1,429 wagundulika kuwa na mtoto wa jicho, wafanyiwa upasuaji

Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mbeya, Agrey Mwaijande akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusiana na Ujio wa madaktari bingwa wa macho. Picha na Hawa Mathias
Muktasari:
- Mratibu wa huduma macho Hosptali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya, Dk Fariji Killewe amesema leo Ijumaa Julai 21 ,2023 wakati akitoa taarifa ya ujio wa madaktari bingwa wa macho kutoka Ujerumani kuweka kambi ya kutoa huduma za vipimo ikiwepo upasuaji kuanzia Agosti 22 mpaka 28 mwaka huu.
Mbeya. Kati ya watu 2,399 waliopimwa tatizo la macho watu 1,429 wamegundulika kuwa na mtoto wa jicho na kufanyiwa upasuaji mdogo kwa kipindi cha mwaka jana mkoani Mbeya.
Mratibu wa huduma macho Hosptali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya, Dk Fariji Killewa amesema hayo leo Ijumaa Julai 21,2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na ujio wa madaktari bingwa wa macho kutoka nchini Ujerumani ambao wataweka kambi ya wiki moja ya kutoa huduma hususani kwa wazee.
Amesema kuwa ujio wa madaktari bingwa ni ufadhili wa Naibu Waziri wa Maji, na Mbunge viti maalum Mkoa wa Mbeya ,Mhandisi Maryprisca Mahundi.
“Tunatarajia kuwapokea madaktari hao kutoka nchini Ujerumani mapema mwezi ujao ambapo wataanza kutoa huduma bure kuanzia Agosti 22 mpaka 28 katika Hosptali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya eneo la Forest jijini hapa,” amesema.
Amesema kuwa lengo la ufadhili huo ni kuwezesha upatikanaji wa huduma za matibabu ya macho na upasuaji bure mara baada ya kubaini kuwepo kwa tatizo kubwa kwa jamii hususani wanaume walio chini ya miaka 55.
“Tuna kila sababu ya kumpongeza na kumshukuru Naibu Waziri wa Maji ,Mhandisi ,Maryprisca Mahusndi kwa kuguswa kusaidia jamii kwani kundi kubwa wamekuwa wakishindwa kufika hosptali kupata huduma kutokana na ukosefu wa kipato,” amesema.
Dk Killewa amesema kuwa kwa Mkoa wa Mbeya kuna changamoto kubwa sana tatizo la mtoto wa jicho hivyo ujio wa madaktari bingwa utakuwa mkombozi kwa wazee ambao wamejikuta kupata upofu kutokana na ukosefu wa kipato.
Aidha ameomba vyombo vya habari kupaza sauti kuelimisha jamii kuhusiana na ujio wa huduma hizo bure ambazo zitaweza kuokoa maisha ya Watanzania wengi huku wakitarajia kupokea madaktari bingwa watatu ambao watashirikiana na wenyeji kutoa huduma.
Kwa upande wake Ofisa Uhusiano wa Hosptali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya, Agrey Mwaijande amemshukuru Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi, Maryprisca Mahundi kwa kuunga mkono juhudi za Serikali kuboresha huduma za kitabibu hususani kwa wazee.
Amesema upatikanaji wa huduma za uchunguzi wa macho bila malipo utawezesha idadi kubwa ya watu walikosa matibabu kutokana na ukosefu wa fedha kupata huduma na kurejea katika hali ya kawaida.
“Ujio wa madaktari bingwa utakuwa chachu kwa madaktari wa hospitali hiyo, kupata uzoefu kutoka kwa wataalam wa kimataifa na kuongeza uwezo wa ndani kugundua matatizo ya macho na kutoa matibabu kwa ufanisi zaidi,” amesema.
Katibu wa Mbunge, Lucia Raphael amesema kiongozi huyo amewiwa kuleta madaktari bingwa wa macho kutokana na Mkoa wa Mbeya kuwa miongoni mwa mikoa iliyo na changamoto ya tatizo la macho kwa kiwango kikubwa.
“Hii sio mara yake ya kwanza kugusa jamii ikumbukwe mwaka jana alileta madaktari ambao waliweka kambi ya matibabu ya festula kwa wakinamama zoezi ambalo lilizaa matunda,” amesema.
Mkazi wa Forest Jijini Mbeya, Joshua Sanga amesema kuwa uwepo wa matibabu ya mtoto wa jicho bure itasaidia kundi kubwa la wazee kurejea katika hali nzuri kiafya kutokana na wengi wao kukosa matibabu kwa sababu ya ukata wa fedha.