155 wajifungia Morogoro kusaka mwarobani somo la hisabati

Muktasari:
- Wakufunzi 155 wa somo la Hisabati kutoka vyuo vya Ualimu 35 vya Serikali wameanza mafunzo kazini ili kusaka suluhu ya changamoto ya ufaulu mdogo wa somo la hisabati kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kwa kuanzisha mafunzo maalumu kwa njia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).
Morogoro. Wizara ya elimu, sayansi na teknolojia imeanza kuzifanyia kazi changamoto zinazochangia ufaulu mdogo wa somo la hisabati kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kwa kuanzisha mafunzo maalumu kwa njia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Carolyne Nombo leo Jumane, Julai 11, 2023 amefungua mafunzo kazini kwa wakufunzi 155 wa somo la Hisabati kutoka vyuo vya Ualimu 35 vya Serikali yanayofanyikia mkoani Morogoro.
Profesa Nombo amesema mafunzo kwa wakufunzi hao ni moja ya utekelezaji wa lengo la Serikali katika kuleta mageuzi kwenye somo la hisabati na kwamba mradi huo umefadhiliwa na Serikali ya Canada.
Amesema mpango huo wa Serikali utaimarisha mbinu za ufundishaji na ujifunzaji wa somo la hisabati ikiwa pamoja na kutumia Tehama katika kipindi ambacho Serikali inatekeleza mageuzi ya elimu nchini.
Katibu mkuu huyo amesema katika kufanikisha mpango huo wa kuinua ufaulu wa somo la hisabati, tayari Serikali kupitia wizara hiyo ya elimu imewekeza kwenye ujenzi wa majengo mapya na kuimarisha miundombinu ikiwemo maabara na kuanzisha majengo mapya ya Tehama kwa kila chuo cha ualimu.
“Sisi sote tunafahamu kuna changamoto ya ufaulu katika somo la hisabati, mazingira ya kufundishia si mazuri hivyo Serikali yetu imeamua kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika vyuo vya Ualimu ili viweze kutoa walimu tarajali watakaofundisha somo hili kwa shule za msingi na sekondari,” amesema Profesa Nombo
Amesema tayari Serikali imewekeza kwa kujenga kituo cha hisabati katika Chuo cha Ualimu Morogoro na kimewezeshwa vifaa mbalimbali vya kisasa vya kitehama ikiwemo vishkwambi, kompyuta ambavyo kwa pamoja vinawezesha wakufunzi hao kujifunza hata wakiwa nje ya vituo vyao.
“Wakufunzi wote watapitishwa kwenye matumizi ya mifumo ya somo la hisabati, matumizi ya vishikwambi kwa ajili ya kufundishia na kujifunzia na kuwajengea mbinu za kufundisha hisabati kwa kutumia Tehama,” amesema.
Amesema baada ya mafunzo hayo wakufunzi hao watakwenda kuwawezesha walimu tarajali ambao nao watakwenda kufundisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kwa lengo la kuinua ufaulu wa somo hilo la hisabati.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo ya Ualimu, Huruma Mageni amesema wizara ya elimu inaendelea na utekelezaji wa kazi mbalimbali za mradi wa kuendeleza elimu ya ualimu (TESP) ikiwemo kutoa mafunzo kazini kwa wakufunzi wanaofundisha somo la hisabati.
Mageni amesema mafunzo hayo yanatolewa kwa wakufunzi wanaofundisha mafunzo ya ualimu wa ngazi ya Cheti na Diploma kutoka katika vyuo hivyo vyote 35 vya Ualimu vya Serikali ambayo yanatolewa kwa njia ya mtandano.
Naye Mratibu wa Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Ualimu, Cosmas Mahenge amesema mafunzo ya Hisabati kwa njia ya Tehama yanatolewa kwa wakufunzi kutoka kanda ya kaskazini, mashariki, nyanda za juu kusini, kanda ya ziwa, magharibi, kati na kusini kwa lengo la uboreshaji wa somo hilo.
Mkufunzi wa somo la Hisabati kutoka Chuo cha Ualimu Morogoro, Gloriana Kakuru amesema mafunzo hayo yatawasaidia kuwatia moyo hasa wanawake kuwa somo hilo sio gumu na wajiamini kuwa wanaweza ili kufanya vyema katika masomo ya hisabati na sayansi.
Amesema mafunzo hayo yatakuwa msaada kwao kama wakufunzi wanaowaandaa walimu na kutarahisisha kuandaa masomo na nyaraka za ufundishaji na ujifunzaji ikiwemo njia ya mawasiliano kwa kutumia majukwaa mbalimbali ya hisabati.