Nkondwe Beach, mwalo wa samaki, maeneo yote hayo nayo yamefurika maji.

“Hoteli ya Nkondwe Beach imefurika maji na imelazimika kufungwa, pia biashara ya samaki imekuwa ngumu baada ya mwalo wa samaki kufurika maji,’’ alisema Diwani Seba.

Baadhi ya wavuvi wa samaki wakizungumzia mafuriko hayo walisema kwamba yamesababisha biashara yao kuwa ngumu.

“Hatuwezi kufika mwaloni, maji kutoka Ziwa Tanganyika yamefurika hapo hakuna tena biashara ya samaki,” alisema Godwin Mwanisawa ambaye ni mvuvi wa samaki.