10 wapoteza maisha kwa ajali wilayani Siha

Muktasari:
- Watu 10 wamefariki dunia baada ya gari aina ya Kirikuu kugongana uso kwa uso na gari la polisi katika eneo la Dachikona, katika Kijiji cha Wiri, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro.
Siha. Watu 10 wamefariki dunia baada ya gari aina ya Kirikuu kugongana uso kwa uso na gari la polisi katika eneo la Dachikona, katika Kijiji cha Wiri, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Christopher Timbuka amethibitisha kutokea kwa ajili hiyo ambapo amesema imetokea leo, Agosti 18 majira ya mchana na miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Siha mkoani humo.
"Idadi ya waliopoteza maisha imeongezeka na kufukia watu 10 na amepatikana majeruhi mmoja ambaye hali yake inaendelea vizuri," amesema.

DC Timbuka amesema miongoni mwa waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni dereva aliyekuwa akiendesha gari la polisi ambaye amefariki papo hapo.
Amesema 9 waliopoteza maisha walikuwa wamepanda Kirikuu ikiwa imebeba mizigo wakiwa wanaenda mnadani eneo la Ngarenairobi ambapo tairi la mbele la gari hilo lilipasuka na kupelekea kupoteza mwelekeo na kwenda kugongana na gari la polisi lililokuwa likitokea uelekeo wa Ngarenairobi.